Tundu Lissu: Upinzani haujawahi kushambuliwa kama unavyoshambuliwa sasa Tanzania

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu

Ni Takriban miezi minane sasa tangu mwanasiasa wa upinzani na Mbunge wa Singida Mashariki nchini Tanzania Tundu Lissu kuwepo nchini Ubelgiji kwa ajili ya kupata matibabu.

Kwa sasa mwanasiasa huyo anasema anataka kurudi nyumbani na kurejea katika shughuli zake za kisiasa kwa kuwa yeye bado ni mbunge na anahitajika kuwahudumia wananchi waliomchagua kwa kipindi cha miaka mitano.

Katika mazungumzo yake na mwandishi wa BBC, Zuhura Yunus ambaye alimtembelea nchini humo ,Tundu Lissu alibainisha hali ya upinzani nchini Tanzania kuwa ina mabadiliko makubwa tofauti na miaka ya nyuma.

Mwanasiasa huyo alidai kwamba wakati wa utawala wa rais Jakaya Kikwete , yeye alikuwa mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani kwa kipindi cha miaka mitano lakini hakuwahi kutishiwa.

Maelezo ya picha,

Tundu Lissu akizungumza na mwandishi wa BBC, Zuhura Yunus

Na katika kipindi chote cha miaka kumi ya uongozi wa Kikwete upinzani ulikuwa na makelele kweli kweli lakini haukuwahi kukutana na vitisho vya hali wanayoiona sasa.

Hali ilikuwa vivyo hivyo hata wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa licha ya kwamba alikuwa hajawa mbunge bado.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli

Tofauti na hali ambayo wanaiona sasa ambapo akijichukulia mfano yeye tangu Rais John Magufuli aingie madarakani kwa kipindi cha miaka miwili tayari amepigwa risasi 16 na amelazwa hospitalini miezi kumi na moja .

Amesema hata ukiangalia katika mazingira ambayo chama chao cha Chadema kinakumbana nayo kwanza inaanzia kwa msaidizi wa mwenyekiti wa chadema hajulikani alipo tangu mwezi Novemba mwaka 2016 mpaka leo hii, na mwenyekiti, katibu mkuu wa chama, naibu makatibu wakuu wa chama wa Tanzania bara na Zanzibar pamoja na wabunge kadhaa akiwemo yeye mwenyewe - wana mashtaka mahakamani kwa uchochezi, kumsema rais vibaya na maandamano.

"Upinzani haujawahi kushambuliwa kwa ukatili katika kipindi chote cha nyuma tangu vyama vingi vianze kufanya kazi nchini Tanzania kama wakati huu,

Kipindi cha Uongozi wa Nyerere hakukuwa na vyama vingi hivyo ukiangalia tangu wakati wa uongozi wa rais Mwinyi mpaka sasa kuna tofauti kubwa",Tundu Lissu alisema.

Maelezo ya picha,

Julius Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania

Licha ya changamoto ambazo wanakutana nazo bado bwana Tundu Lissu anasema kwamba suluhisho sio kukaa kimya pamoja na kwamba ukatili ambao wanakabiliana nao ni mkubwa sana.

"Tumeingia kwenye kile kipindi ambacho tulikizungumzia hata mapema kabisa na inawezekana ndio sababu niko hapa maana tumeingia katika giza la utawala wa kidikteta,"Lissu alieleza.

Lissu ambaye alipigwa risasi na watu wasiojulikana katikati mwa ya mwaka jana na kufanyiwa upasuaji mara kadhaa anasema hana uhakika atarejerea lini nchini Tanzania mpaka pale ambapo daktari atakapotoa ruhusa.

"Lazima nitarejea na nitakuwa na tahadhari zaidi maana ni jambo la lazima mimi kurudi,nikirejea nitaendelea kuwa kwenye siasa na wala siogopi kwa sababu bado mimi ni mbunge wa singida mashariki niliyechaguliwa na wananchi kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano"Lissu alisisitiza.

Kwa upande wa kesi yake Tundu Lissu anasema hakuna aliyekamatwa wala kutuhumiwa kuhusika ingawa anachofahamu yeye ni kuwa mtu huhitaji kuwa profesa wa chuo kikuu kujua ni nani amefanya tukio hilo licha ya kwamba hana ushaidi wa nani amefanya kwa jina.

Maelezo ya video,

Tundu Lissu akosa msaada kutoka serikali ya Tanzania

Tamko la Serikali

Hatahivyo serikali kwa upande wake imeeleza kuwa Bwana Tundu Lissu hakufuata utaratibu unaotakiwa wa kupelekwa kwanza katika hospitali ya taifa ya Muhimbili ili aweze kuandikiwa mapendekezo ya kupelekwa na kutibiwa nje ya nchi au katika hospitali nyingine.

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ameiambia BBC Dira ya Dunia kwamba iwapo utaratibu huo utafuatwa hata sasa, malipo ya huduma zote za matibabu zitalipwa na bunge la Tanzania.