Baphomet: Sanamu ya shetani inayozua utata Marekani

Rannie Rodil akiigiza Baphomet katika tamasha ya Son Of Monsterpalooza 2013 katika uwanja wa ndege wa Burbank Airport Marriott on October 12, 2013 in Burbank, California. (Photo by Albert L. Ortega/Getty Images)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rannie Rodil akiigiza Baphomet katika tamasha ya Son Of Monsterpalooza 2013 mjini Burbank, California.

Binadamu tangu zama za kale amekuwa akijenga, kuchonga na kuweka sanamu za aina nyingi kwa sababu mbalimbali.

Baadhi hutumiwa kuwaenzi watu maarufu na kuwakumbuka, na nyingine huabudiwa kama miungu.

Kwa muda mrefu hata hivyo, imekuwa ni nadra kuona sanamua ambayo moja kwa moja inahusishwa na shetani au ibilisi.

Lakini ukifika Marekani, mambo ni tofauti.

Kuna sanamu moja kubwa ya shaba ambayo inahusishwa na ushetani.

Ni sanamu ya, Baphomet ni kiumbe mwenye kichwa kinachofanana na cha mbuzi lakini ameongezwa maungo ya ajabu.

Ni kiumbe huntha mwenye mabawa, na kwenye sanamu hiyo inayotumiwa kwa sasa huoneshwa akiwa na watoto wawili wanaotabasamu.

Sanamu inayotumiwa kwa sasa ina urefu wa karibu futi 9, na iligharimu $100,000 (£64,000) kuitengeneza.

Sanamu hii imekuwa ikitumiwa kuwapiga vita wale walio na imani za Kikristo na imani nyingine zenye kumcha Mungu mmoja. Ni sanamu hii ambayo imekuwa ikitumiwa kuendesha vita dhidi ya kuwekwa kwa sanamu za Kikristo na dini nyingine katika majengo maarufu, bustani na maeneo ya umma nchini Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Agosti 17, sanamu hiyo ya kiumbe anayefahamika kama Baphomet ilipelekwa katika jimbo la Arkansas anakotoka rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Wanaotumia sanamu hiyo ni watu wa kundi linalofahamika kama Satanic Temple (Hekalu la Shetani) ambalo ni kundi la 'kidini' na kisiasa ambalo hupinga kuingizwa kwa dini katika masuala ya serikali.

Kundi hilo liliandaa maandamano ya watu 150 waliyojumuisha waabudu shetani, watu wasioamini Mungu yupo na Wakristo pia.

Maandamano hayo yalifanyika nje ya jengo lililo makao makuu ya jimbo la Arkansas katika mji wa Little Rock.

Walikuwa wamekerwa na hatua ya kuweka sanamu ya Mnara wa Amri Kumi za Mungu katika uwanja wa makao makuu hayo.

Satanic Temple walisema sanamu hiyo inakiuka Sheria ya Kwanza ya Marekebisho ya Katiba nchini Marekani ambayo huzungumzia uhuru na haki za kidini.

"Ikiwa utakubalia kuwepo kwa sanamu ya dini moja basi kunafaa kuwa na uhuru kwa wengine kuweka sanamu za kidini, na ukizuia basi kusiwe na sanamu yoyote ile," mwanzilishi mwenza wa tawi la Satanic Temple katika jimb la Arkansas Ivy Forrester alinukuliwa na wanahabari siku hiyo ya maandamano.

Chanzo cha picha, Matt Anderson

Maelezo ya picha,

Sanamu ya Baphomet inayotumiwa na Satanic Temple

Ndoto yao ni kuwa na sanamu ya kudumu, lakini siku hiyo hawakuruhusiwa na sheria kuiweka kwa muda mrefu. Kuna sheria ya Arkansas ya mwaka 2017 inayohitaji sanamu ya kuwekwa maeneo ya serikali iwe na udhamini wa mbunge ambaye atawasilisha mswada iidhinishwe kupitia bunge.

Sanamu hiyo ya Mnara wa Amri Kumi za Mungu ilidhaminiwa na mwanasiasa wa Republican, Seneta Jason Rapert. Hata hivyo, chini ya saa 24 baada ya kuwekwa, mwanamume mmoja alivurumisha gari na kuugonga mnara huo na kuubomoa.

Maandamano ya Satanic Temple Arkansas yalisababisha kuandaliwa kwa maandamano mengine ya kuwapinga yaliyoandaliwa na makundi ya Kikristo na wanachama wa Republican. Wakristo walikuwa wamebeba karatasi zilizokuwa na ujumbe kutoka kwa Biblia.

Satanic Temple waliwasilisha ombi la kushirikishwa kwenye kesi ya kupinga mnara huo wa Amri Kumi za Mungu iliyowasilishwa na shirika la haki za kiraia la American Civil Liberties Union, lakini kundi hilo limewasilisha ombi kutaka wasishirikishwe kwenye kesi hiyo.

Sanamu ya Detroit

Sanamu hiyo ya Baphomet ilizinduliwa mara ya kwanza katika mji wa Detroit, Michigan.

Mipango ya kuuweka nje ya makao makuu ya jimbo la Oklahoma ambapo kulikuwa kumewekwa mnara mwingine wa Amri Kumi za Mungu mwaka 2015.

Mnara huo ulizinduliwa 25 Julai mwaka huo, ambapo kupitia taarifa, Satanic temple walisema: "Tulichagua Baphomet kwa sababu ni kiumbe ambaye huhusishwa na Shetani na maana inayohusishwa naye inafaa sana akiwekwa kando na sanamu inayowakilisha dini nyingine."

Sherehe ya kuuzindua ilikuwa ya faragha, na ukumbi uliotumiwa uliwekwa siri kubwa kwani Wakristo walikuwa wameandamana awali kuipinga mjini. Picha zilizopakiwa kwenye Facebook zilionyesha uzinduzi wake ulifanyika karibu na Mto wa Detroit.

Kabla ya uzinduzi huo kufanyika, waumini takriban 200 walihudhuria ibada ya misa katika kanisa la St. Joseph mjini humo kupinga sanamu hiyo. Wengine 50 walifanya maombi mjini katika eneo ambalo awali Satanic Temple walikuwa wamepanga kuuzindulia mnara huo hapo.

Mwanamume yule yule aliyeuharibu mnara wa Arkansas anadaiwa kufanya vivyo hivyo na kuubomoa mnara mwingine kama huo wa Amri Kumi za Mungu nje ya makao makuu ya jimbo la Oklahoma.

Satanic Temple walisitisha juhudi zao za kutaka kuweka sanamu ya Baphomet huko baada ya Mahakama ya Juu ya Oklahoma kuamua kwamba Sanamu ya Mnara wa Amri Kumi za Mungu ilikuwa imewekwa kinyume cha sheria, hivyo wakawa wameshinda vita bila kupigana.

Mahakama ilisema ni kinyume cha sheria kutumia mali ya umma kwa manufaa ya dini yoyote ile.

Chanzo cha picha, Chris Switzer/Facebook

Maelezo ya picha,

Waliohudhuria sherehe ya uzinduzi walihudhuria kwa mwaliko

Jina Baphomet lilitoka wapi na asili yake wapi?

Jina hili asili yake ni enzi ya kukomesha uasi katika Kanisa Katoliki katika miaka ya 1100, kwa Kiingereza Inquisition, na kuteswa kwa wapiganaji wa kidini kwa jina Knights Templar waliokuwa wanateswa ili wafichue siri zao na wakubali kuifuata dini kwa mujibu wa viongozi wa kanisa wa wakati huo.

Kwa mujibu wa waandishi wa enzi za vita vya kidini maarufu kama Crusade, wapiganaji hao walikiri kumuabudu miungo wa wapagani kwa jina Baphometh.

Baadhi ya wasomi hata hivyo huamini kwamba "Baphometh" ni upotoshaji wa jina "Mahomet" - ambalo hutumiwa kumrejelea Nabii Muhammad, jambo linalozua utata zaidi.

Lakini kadiri miaka ilivyosonga na mafumbo na siri kuwahusu tata na Knights Templar kuzidi, ndivyo ufafanuzi wa neno hilo na maana yake ulivyozidi kutofautiana.

Moja ya ufasiri wa neno hilo unapatikana katika kitabu cha Da Vinci Code chake Dan Brown ambapo, neno Baphomet limefafanuliwa na kutafsiriwa kama "Sophia" au busara.

Baphomet kwa mujibu wa Levi

Chanzo cha picha, Other

Picha maarufu zaidi ya Baphomet ilichorwa na mwanamizungu wa Ufaransa Eliphas Levi mwaka 1856 katika kitabu chake cha Transcendental Magic: Its Doctrine and Ritual.

Alichora kiumbe huntha mwenye mabawa na mwenye pembe na mwenge ulio katikati ya pembe hizo kichwani.

Kuna mchoro pia wa pembe nane kwenye paji la uso.

Mikononi kumeandikwa maneno ya Kilatino SOLVE (tenganishwa) na COAGULA (fungamanisha) - ambazo ni nguvu za kuunganisha na kutenganisha ambazo zilitwaliwa kutoka kwa Mungu.

Mchoro wa Levi ulihamasisha zaidi sanamu inayotumiwa na Satanic Temple.

Ni jinsia mbili kwa pamoja, nusu mnyama na nusu binadamu.

Saluti ya vidole viwili

Sanamu hiyo ina vidole viwili vilivyoelekezwa juu mkono wa kulia na viwili vinavyoelekezwa chini mkono wa kushoto, maana yake "kama ilivyo juu, na chini iwe pia".

Maneno hayo na ishara hiyo ya vidole ni maarufu miongoni mwa wenye kuamini katika mizungu na mafumbo.

Chanzo chake ni kazi za kale za msomi Hermes Trismegistus, ambaye vitabu vyake vilikuwa maarufu sana enzi ya Kipindi mwamko-sanaa na mageuzi ya kidini, maarufu kama Renaissance and Reformation barani Ulaya.

Maneno hayo pia hutumiwa kuhusiana na sayansi, vitu vyote na Mungu, lakini Levi aliandika kwamba kwa kutumia ishara hiyo, Baphomet wake alikuwa anaashiria kuwiana sawa kwa fadhila na haki.

Watoto wawili

Lucien Greaves, msemaji wa Satanic Temple anasema lengo lao ni kwamba watoto watatazama kazi hiyo ya sanaa kama salama, isiyofaa kuzua wasiwasi wowote.

"Sura ya mbuzi huyo haioneshi chochote. Si ya kishetani wala ya kutisha - kama wanavyodai baadhi ya watu - ukiitazama bila kuongozwa na mzigo wa utamaduni."

Lakini watoto hawafai kumuoogopa Shetani?

"Sifikiri watoto wanaokutana na sanamu hii bila kutiwa hofu na propaganda wanaweza kuona chochote cha kuwatia wasiwasi," anasema Greaves.

"Lakini si kwamba tunapinga kuwaingiza watoto kwenye mitazamo ya kidini. Mara nyingi watoto hulazimishwa kuingia kwenye dini. Hilo ni jambo hatutaki kulifanya kamwe."

Caduceus

Kwenye tumbo la Baphomet kuna ishara ya kale ya Kigiriki ya nyoka wawili walio kwenye fimbo - fimbo ambayo ilibebwa na Hermes na maafisa wa kueneza matangazo au kutoa matangazo rasmi waliotumiwa kutoa matamko rasmi.

Ishara hiyo kwenye sanamu hiyo inaashiria biashara, mashauriano na kutendeana, na iliingizwa kwenye Baphomet na Levi.

"Kwetu ni ishara ya maridhiano ya vitu viwili tofauti - kwa mfano kuwa na sanamu ya Kishetani karibu na sanamu ya Kikristo," anasema Greaves.

"Tunafikiri ni ujumbe wenyenguvu sana kuwa na sanamu hii ikiwa karibu na sanamu ya Amri Kumi za Mungu. Unaweza kuwa na mambo mawili tofauti kwa pamoja bila mzozo."

Maziwa

Baphomet wa Levi alikuwa huntha mwenye maziwa, lakini "tuliyaondoa maziwa hayo" anasema Greaves. Anasema hakutana wajipate kwenye mdahalo kuhusu jinsia ya kiumbe huyo wao jambo ambalo lingewafanya watu kupoteza maana halisi.

Badala yake anasema watoto wawili, mvulana na msichana, ndio wanaowakilisha jinsia.

'Pentagram'

Chanzo cha picha, Satanic Temple

Maelezo ya picha,

Mchoro wa awali wa sanamu hiyo

Kwenye paji la uso la Baphomet na kwenye kiti cha enzi alichokikalia kuna mchoro wa nyota ya pembe tano, ishara ambayo mara nyingi hutambuliwa kama ishara ya shetani.

Mara nyingi huonekana ikiwa imepinduliwa.

Msalaba wa Peter pia hupinduliwa.

Greaves anasema lengo lao ni kuwafanya watu wabadilishe mtazamo wao na kuacha kuongozwa na waliyofunzwa na utamaduni wao. Waangazie mambo kwa kuzingatia ushahidi uliopo.

Anasema mtazamo huo huwazuia watu kuchukua msimamo huru kuhusu masuala kama vile ndoa za wapenzi wa jinsia moja na haki za kutoa mimba pamoja na huduma nyingine za uzazi wa mpango.

Chanzo cha picha, Matt Anderson/Facebook

Mwenge kati ya pembe

"Mwenge wa maarifa ndio kama upembe wa kati - na inatukuza juhudi za kutafuta elimu na maarifa. Tunathamini hilo sana," anasema Greaves.

Levi mwenyewe aliandika kwamba mwenge wa maarifa uolikuwa unawaka katikati ya pembe za Baphomet ni mwanga wa kusawazisha vitu vyote. Ni taswira ya roho iliyo juu ya vitu vyote vinavyoonekana, kama zilivyo ndimi za moto, ingawa bado imeunganishwa na vitu hivyo, mfano moto unavyoendelea kung'aa juu ya mafuta au kijiti.

Maandiko

Kulikuwa na mpango wa kuongeza maandiko kwenye mchoro wa nyota ya pembe tano ya moja ya nguzo saba kuu za Satanic Temple: "moyo wa huruma, busara na haki unafaa daima kuongoza zaidi ya neno lililoandikwa au kutamkwa."

Chanzo cha picha, Matt Anderson/Satanic Temple

Nyuma ya sanamu hiyo, kutakuwa na nukuu kutoka kwa kitabu cha Cain chake Lord Byron unaosema: "Kisha, nani alikuwa Ibilisi? Yule hangekuruhusu wewe uishi milele, au yule ambaye angelikuumba uishi milele, katika raha na nguvu za elimu na maarifa?"

Satanic Temple ndio nani?

Kwa mujibu wa tovuti yao Satanic Temple wanaamini kwamba "kimsingi watu kuteseka au kuumia ni vibaya, na chochote kile kinachopunguza madhilana mateso ni kizuri."

Hawaamini katika kutenda mabaya.

Wanasema: "Huwa tunakumabtia kukufuru kama njia halali ya kujieleza na kuonyesha uhuru wa mtu binafsi dhidi ya imani za kitamaduni zisizo na tija."

"Msimamo wa Satanic Temple ni kwamba dini inaweza, na inafaa kutenganishwa na ushirikina. Hivyo basi, huwa hawaendelezi imani katika Shetani binafsi.

"Kukumbatia jina la Shetani ni kukumbatia mtazamo wa kutumia fikira na kujindoa kutoka kwa mfumo wa kuamini katika nguvu za kipekee za kutoka nje ya dunia na utamaduni uliopitwa na wakati wenye msingi wake katika ushirikina."

Unaweza kusoma pia: