Trump: Mkiniondoa madarakani masoko yataporomoka na mtakuwa maskini

US President Donald Trump at an awards ceremony at the White House, 22 August 2018

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amejibu uvumi kuwa anaweza kuondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani naye kwa kuonya kuwa uchumi utaharibika

Wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha Fox & Friends alisema masoko yataporomoka na "kila mtu atakuwa maskini".

Alikuwa akizungumza baada ya Michael Cohen, wakili wake wa zamani kukiri kuvunja sheria za uchaguzi na kusema alishauriwa kufanya hivyo na Trump.

Si kawaida kwa Trump kuzungumzia suala la kutolewa mamlakani.

Waandishi wa habari wanasema haiwezekani kuwa wapinzani wa Trump watajaribu kumuondoa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye kabla ya uchaguzi wa kati ya muhula wa mwezi Novemba.

Ni kwa nini Trump anasema kuwa masoko yataporomoka?

"Sijui ni kwa njia gani mtamtoa madarakani mtu ambaye amefanya kazi nzuri," Trump alikiambia kipindi cha Fox and Friends.

"Ninawaambia hivi, ikiwa nitaondolewa nafikiri masoko yataporomoka, nafikiri kila mtu atakuwa maskini."

Trump alitetea malipo kwa wanawake wawili na kusema hakuwa anawajua wakati huo.

Matamshi yake yanaenda kinyume na taarifa zilizotolewa mapema na Cohen ambapo alisema kuwa Rais Trump aliimuagiza kufanya malipo hayo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Cohen

Mwezi Julai Cohen alitoa kanda ya sauti yake na Trump wakizungumzia moja ya malipo hayo kabla ya uchaguzi

Cohen anasem alifanya malipo hayo kwa wanawake wawili wakati wa kampeni ya urais ya mwaka 2016.

Wanawawe hao wawili wanatajwa kuwa manyota wa filamu za ngono Stormy Daniels na Karen McDougal, wote walidai walikuwa na uhusiano na Trump

Lakini Trump alisisitiza kuwa malipo hayo hayakukiuka sheria za uchaguzi.

Alisema malipo hayo yalitoka kwake mwenyewe na sio kutoka kwa kampeni lakini hakufahamua kuyahusu hadi baadaye.

Malipo hayo yalivunja sheria?

Malipo hayo hayakuripotiwa kwa tume ya uchaguzi wakati wa kampemi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Stormy Daniels (kushoto) na Karen McDougal (kulia)

Swali ni ikiwa malipo hayo yalifanywa kulinda jina la Trump kama mgombea wa urais.

Chini ya sheria za uchaguzi nchini Marekani malipo yote yanayofanywa kwa lengo la kushawishi uchaguzi ni lazima yaripotiwe.

Ikiwa Bw Trump atashtakiwa kwa pesa hizo, bila kwa kutumia mahakama za kawaida kwa sababu ni rais, lakini kwa kupitia bunge kwa njia ya kura ya kutokuwa na imani naye -wachunguzi ni lazima watahitaji kubaini kuwa kweli Trump alimpa Cohen pesa hizo kwa minajili ya uchaguzi.