Mfahamu Emmanuel Ramazani Shadary, mrithi wa rais Joseph Kabila DR Congo

Emmanuel Ramazani Shadary Haki miliki ya picha PPRD

Rais Joseph kabila amemteua katibu wa kudumu katika chama tawala cha PPRD Emmanuel Ramazani kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi ujao wa mwezi Disemba.

Emmanuel Ramazani Shadary aliwahi kuhudumu kama waziri wa maswala ya ndani na katibu wa kudumu katika chama cha PPRD.

Anatoka mkoa wa Maniema uliopo mashariki mwa mkoa wa DR Congo.

Akiwa mzaliwa wa Kasongo 1960, alijifunza katika chuo kikuu cha Lubumbashi katika kitengo cha jamii, usimamizi na sayansi ya kisiasa ambapo alifuzu na shahada.

Baadaye alielekea katika chuo kikuu cha Kinshasa ambapo alikamilisha masomo yake ya awamu ya tatu ya sayansi ya kisiasa na uzimamizi.

Amekuwa akisomea shahada ya udaktari tangu 2015.

Akiwa baba ya watoto wanane, Shadary ana uzoefu mwingi wa kikazi.

Amekuwa naibu na mkurugenzi mkuu wa elimu ya juu na ile ya chuo kikuu, mbali na kuwa mwanaharakati wa mashirika ya kijamii mkoani Maniema.

Aliwahi kuhudumu kama naibu gavana wa Maniema {1998-2001) chini ya usimamizi wa rais Laurent Désiré Kabila, babaake Kabila.

Ni mwanzilishi mwenza chama cha ujenzi na demokrasia PPRD mwaka 2002, ambapo alikuwa katibu mkuu anayesimamia maswala ya uchaguzi na nidhamu kutoka 2005 hadi 2015.

Alichaguliwa naibu wa kitaifa katika eneo bunge la Kambarare mwaka 2006 na 2011.

Katika kipindi hicho, alikuwa mkurugenzi wa kampeni za urais za Joseph Kabila mkoani Maniema.

Pia aliwahi kuhudumu kama makamu wa rais wa tume ya PAJ bungeni kati ya 2006-2011, kabla ya kuchukua uongozi wa chama cha PPRD bungeni mbali na kuwa mshirikishi wa wabunge walio wengi katika bunge hilo hadi kufikia sasa.

Mnamo tarehe 17 May 2015, aliteuliwa naibu katibu mkuu wa chama cha PPRD na rais Joseph Kabila.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii