Tanzeela Qambrani: Mwanamke mwenye asili ya Tanzania ateuliwa mbunge Pakistan na kuweka historia

Tanzeela Qambrani meets members of the public
Image caption Tanzeela Qambrani (kulia) anataka jamii yake iheshimiwe

Mwanamke mwenye asili ya Tanzania amekuwa wa kwanza wa asili ya Afrika kuteuliwa kuwa mbunge nchini Pakistan, na kutoa matumaini kwa watu wa jamii ndogo na maskini nchini humo yenye asili yake Afrika.

Tanzeela Qambrani, 39, aliteuliwa na chama cha Pakistan People's Party (PPP), cha waziri wa zamani Benazir Bhutto kuhudumu katika kiti kilichotengewa wanawake kwenye bunge la mkoa wa Sindh kusini mwa India.

Ana matumaini kuwa uteuzi wake baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita utasaidia kuondoa unyanyapaa ambao umekuwepo dhidi ya jamii ya Sidi, jina wanaloitwa watu wa asili ya Afrika wanaoishi maeneo ya pwani ya Makran na Sindh nchini Pakistan.

"Kama jamii ndogo iliyopotelea kwenye jamii kubwa za wenyeji, tumekuwa na wakati mgumu kudumisha mizizi yetu ya Afrika na tamaduni, lakini ningependa kuona kuwa jina Sidi linakuwa lenye heshima," Bi Qambrani ambaye mababu zake walitokea Tanzania aliiambia BBC.

Mwanamke huyo aliapishwa Jumatatu wiki hii na amenukiliwa na mtandao wa The News International akisema kwamba alijihisi kama Nelson Mandela.

Alivalia mavazi ya kitamaduni ya Kiafrika wakati wa kuapishwa kwake.

Watu wengi wa jamii ya Sidi walitokana na watumwa waliopelekwa India kutoka Afrika Mashariki na Wareno.

Wanahistoria wanasema mababu zao walikuwa pia wanajeshi, wafanyabiashara, madereva na mahujaji wa Kiislamu.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Watu wa Sidi wakiwa kwenye tamasha la kitamaduni

Walishika nyadhifa za juu wakati wa utawala wa Mughal lakini wakatengwa sana chini ya ukoloni wa Mwingereza.

Makadirio yanaonyesha kuwa idadi yao ni elfu kadha nchini Pakistan.

Walichanganyika na watu wengine lakini wao wamedumisha baadhi ya tamaduni zao. Huwa wanaandaa tamasha ambayo huchanganya baadhi ya imani za Kiislamu na mamba, na pia nyimbo zao huchanganya Uswahili na lugha ya wenyeji ifahamikayo kama Baluchi.

Jamii za Sidi pia huishi kwenye majimbo ya Karnataka, Gujarat na Andhra Pradesh nchini India.

Watu wa jamii ya Sidi ni wengi wilaya ya Lyari huko Karachi na wamekuwa wafuasi wakubwa wa chama cha PPP ambacho kwa sasa kinaongozwa na mtoto wake Benazir Bhutto, Bilawal Zardari Bhutto.

Hata hivyo hakuna mtu kutoka jamii ya Sidi aliwahi kuingia bungeni hadi Bw Bhutto Zardari alipomteua Bi Qambrani kwenye kiti maalum.

"Vile Colombus alivyogundua Amerika, Bilawal (mwanawe Benazir Bhutto) pia amewagundua watu wa jamii ya Sidi," alisema Bi Qambrani ambaye mababu zake waliingia Sidhi wakitokea Tanzania.

Haki miliki ya picha Tanzeela Qambrani
Image caption Mi Qambrani (wa pili kutoka kushoto) kiongozi wa PPP Bilawal Bhutto Zardari (wa pili kutoka kulia)

Chama cha PPP kilichukua nafasi ya tatu kwenye uchaguzi uliopita ulioshindwa na mcheza kriketi wa zamani Imran Khan wa chama cha PTI.

Bi Qambrani ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta ambapo ana shahada ya uzamili (shahada ya pili) katika somo la kompyuta kutoka chuo kikuu cha Sindh, Jamshoro.

Ameolewa na amejaliwa watoto watatu.

Dadake ameolewa Tanzania

Anatokea eneo la Matli katika wilaya ya Badin inayopatikana eneo la pwani katika mkoa wa Sindh. Amekuwa mtetezi wa elimu kwa wasichana.

Baba yake Abdul Bari alikuwa ni wakili na mama yake ni mwalimu mstaafu.

Familia yake imedumisha uhusiano wake na Afrika; mmoja wa dada zake aliolewa nchini Tanzania.

Mwingine mumewe anatokea nchini Ghana.

"Dadangu alipoolewa na mwanamume kutoka Ghana, vijana wa hapa na wageni kutoka Ghana walicheza kwa madaha na kusherehekea kijijini," anasema.

"Walicheza ngoma za asili za Wasidi na pia ngoma za Mogo ambazo hudaiwa kutoka Ghana lakini kiasili zilichezwa kwetu nyumbani. Haungeweza kumtofautisha mchezaji ngoma wa Sidi na Mwafrika."

Sawa na watu wengine wa jamii za Sidi huko Sindh, Tanzeela Qambrani amehusishwa kwa muda mrefu na chama cha PPP. Ana ujuzi wa siasa kwa kuwa ashahudumu kama diwani tangu 2010.

Lakini anasema kuwa anatambua kuchukua wadhifa kwenye bunge la mkoa kutatoa changamoto mpya hasa kwa jamii yake.

"Tayari ninahisi uzito," alisema. "Mimi ni Msidi, na watu hawa wa tabaka la kati, la chini na la wafanya kazi wanajua kuwa mimi ni mmoja wao. Ni hii inamaanisha kuwa kutakuwa na matarajio makuu."

Mada zinazohusiana