Vikwazo dhidi ya Iran: Marekani haiwezi kutuzuia kuuza mafuta, asema waziri

Dola za Marekani. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sarafu ya Iran imepoteza nusu ya thamani yake tangu mwezi Aprili.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Iran Javad Zarrif amesema kuwa Marekani haitaweza kuizuia Iran kuuza mafuta yake nje.

Mohammed Javad Zarrif aliambia gazeti la Iran kwamba malengo ya rais Trump ya kulazimu ulimwengu wote kutonunua mafuta ya Iran hayawezi kufua dafu.

Rais huyo wa Marekani alikwenda katika akaunti yake ya Twitter siku ya Jumanne na kutoa onyo kali kwa mtu yeyote anayeshirikiana na Iran kufanya biashara baada ya kuliwekea vikwazo taifa hilo.

Anajaribu kuilazimu Iran kukubali kuingia katika mktaba mpya, lakini Uingereza, Ufaransa , Urusi na China zimeahidi kuunga mkono makubaliano hayo walioafikia pamoja na Marekani 2015 na kuendelea kufanya biashara na Iran.

Rais Trump alijiondoa katika makubaliano hayo ambayo yaliilazimu Iran kupunguza vitendo vyake vya kinyuklia kwa lengo la kuondolewa vikwazo mnamo mwezi Mei.

Alisema kuwa mkataba huo ulifeli kuafikia malengo yake muhimu ya kuzuia Iran kutengeneza bomu la kinyuklia na hayakuangazia vitendo vya ukandamizaji vya Iran mbali na utengenezaji wa silaha za masafa marefu na kuunga mkono ugaidi.

Rais wa Iran Hassan Rouhani ambaye anasisitiza kuwa mpango wake wa kinyuklia ni wa amani, amemshutumu rais Trump kwa kuanzisha vita vya kisaikolojia na kukataa mazungumzo ya ana kwa ana na yeye iwapo vikwazo hivyo vitaendelea.

Siku ya Jumanne , Marekani ilirudisha vikwazo dhidi ya Iran ikilipiga marufuku taifa hilo katika ununuzi wa noti zake za dola, biashara ya Iran ya dhahabu na madini mengine pamoja na sekta ya magari.

Mnamo mwezi Novemba awamu ya pili ya vikwazo vikali zaidi vitawekwa dhidi ya waendesha bandari ya Iran, sekta ya kawi, uchukuzi wa majini pamoja na sekta ya uundaji wa meli.

Vikwazo dhidi ya kuuza mafuta na maswala ya ubadilishanaji wa fedha kati ya taasisi za kifedha za kigeni na benki kuu ya Iran pia zitaathiriwa.

Katika Ujumbe wa twitter , bwana Trump alionya, ''mtu yeyote anayefanya biashara na Iran hataruhusiwa kufanya biashara na Marekani . Nataka amani duniani sitaki sina mengi''.

Baadye bwana Zarrif alijibu katika mtandao wa twitter akisema: Kujionyesha na jumbe nyingi za Twitter zenye maneneo yenye herufi kubwa hakutabadilisha ukweli kwamba dunia imechoshwa na ukoloni wa Marekani.."

"Kusitisha biashara na Marekani na kuharbu kazi 100,000 hakututii wasiwasi, lakini ulimwengu hautafuata madikteta wanaotumia twitter. Uliza EU, Urusi, China na washirika wetu wengi wa kibishara''.

Katika mahojiano na gazeti la Iran yaliochapishwa siku ya Jumatano , Javad zarrif alisema kuwa lengo la utawala wa Trump kukatiza uagizaji wa mafuta kutoka taifa hilo halitaathiri chochote na haliwezekani

"Mataifa ambayo Marekani inajadiliana nayo wameambia Washington kwamba yataendelea kununua mafuta kutoka Iran'' , alielezea.

Bwana Zarrif amesema kuwa mataifa ya Ulaya ambayo yamesema kuwa yanaunga mkono makubaliano hayo ya kinyuklia yametaka mataifa mengini kuendelea kununua mafuta kutoka Iran ama hata kuanza kufanya hivyo wakati wa awamu ya pili ya vikwazo itakapotekelezwa.

Anasema kuwa mataifa hyao pia yalikuwa yamependekeza kuanzisha akaunti ya benki kuu ya Iran katika mabenki yao huko Ulaya, aliongezea.

''Kufuatia hatua yake , Marekani imetengwa''.

Muungano wa Ulaya pia umeanzisha sheria itakayolinda makampuni yake yanayofanya biashara na Iran dhidi ya vikwazo hivyo vya Marekani.

Hatahivyo afisa mmoja mkuu nchini Marekani amesema kuwa haina wasiwasi kwa sababu tayari makampuni mengi yameanza kuondoka nchini Iran.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii