Maafisa ununuzi kutoka nchi 46 wakutana Tanzania

Maafisa Ununuzi wa Umma, hushughulika pia na manunuzi ya chakula katika Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa Ununuzi wa Umma, hushughulika pia na manunuzi ya chakula katika maeneo mbalimbali

Kongamano la nane la Kimataifa la Maafisa Ununuzi wa Umma linaloshirikisha washiriki takriban 370 kutoka nchi 46 linafanyika mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania, likijadili mafanikio na changamoto za ununuzi wa umma.

Akizungumza na BBC, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania, Dokta Hellen Bandio amesema lengo la mkutano huo pia ni kupata uzoefu kutoka sehemu nyingine duniani.

Katika mkutano huo wamezungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo rushwa.

Dkt Hellen amefahamisha kuwa kwa muda mrefu sasa sekta hii ya Ununuzi wa Umma imekuwa ikilalamikiwa kwa tuhuma za rushwa, na kwamba kwa sasa wamekuwa wakijaribu kuhakikisha kuna matumizi bora ya fedha za umma, hususan katika upande wa manunuzi.

''...Uzuri ni kwamba serikali ya Tanzania sasa hivi inachukia rushwa na yule ambaye anafanya mambo haya yuko matatani...''

Aidha amesema manunuzi katika serikali ni zaidi ya asilimia 70 na hivyo kama rushwa itakuwepo, mambo mengi ambayo wananchi wanapaswa kufanyiwa, yatashindikana.

Baadhi ya washiriki wa mkutanoi huo wamezungumzia pia rushwa inavyosumbua na kuangalia jinsi ya kuondoa kabisa.

Haki miliki ya picha ATLAS
Image caption Ramani ya Tanzania

Kutokana na sekta ya Ununuzi kuwa na umuhimu, Dokta Hellen amesema inapaswa kuhakikisha kuwa wale wanaofanya manunuzi wanatahiniwa kuhakikisha kuwa wana viwango na maadili yanayotakikana kufanya kazi yao vizuri.

''Hii sekta ni muhimu inawezekana usinunue vifaa lakini huduma utainunua, kama tutajenga barabara ina maana tutahitaji vifaa'' sasa hivi Tanzania ya viwanda, kama Tanzania ya viwanda ina maana kwamba vifaa vyote vitakavyohitajika vitanunuliwa.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania, Dkt Hellen Bandio amesema Tanzania iko katika maandalizi ya kutumia teknolojia ya kisasa katika matumizi ya umma kwa nchi nzima.

Amesema licha ya changamoto zitakazowakabili katika kufanikisha hilo, wako tayari kuzikabili.

Mada zinazohusiana