Kifo cha Annan: Viongozi nchini Kenya watuma rambi rambi zao

Annan alitoa mchango mkuwa kwa kuleta mapatano nchini Kenya baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Annan alitoa mchango mkuwa kwa kuleta mapatano nchini Kenya baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Viongozi mbali mbali hasa nchini nchini Kenya wametoa rambi rambi zao kufuatia kufariki kwa aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataiafa Kofi Annan.

Annan alitoa mchango mkuwa kwa kuleta mapatano nchini Kenya baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

"Nimesikitika kusikia kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mshindi wa tuzo la Nobel Kofi Annan ameaga dunia". alisema rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

"Natuma risala zangu za rambi rambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa marehemu. Nawaombea faraja wakati huu wa maombolezo.

"Tunaomba Mwenyezi Mungu aipe jamaa, ndugu na marafiki uwezo na neema ya kuhimili msiba huo. aliongeza Rais Kenyatta.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Kenyatta alisema amesikitika kusikia kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mshindi wa tuzo la Nobel Kofi Annan ameaga dunia

Kofi Annan alihudumu kama Katibu Mkuu wa saba wa Umoja wa Mataifa kwa vipindi viwili kuanzia mwaka wa 1997 hadi 2006.

Kwa upande wake kiongozi wa upnzani nchini Kenya Raila Odinga ametuma rambi rambi na kuelezea kushangazwa ni kifo cha Annan.

"Nchini Kenya bado tuna kumbukumbu za Annan ambaye aliingilia kati na kuisaidia nchi yetu isitumbukie kwenye ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007". Alisema Odinga.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Odinga alimkumbuka Annan kwa mchango alioutoa kwa amani ya duniani na hasa kwa afrika

Odinga alimkumbuka Annan kwa mchango alioutoa kwa amani ya duniani na hasa kwa afrika katika demokrasia, kuheshimiwa haki za binadamu na maendeleo ya kiuchumi na amani.

Alisema Annan alielewa vyema na akaiongoza dunia kufahamu umuhimu wa haki za binadamu kwa amani na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Odinga alisema kifo cha Annan ni pigo kubwa kwa kuheshimiwa haki za binadamu kote duniani.