Tendai Biti: Rais Emmerson Mnangagwa asema alichangia mwanasiasa wa upinzani kuachiliwa huru kwa dhamana Zimbabwe

Tendai Biti Haki miliki ya picha AFP

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema mwanasiasa wa upinzani Tendai Biti ameachiliwa huru na mahakama baada ya yeye kuingilia kati.

Akiandika katika mtandao wa Twitter, kiongozi huyo wa Zimbabwe ametaka kuwepo kwa amani.

Lakini amesisitiza kuwa taratibu zaidi za kisheria zitafuata mkondo wake.

Bwana Biti alikamatwa baada ya kushutumiwa kuutangazia umma wa Zimbabwe kuwa chama cha upinzani MDC kimeshinda uchaguzi wa hivi karibuni, kitendo ambacho kinatajwa kuchochea vurugu kwa wananchi.

Image caption Alikamatwa kwa amri ya mahakama wakati akielekea Zambia kwa hifadhi

Biti ambaye alirejeshwa nchini Zimbabwe baada ya kujaribu kuingia Zambia, ni mwanasiasa wenye ushawishi mkubwa na waziri wa zamani wa fedha kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa na Rais wa zamani Robert Mugabe na aliyekuwa waziri mkuu hayati Morgan Tsvangirai.

Wakuu wa jeshi wateuliwa kuwa mawaziri Zimbabwe

Kurejeshwa kwake kulifuatia agizo la mahakama la kumtafuta popote alipo, baada ya tamko alilolitoa la ushindi wa chama cha upinzani kwenye uchaguzi mkuu uliomaliika hivi majuzi na kumuweka madarakani mwanasiasa mkongwe Emmerson Mnangagwa.

Image caption Kauli yake inatajwa kusababisha vurugu ambazo hata hivyo zilizuiliwa na jeshi la Zimbabwe

Seneta wa chama cha MDC David Coultart ameiambia BBC kuwa bwana Biti aliteswa wakati wa utawala wa rais wa zamani Robert Mugabe, na kwa sasa anahofia usalama wake hivyo ni vyema mahakama hata baada ya kumuachia impe ulinzi.

Awali mwanasheria wa Biti alisema maisha ya mwanasiasa huyo yapo hatarini nchini Zimbabwe kauli ambayo ilikanushwa vikali na waziri wa mamambo ya nje wa Zambia Joseph Malanji akisema serikali yake haiamini kama Biti anaweza kuwa katika hatari ndani ya nchi yake mwenyewe.

Tendai Biti ni Nani?

 • Tendai Laxton Biti alizaliwa tarehe 6 Agosti mwaka 1966 huko Dzivarasekwa, Harare na ndiye kifungua mimba wa familia ya watoto 6.
 • Kuanzia mwaka 1980 hadi 1985 alisomea shule ya upili ya Goromonzi ambapo aliteuliwa kawa kiranja mkuu mwaka 1985.
 • Alijiunga na chuo kikuu cha Zimbabwe kusomea sheria mwaka 1986 na kati ya mwaka 1988 na 1989 Biti akawa katibu mkuu wa chama cha wanafuzi kwenye chuo cha Zimbabwe
 • Baada ya kumaliza chuo kikuu alijiunga na kampuni ya mawakili ya Honey and Blackenberg, ambapo alikuwa mshirika mwenye umri mdogo zaidi akiwa na miaka 26.
 • Mwaka 1999 alisaidia kuanzisha chama cha MDC na akateuliwa kuwa mbunge wa eneo bunge la mjini Harare mwaka 2000.
 • Alikamatwa mwaka 2007 na wengine wengi akiwemo kiongoza wa MDC Morgan Tsvangirai baada ya mkutano wa maombi uliofanyika eneo la Highfiled mjini Harare.
 • Biti alichaguliwa tena kama mbunge eneo la Harare Mashariki machi mwaka 2008 na kulingana na matokeo rasmi alipata kura 8,377 dhidi ya za mpinzani wake 2.587 wa chama ZANU-PF.
 • Alikamatwa mwaka 2007 na wengine wengi akiwemo kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai baada ya mkutano wa maombi uliofanyika eneo la Highfiled mjini Harare.
 • Katika kipindi cha baada ya uchaguzi aliishi nje ya nchi hasusan Afrika Kusini pamoja na Tsvangirai kutokana na ghasia zilizokuwa zikiendelea hasa dhidi ya chama cha MDC.
 • Biti alirudi nchini Zimbabwe tarehe 12 Juni mwaka 2008 na akakamatwa mara moja kwenye uwanja wa ndege wa Harare ambapoa polisi walisema wangemfugulia mashtaka ya uhaini.
 • Tarehe 10 Februari mwaka 2009 kiongozi wa MDC na waziri mkuu Morgan Tsvangirai alitangaza uteuzi wa Biti kuwa waziri wa fedha kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 • Biti ni shabiki mkubwa wa klabu ya Arsenal na hutazama mechi nyingi kupitia runinga akiwa Zimbabwe na pia uhudhuria mechi na kutazamaa moja kwa moja mjini London.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii