Kwa Picha: Mkutano wa Uhuru Kenyatta na Donald Trump White House Marekani

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Jumatatu alikutana na Rais Donald Trump wa Marekani katika Ikulu ya White House na akaiomba nchi ya Marekani kuongeza zaidi biashara na uwekezaji wake katika bara la Afrika.

Kenyatta na Trump

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Rais Kenyatta na mwenyeji wake Trump pia walikubaliana kuimarisha ufungamano wa Kenya na Marekani katika udumishaji wa amani na usalama hasa katika eneo la upembe wa Afrika.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

"Tumekuwa na ushirikiano mzuri na wa kipekee na Marekani katika masuala ya usalama na ulinzi, hasa katika harakati za kukabiliana na ugaidi. Muhimu zaidi tuko hapa kuboresha ufungamano wetu katika biashara na uekezaji, " alisema Bw Kenyatta.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Rais Trump alisema Kenya na Marekani zitaendelea kushirikiana kuimarisha ufungamano wao katika biashara, uekezaji na usalama.

"Tunafanya shughuli nyingi za utalii, biashara na ulinzi. Na kwa wakati huu tunajibidiisha kuboresha usalama," alisema Rais Trump. "Tunafurahia sana kuwa nawe hapa."

Chanzo cha picha, Ikulu, Kenya

Viongozi hao wawili walijadiliana kuhusu safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York zitakazoanza mwezi Oktoba mwaka huu.

Walikubaliana kwamba safari hizo za ndege zitaimarisha zaidi utalii na biashara kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Walitoa mfano wa Mkataba wa Nafasi na Ustawi wa Afrika maarufu kama Mkataba wa AGOA kama moja wapo wa nyanja zitakazonufaika na safari hizo za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Mapema walipowasili katika Ikulu ya White House, mjini Washington DC, saa nane alasiri saa za Marekani ambapo ilikuwa saa tatu usiku Afrika Mashariki Kenya, Rais Kenyatta na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta walilakiwa na wenyeji wao Rais Trump na Mkewe Melania Trump.

Chanzo cha picha, Ikulu, Kenya

Chanzo cha picha, Ikulu, Kenya

Baada ya mapokezi rasmi, Rais Trump alimualika Rais Kenyatta kuingia katika afisi ya Oval kwa mashauri ya ana kwa ana kabla ya kujiunga na jumbe zao kwa mashauri kuhusu nchi hizi mbili katika chumba cha masuala ya baraza la mawaziri.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Vile vile, Mke wa Marekani Melania Trump na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta walifanya mashauri ya faragha katika chumba cha masuala ya kidiplomasia katika upande wa Magharibi wa Jengo la White House.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Ziara ya kihistoria ya Rais Kenyatta katika Ikulu ya White House na kufanya mashauri ya ana kwa ana na Rais Trump ni ya tatu kufanywa na kiongozi wa Afrika.

Wengine ambao wamewahi kufanya hivyo ni Rais Abdel-Fattah el-Sisi wa Misri mnamo mwezi April mwaka jana na Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria mnamo mwezi April mwaka huu.

Kabla ya ziara yake katika Ikulu ya White House, Rais Kenyatta alikutana na kuhutubia wanachama wa Baraza la Kibiashara la Uelewano wa Kimataifa na akawahimiza watumie nafasi inayotokana na nguzo nne za ajenda kuu ya maendeleo kwa kuongeza uekezaji nchini Kenya.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Kwa mujibu wa ikulu, mashauriano hayo kati ya Rais Kenyatta na Rais Trump yanaimarisha zaidi nguzo nne ya ajenda kuu ya maendeleo ya Rais Kenyatta na vile vile kuchochea vita dhidi ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi nchini humo.

Chanzo cha picha, IKULU, Kenya

Picha zote: Ikulu, Kenya