Tendai Biti: Mwanasiasa wa Zimbabwe aliyemtangaza Chamisa kuwa mshindi na kutafuta hifadhi Zambia arejeshwa

Biti alikuwa ni waziri wa fedha kwenye serikali ya umoja iliyobuniwa baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2008 na ilisifiwa kwa kusaidia kuboresha uchumi. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Biti alikuwa ni waziri wa fedha kwenye serikali ya umoja iliyobuniwa baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2008 na ilisifiwa kwa kusaidia kuboresha uchumi.

Mwanasiasa wa cheo cha juu kwenye muungano wa upinzani nchini Zimbabwe MDC, Tendai Biti, amenyimwa hifadhi kwenye taifa jirani la Zambia.

Maafisa wa serikali ya Zambia wamemrejesha Biti hadi nchini Zimbabwe, licha ya kuwepo agizo la mahakama lililowazuia kufanya hivyo.

Mahakama kuu nchini Zambia ilikuwa imempa mwanasiasa huyo haki ya kuwasilisha ombi lake la kuomba hifadhi.

Lakini wakili wake Gilbert Phiri anasema Biti amekabidhiwa maafisa wa polisi wa Zimbabwe.

Polisi wa Zimbabwe wanamlaumu Bw Biti kwa kuchochea ghasia kufuatia uchaguzi wa wiki iliyopita.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Zambia Joe Malanji aliiambia BBC kuwa vigezo vyake kuomba hifadhi vilikuwa dhaifu.

"Alizuiwa eneo salama hadi pale aliporejeshwa Zimbabwe," waziri alisema.

Mapema wakili wake alisema mteja wake alikuwa amezuiwa kwenye mpaka na Zambia na mamlaka za Zimbabwe.

Ripoti nyingine za polisi wa Zambia zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii awali zilikuwa zinasema kuwa maafisa wa Zimbabwe walijaribu kumkamata Bw Biti baada ya yeye kuvuka na kuingia Zambia.

Mwanasiasa huyo wa upinzani akaomba msaada kwa sauti na karibuwasafiri 300 wa Zimbabwe wakawazuia maafisa wa usalama wa serikali kumkamata, kulingana na ripoti.

Maafisa wa Zambia kisha wakaingilia kati na kutishia kuwakamata maafisa wa Zimbabwe kwa kujaribu kutekeleza wajibu wao ndani ya ardhi ya Zambia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tendai Biti anadaiwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi

Kulikuwa na matumaini kuwa uchaguzi wa mwezi Julai ungeleta mabadiliko makubwa baada ya kumalizika kwa utawala wa Rais Robert Mugabe Novemba iliyopita.

Lakini wiki iliyopita watu 6 waliuawa baada ya jeshi kuingilia kati kuzima maandamano ya upinzani kwenye mji mkuu Harare.

Waandishi wa habari wanasema kuna hali ya hofu nchini Zimbabwe huku baadhi ya wanachama wa upinzani wakiingia mafichoni.

Tume ya uchaguzi ilitangaza kuwa Rais Emmerson Mnangagwa alishinda uchaguzi lakini muungano wa MDC unadai kuwa uchaguzi uliibwa.

Upinzani unasema mgombea wake Nelson Chamisa ndiye alikuwa mshindi na matokeo yalikarabatiwa

Biti alikuwa ni waziri wa fedha kwenye serikali ya umoja iliyobuniwa baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2008 na ilisifiwa kwa kusaidia kuboresha uchumi.

Tendai Biti ni Nani?

 • Tendai Laxton Biti alizaliwa tarehe 6 Agosti mwaka 1966 huko Dzivarasekwa, Harare na ndiye kifungua mimba wa familia ya watoto 6.
 • Kuanzia mwaka 1980 hadi 1985 alisomea shule ya upili ya Goromonzi ambapo aliteuliwa kawa kiranja mkuu mwaka 1985.
 • Alijiunga na chuo kikuu cha Zimbabwe kusomea sheria mwaka 1986 na kati ya mwaka 1988 na 1989 Biti akawa katibu mkuu wa chama cha wanafuzi kwenye chuo cha Zimbabwe
 • Baada ya kumaliza chuo kikuu alijiunga na kampuni ya mawakili ya Honey and Blackenberg, ambapo alikuwa mshirika mwenye umri mdogo zaidi akiwa na miaka 26.
 • Mwaka 1999 alisaidia kuanzisha chama cha MDC na akateuliwa kuwa mbunge wa eneo bunge la mjini Harare mwaka 2000.
 • Alikamatwa mwaka 2007 na wengine wengi akiwemo kiongoza wa MDC Morgan Tsvangirai baada ya mkutano wa maombi uliofanyika eneo la Highfiled mjini Harare.
 • Biti alichaguliwa tena kama mbunge eneo la Harare Mashariki machi mwaka 2008 na kulingana na matokeo rasmi alipata kura 8,377 dhidi ya za mpinzani wake 2.587 wa chama ZANU-PF.
 • Alikamatwa mwaka 2007 na wengine wengi akiwemo kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai baada ya mkutano wa maombi uliofanyika eneo la Highfiled mjini Harare.
 • Katika kipindi cha baada ya uchaguzi aliishi nje ya nchi hasusan Afrika Kusini pamoja na Tsvangirai kutokana na ghasia zilizokuwa zikiendelea hasa dhidi ya chama cha MDC.
 • Biti alirudi nchini Zimbabwe tarehe 12 Juni mwaka 2008 na akakamatwa mara moja kwenye uwanja wa ndege wa Harare ambapoa polisi walisema wangemfugulia mashtaka ya uhaini.
 • Tarehe 10 Februari mwaka 2009 kiongozi wa MDC na waziri mkuu Morgan Tsvangirai alitangaza uteuzi wa Biti kuwa waziri wa fedha kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 • Biti ni shabiki mkubwa wa klabu ya Arsenal na hutazama mechi nyingi kupitia runinga akiwa Zimbabwe na pia uhudhuria mechi na kutazamaa moja kwa moja mjini London.

Mada zinazohusiana