Bobi Wine: Mbunge wa Uganda anayemkaidi Museveni

Bobi wine Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wine anasema Museveni hazingatii maadili yaliomuongoza kwa wakati mmoja

Mwanamuziki wa Uganda aliyegueka kuwa mwanasiasa Bobi Wine amepigwa na vikosi vya usalama na hawezi kuzungumza wala kutembea , mawakili wake wanasema.

Mbunge huyo wa upinzani amefikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi katika mji wa kaskazini Gulu, alikoshtakiwa kwa mashtaka mawili ya kumiliki silaha kinyume cha sheria na shtaka moja la kupatikana na silaha , lakini sio uhaini kama ilivyoripotiwa awali.

Alikamatwa baada ya gari lililokuwa kwenye msafara wa rais Museveni kushambuliwa Jumatatu katika mji wa Arua, kufuatia kuwadia uhaguzi mdogo ulioshindaniwa vikali.

Dereva wa Wine baadaye alipigwa risasi na kuuawa, katika kinachotajwa na mbunge huyo kuwa ni jaribio la kumuua yeye.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakosoaji wanasema Bobi Wine amelenga kushinikiza umati tu lakini hajawasilishwa miswada bungeni kwa masuala anayoyapigania katika kampeni

Mshirika wake Kassiano Wadri, aliyeshinda uchaguzi huo wa Arua, awali alishatkiwa na uhaini akiwa pamoja na wengine 31.

Serikali haijatoa tamko kuhusu tuhuma kwamba Bobi alishambuliwa akiwa kizuizini.

Mbunge huyo mwenye miaka 36 kwa muda mrefu amekuwa akiikosoa wazi serikali ya Uganda.

"Wakati viongozi wetu wamekuwa wapotoshaji na watesaji. Wakati uhuru wa kujieleza unalengwa na kukandamizwa, nafasi yetu inakuwa ni ya upinzani."

Hayo ni maneno katika wimbo unaoitwa Situka, iliyo na maana sawa na Zinduka, aliouimba Wine kufuatia kuwadia kwa uchaguzi mkuu mnamo 2016.

Alitumia wimbo huo kuwashinikiza Waganda wawajibike kupambana na rushwa na ukandamizaji nchini mwao.

Kwa wakati huo wasanii wengi nchini wa zamani walimuunga mkono raisi Yoweri Museveni kuchaguliwa tena lakini Wine alikataa kuingia kwenye mkondo huo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bobi Wine aliwashinda wagombea kutoka kwa chama kikuu cha siasa katika uchaguzi mdogo mwaka jana na kuibuka kuwa mbunge

Ni hapo watu walishuku kwamba huenda Wine alitaka kuingia katika siasa.

Bobi Wine ni nani?

Nyota huyo wa mtindo wa Afrobeats aliingia katika taaluma ya muziki katika miaka ya 2000, hna anaelezea kipaji chake kuwa ni cha kuelimisha na kuburudisha. Mojawapo ya vibao vyake vya awali Kadingo, inahusu usafi wa mwili.

Jina lake rasmi Wine, ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka jana wilayani Kyadondo mashariki, Uganda ya kati.

Aliwashinda wagombea kutoka chama tawala National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).

Baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.

"Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki...Ninataka siasa zitulete pamoja... jinsi muziki ufanyavyo."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wine anajiita "Ghetto President" na anaungwa mkono pakubwa na vijana

Ufuasi wa Vijana

Mchambuzi wa kisiasa Nicholas Sengoba anasema uchaguzi mdogo wa Arua ulioshindwa na mgombea aliyeungwa mkono na Wine ulikuwa ni wa 'kufa au kupona kwa Museveni'.

"Chama chake kitawaza iwapo sasa huu ni msururu. Bobi Wine sasa amemshinda Museveni na kiongozi wa upinzani Kizza Besigye mara nne'' katika uchaguzi mdogo.

"Bobi amepata ufuasi kwa nemba yake ya 'nguvu za watu', na ananuia kushinikiza na kupanga liwe vuguvugu," anaongeza.

Mchambuzi wa kisiasa Robert Kirunda anasema mvuto wa Wines unatokana na kuwepo 'pengo la uongozi' Uganda.

"Kuna vijana wengi Uganda ambao hawana haja ya kujua vita vya kihistoria vilivyoiingiza NRM uongozini, au ukaidi wa upinzani mkuu. Wengi wanataka ajira na wanahisi uchumi hauwasaidi."

Kirunda anasema Wine 'anapigia upatu sana'. "Anaweza kushinikiza watu pakubwa, lakini bado hajapata nguvu kama alizonazo Besigye katika upinzani".

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii