Wasifu wa Prince Philip: Kumkumbukizi ya Mwanamfalme Mtawala wa Edinburgh, Uingereza

Duke of Edinburgh

Chanzo cha picha, Terry O'Neill

Mwanamfalme Philip, Mtawala wa Edinburgh, aliheshimiwa na wengi kwa sababu ya kujitolea kwake kikamilifu kumuunga mkono Malkia wa Uingereza katika shughuli zake nyingi.

Huo ulikuwa wajibu mgumu kwa mtu yeyote yule, licha ya kwamba alikuwa amezoea kuwa kamanda wa jeshi la wanamaji aliyekuwa na maoni thabiti kuhusiana na masuala mbalimbali.

Hata hivyo ukakamavu wake ndio uliomsaidia kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kumsaidia mkewe Malkia kutekeleza wajibu wake kama Malkia.

Kama mume wa Malkia mwenye mamlaka makuu, Mwanamfalme Philip hakuwa na majukumu rasmi ya kutekelezwa na mtu wa wadhifa wake nchini humo. Lakini hakuna mtu aliyekuwa karibu sana na ufalme au umuhimu kwa ufalme kuliko yeye.

Mwanamfalme Philip alizaliwa katika familia ya kifalme ya Ugiriki mnamo 10 Juni, mwaka 1921 kwa kuwa wakati ule Ugiriki haikuwa ikitumia kalenda ya ijulikanayo kama Gregorian. Kutokana na hali hiyo cheti chake cha kuzaliwa kinasema kuwa alizaliwa Mei 28, mwaka 1921.

Baba yake alikuwa Mwanamfalme wa Ugiriki aliyejulikana kama Andrew, mwana mdogo wa Mfalme Goerge wa Kwanza wa Hellenes (Ufalme wa Wagiriki). Mamake alikuwa Bintimfalme Alice wa Battenberg, ambaye alikuwa mtoto mkubwa zaidi wa Mwanamfalme Louis wa Battenberg na dadake Earl wa Mountbatten wa Burma.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1922, Babake alitimuliwa kutoka nchini Ugriki na Baraza la Mapinduzi.

Meli ya kivita iliyotumwa na Binamu wake wa pili, Mfalme George wa Tano, ilisaidia kuhamisha familia hiyo hadi nchini Ufaransa. Mtoto Philip alisafirishwa kwenye kijisanduku cha kupakia machungwa wakati wote wa safari ya Baharini.

Chanzo cha picha, Royal Collection

Maelezo ya picha,

Mama yake, Binti mfalme Alice alikuwa kitukuu wa Malkia Victoria

Alikuwa mtoto mchanga zaidi na pia mvulana wa pekee katika familia yake na kwa hivyo alilelewa katika mazingira ya mapenzi makuu akiwa mchanga.

Mwanamfalme alianza elimu yake nchini Ufaransa lakini alipotimu umri wa miaka saba, alirudi kuishi na jamaa zake wa ukoo wa Mountbatten nchini Uingereza, ambapo alihudhuria masomo katika shule moja ya msingi eneo la Surrey.

Kufikia wakati huu mama yake alikuwa tayari amegunduliwa kuwa na maradhi ya akili na kufungiwa katika hospitali maalumu. Kwa hivyo hakuishi na mama yake muda mrefu maishani.

Mwaka 1933, alipelekwa katika shule maarufu ya Schule Schloss Salem kusini mwa Ujerumani iliyosimamiwa na mtaalamu wa elimu Kurt Hahn. Lakini baada ya miezi michache Hahn, aliyekuwa Myahudi alilazimika kutoroka mateso ya kundi la Nazi.

Kutajwa kwenye taarifa

Hahn alihamia Scotland ambapo baada ya miaka miwili alianzisha shule nyingine maarufu ijulikanayo kama Gordonstoun, ambayo Mwanamfalme alihamia baada ya mihula miwili pekee nchini Ujerumani.

Maisha ya ugumu katika shule ya Gordonstoun, yanayotilia mkazo hali ya kujitegemea yalikuwa mazingira bora kwa mvulana chipukizi, hasa yule ambaye ametengwa na wazazi wake, na aliyeishi kwa upweke.

Kwa kuwa ilionekana wazi kuwa vita viko karibu, Mwana Mfalme Philip aliamua kujiunga na jeshi. Alitaka kujiunga na jeshi la wanahewa lakini familia ya mama yake ilikuwa na Historia ya muda mrefu ya kujiunga na jeshi la wanamaji. Kufuatia shinikizo za familia ya mamake alijiunga na chuo cha Royal Naval College, Dartmouth.

Alipokuwa katika chuo hicho alipewa jukumu la kuwasindikiza mabinti wafalme wawili - Elizabeth na Margaret - wakati Mfalme George wa Sita na Malkia Elizabeth walipozuru chuo hicho.

Kulingana na walioshuhudia Philip alikuwa mtu wa madaha sana. Lakini kukutana kwao kulimvutia sana Bintimfalme Elizabeth.

Prince Philip alimvutia Binti Mfalme Elizabeth sana wakati aliposhinda katika mitihani yake ambapo mwaka Januari 1940 alikuwa nambari moja katika darasa lake. Alipigana vita katika Bahari ya Hindi na kuthibitisha ubabe wake katika jeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Philip (aliyeketi) alifana sana Gordonstoun ambapo alifurahia pia michezo ya sarakasi na uigizaji

Katika stakabadhi za vita anatajwa katika Meli ya kivita ya HMS Valiant katika kikosi cha meli za kivita za Bahari ya Mediterranean anatajwa kushiriki katika Makabiliano katika vita katika Rasi ya Matapan mwaka 1941.

Kwa kuwa yeye ndiye aliyesimamia ndege za kuchunguza adui aliyekaribu, alishiriki kikamilifu katika kuamua jinsi vita hivyo vya Rasi ya Matapan vilitekelezwa.

"Nilipata meli nyingine na ikawaka moto sehemu ya kati, ni kama tu ilimwezwa na kutumbukia moja chini baada ya kushambuliwa kwa mizinga ya kurusha makombora ya inchi 15 kwa karibu sana."

Ilipofika mwaka 1942 alikuwa miongoni mwa wanajeshi wachanga zaidi walioshikilia cheo cha Luteni katika Jeshi la Wanamaji la Uingereza, ambapo alihudumu katika meli ya kijeshi ya HMS Wallace.

Kuchumbiana

Wakati huu wote yeye na Binti Mflame Elizabeth walikuwa wakiandikiana barua na mara kwa mara alialikwa kuishi katika kasri ya mfalme.

Ni baada ya mojawapo wa mialiko hii katika kasri kipindi cha Krismasi mwaka 1943, ambapo baadaye Binti Mfalme Elizabeth alichukua picha ya Prince Philip aliyokuwa amevalia sare za kijeshi na kuiweka kwenye meza yake ya kuvalia nguo.

Uhusiano kati yao ulinawiri wakati wa amani ingawa kuna watu wa karibu na Binti Mfalme waliopinga uhusiano huo wakisema kuwa Prince Philip hakustahili. Mmoja wao alimtaja Prince Philip kama mtu aliyekaidi na aliye na tabia mbovu.

Licha ya yote yaliyosemwa Binti Mfalme alimpenda Prince Philip kupindukia hivi kwamba katika msimu wa joto wa 1946 Mwana Mfalme wa Ugiriki alimwomba Mfalme, babake Elizabeth idhini ya kumuoa bintiye.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Philip alifanikiwa sana katika jeshi la wanamaji

Hata hivyo, kabla uchumba huo kutangazwa, Mwana Mfalme alihitaji kupata uraia mpya na jina la ukoo.

Alifutilia mbali uraia wake wa Ugiriki na vyeo vyake vyote vya kifalme na kuwa raia wa Uingereza kabla ya kuchukua jina kutoka upande wa mama yake na kupewa jina Mountbatten.

Siku ya kuamkia siku ya harusi, Mfalme George wa Sita alimkabidhi Prince Philip jina rasmi la kifalme la His Royal Highness (HRH) na asubuhi ya Harusi akampachika jina la cheo: Duke of Edinburgh (Mtawala wa Edinburgh), Earl of Merioneth na Baron of Greenwich.

Harusi hiyo ilifanywa katika kanisa la West Minister Abbey tarehe 20 November 1947. Waziri Mkuu wa wakati ule, Winston Churchill, alitaja harusi hiyo kama iliyoleta mwanga na msisimko Uingereza kipindi cha baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Kusitishwa kwa ndoto yake jeshini

Prince Philip alirejelea kazi yake kama afisa wa jeshi la wanamaji na akatumwa hadi Malta kwa kazi, ambapo waliishi maisha ya kawaida ingawa kwa muda mfupi. Hapa waliishi kama familia ya kawaida ya kijeshi.

Mwana wao wa kwanza wa kiume, Prince Charles, alizaliwa Buckingham Palace mwaka 1948, na binti wao, Princess Anne, alizaliwa 1950.

Septemba tarehe 2, 1950, alipata cheo ambacho mwanamaji yeyote hufurahia sana. Alitangazwa kuwa kamanda wa meli yake ya kijeshi ya HMS Magpie.

Lakini maisha yake jeshini yalisitishwa. Hali kwamba afya ya George VI ilikuwa inadhoofika sana ilikuwa na maana kwamba binti yake alihitajika kuchukua majukumu zaidi ya kifalme na mumewe alihitajika karibu naye.

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Winston Churchill, alitaja harusi hiyo kama iliyoleta mwanga na msisimko Uingereza kipindi cha baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Philip aliomba likizo kwenye jeshi la wanamaji mnamo Julai 1951.

Hakurejea tena katika shughuli za kawaida za kijeshi.

Philip hakuwa mtu wa kusikitikia mambo maishani na hakulalamika kuwa alisitishiwa mpango wake wa kuendelea kufanya kazi jeshini. Lakini baadaye maishani aliwahi kusema kwamba alisikitika kwamba hakuweza kuendelea na kazi yake jeshini.

Waliokuwa wakifanya kazi naye jeshini walisema kuna uwezekano kwamba angepanda cheo na kufikia cheo cha juu zaidi.

Mwaka 1952 Prince Philip na mkewe walianza ziara ya maeneo ya Jumuiya ya Madola. Hiyo ziara ilikuwa awali imepangwa kufanywa na Mfalme na Malkia.

Mawazo ya kisasa

Alikuwa katika mgahawa mmoja katika mbuga ya wanyama pori nchini Kenya Februari ambapo habari zilimfikia kuwa Mfalme alikuwa amefariki.

Alifariki kutokana na kuganda kwa damu katika moyo wake.

Wajibu wa kumfahamisha mkewe kuwa ni alikuwa sasa ni Malkia ulipewa Prince Philip. Rafiki yake mmoja aliambia shirika la habari la BBC kuwa baada ya kupokea habari za kufariki kwa Mfalme, Prince Philip alionekana kama aliyeporomokewa na dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Philip alikuwa wa kwanza kutoa heshima zake kwa Malkia baada ya kutawazwa kwake

Kwa kuwa kazi yake ya kuwa mwanajeshi ilikuwa imekatizwa, na mkewe alikuwa ametangazwa kuwa Malkia, alijiuliza afanye nini sasa. Ilikuwa ni lazima kwake kujitafutia majukumu.

Wakati wa kutawazwa ulipokaribia ilitangazwa kuwa Philip angeshikilia cheo cha pili baada ya Malkia lakini ikatangazwa kuwa hawezi kupewa kazi nyingine yoyote kikatiba.

Philip alikuwa na maoni mengi ya kuimarisha hali ya kifalme kuendana na maisha ya kisasa lakini alikatizwa mara kwa mara na washauri wa ufalme wasiopenda mabadiliko katika kasri ya Mfalme.

Pigo kubwa

Prince Philip alianza kushiriki katika masuala mengi ya kijamii ili kuhakikisha anaendelea kufanya kitu cha maana.

Yeye na marafiki wake kadhaa wa kiume walianzisha mikutano ya kila juma kwenye hoteli moja katika eneo la Soho jijini London. Mikutano hiyo ilikuwa mirefu ambapo chakula cha mchana na burudani kilichukua masaa kadhaa na kutoa nafasi ya kushauriana. Wakati mwingine alitembelea vyumba vya burudani usiku na kupigwa picha.

Mara kwa mara Prince Philip alipigwa picha na watu maarufu nchini humo.

Prince Philip alipewa mamlaka makuu juu ya familia yake lakini alinyimwa madaraka kuhusu jina ambalo watoto wake wangelitumia.

Maelezo ya picha,

Alilazimika kuyazoea maisha kama mume wa Malkia mwenye nguvu

Uamuzi wa Malkia, kuwa watoto wataendelea kutumia majina ya ukoo wa Elizabeth wa Windsor badala wa ule wa Prince Philip wa Mountbatten, ulikuwa pigo kubwa kwa Mwanamfalme Philip.

Alisikika wakati huo akiwambia rafikize kuwa "Mimi ndiye mwanamume wa pekee ambaye haruhusiwi kutumia jina lake kwa watoto wake."

"Mimi si kitu, ila kama 'amoeba' (viini) hivi."

Wengi walisema katika shughuli zake za uzazi alionekana kuwa mtu asiyejali sana yanayoendelea katika familia.

Kulingana na aliyeandika habari kuhusu maisha ya Prince Charles, Jonathan Dimbleby, mara kwa mara Prince Philip alimkemea hadharani Prince Charles ambaye mara kwa mara angelia kutokana na kukemewa huko

Uhusiano kati ya Prince Philip na mwanawe wa kwanza haukuwa mzuri kwa kuwa ulikuwa wa kusukumana sukumana tu.

Kuwa imara

Philip alisisitiza kuwa Prince Charles alipaswa kwenda katika shule aliyohudhuria yeye ya Godonstoun, akiamini kuwa usimamizi wa shule hiyo utamlazimisha mwanawe kuwa na bidii zaidi kuliiko ulegevu mkubwa aliokuwa nao Prince Charles.

Prince Charles alichukia shule hiyo, na aliyatamani sana tena maisha ya nyumbani. Aidha, alisumbuliwa na wanafunzi watukutu.

Mwanamfalme Philip mara nyingi alichukua hatua zilizoonyesha ugumu wa maisha yake ya utotoni ambapo mara nyingi alikuwa na upweke utotoni.

Philip alitaka kumlazimisha mwanawe aanze kujitegemea mapema kama alivyokuwa yeye kwa wakati ambapo alitenganishwa na wazazi wake kama hatua ya kumfanya mwanawe awe mkakamavu zaidi. Alikuwa anashangaa ni kwa nini wengine hawakuwa hivyo, kama alivyokuwa yeye.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kusisitiza kwake kwamba Prince Charles ahudhurie shule ya Gordonstoun kulizua mzozo mkubwa kati ya baba na mwanawe

Mojawapo ya mambo yaliyomvutia sana Prince Philip ni hali ya maisha ya vijana au watu wachanga. Mnamo mwaka 1956 alianzisha mpango uliofaulu sana wa Tuzo ya Edinburgh.

Tangu kuanzishwa kwake, tuzo hiyo imewanufaisha zaidi ya vijana milioni sita walio walemavu na wale wa kawaida walio na umri kati ya miaka 15 - 25.

Vijana hao walipata tuzo kutokana na kujitolewa kwao kimwili, kiakili na katika mambo mengine mengi ya kimichezo na katika shughuli nyingine za kufanywa nje zenye lengo la kuwahimiza watu kuzoea kufanya kazi kwa pamoja, kuwa wa kufaa katika jamii na kuheshimu malisasili na mazingira.

"Iwapo unaweza kuwawezesha vijana kufaulu katika jambo lolote lile linalohitaji ushiriki wao," aliambia BBC, "hisia hizo na msisimko husambaa na kuwafikia wengine wengi."

Katika maisha yake yote, Prince Philip alijitolea kwa wingi kujitolea mhanga kushughulikia mpango huo ambapo alijihusisha katika mikutano mingi iliyohusu uendeshaji wa mradi huo.

'Kufuata haki'

Alikuwa pia mpenzi wa wanyama wa pori na mazingira hata ingawa uamuzi wake wa kumpiga risasi chui milia nchini India mwaka 1961 ulikosolewa vikali.

Uchapishaji wa picha ya chui huyo uliyafanya mambo kuwa mabaya Zaidi.

Hata hivyo alisaidia sana kuchangisha fedha la shirika la wanyama wa pori la dunia (WWF) na alikuwa Rais wake wa kwanza.

Katika mahojiano na BBC alinukuliwa kusema: "Ni jambo la kufurahisha kuwa tunayo maisha aina aina katika dunia hii ambapo viumbe wote wanategemeana."

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Duke of Edinburgh alijihusisha sana na shughuli za uhifadhi

Aliongezea: "Naamini pia kwamba iwapo sisi wanadamu tuna uwezo wa kufa na kupona - au kuangamiza kabisa au kuendelea na maisha - tunapaswa kuwajibika. Kwa nini kuangamiza kitu kabisa wakati ambapo tunaweza kukiendeleza?"

Alikasirisha baadhi ya wapenda mazingira wakati alipounga mkono kuuawa kwa ainda fulani ya ndege wajulikanao kama grouse kwa kuwapiga risasi.

"Iwapo kuna aina fulani ya mnyama unataka aendelee kuwepo ili mwaka ujao awepo - kama afanyavyo mkulima. Unataka kuwapunguza wala sio kuwaangamiza kabisa, " alisema.

Kusema waziwazi

Hata hivyo alipongezwa sana kwa kuhifadhi misitu duniani na pia kwa kuongoza kampeni ya kupinga uvuaji wa samaki wa kupindukia katika Bahari.

Prince Philip pia alivutiwa sana na viwanda ambapo alitembelea viwanda na wakati fulani akawa mdhamini wa chama cha wenye viwanda ambacho kwa sasa kinatambuliwa kama Work Foundation.

Atakumbukwa juu ya taarifa aliyoitoa kwa wenye viwanda mwaka 1961 ambapo Prince Philip aliwaeleza wazi wazi ambapo aliwambia "Waungwana umefika wakati ambapo tunapaswa kuvitoa kabisa vidole vyetu."

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Alifuatilia sana kwa karibu viwanda Uingereza

Taibia hii yake ya kusema mambo waziwazi bila kujali zilimletea wakosaji wengi wakati mwingine. Mara nyingi aliweza kusema mambo bila haya, hasa akiwa ng'ambo.

Kuna wale waliosema alikuwa na kiburi na alijikuta kwenye matatizo akiwa ugenini.

Wakati mmoja alipokuwa ziarani Uchina akiwa na Malkia mwaka 1986 alisikika akisema wakazi wa huko wana macho madogo sana, akidhani hakuwa hasikiki.

Ingawa Wachina wenyewe hawakukerwa na hilo kwa vyovyote vile, vyombo vya habari vya Magharibi vilimkosoa pakubwa.

Alipokuwa akitembelea Australia mwaka 2002 alimwuliza mfanya biashara mmoja mwenye asili ya Kiaborijini: "Bado mnarushiana mikuki nyinyi?".

Wasiwasi

Ingawa alikosolewa pakubwa na baadhi ya watu kwa maneno hayo yake ya kusema waziwazi, kunao waliotazama hilo kama ishara ya sifa zake halisi kama mwanamume, mwanamume aliyekataa kuficha mambo na uhalisia wake kwa ajili ya kuonekana kuwa sawa kisiasa.

Kuna wengi ambao waliotazama makosa hayo yake kama jaribio tu la kutaka kuchangamsha mambo mikutanoni na kuwawezesha watu aliokuwa nao kutulia.

Katika maisha yake yote, Prince Philip alifurahia sana riadha na michezo mingine. Alishindana katika mashua, alicheza kriketi na polo. Alifanikiwa sana katika mbio za magari ya kuvutwa na farasi na alikuwa rais wa shirikisho la kimataifa la mbio za farasi, International Equestrian Federation, kwa miaka mingi.

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Aliupenda sana mchezo wa polo

Uhasama kati yake na mwanawe wa kwanza, Prince Charles, ulitokezea tena baada ya kuchapishwa kwa kitabu cha maisha ya Prince Charles na Jonathan Dembleby.

Ilidaiwa kuwa Mtawala huyo wa Edinbburgh alimlazimisha Charles kumwoa Diana Spencer.

Hata hivyo Philip alikuwa mvumilivu zaidi na mwenye kujali sana wakati ndoa za wana wake zilipokuwa zikiporomoka.

Alikuwa mastari wa mbele katika kujaribu kuelewa ni kitu gani hasa kilichokuwa kikisibu ndoa zao. Yeye mwenyewe aliweza kufahamu shida za kuoa katika familia ya kifalme.

Safari ya imani

Prince Philip alisikitishwa sana kuporomoka kwa ndoa za watoto wake watatu kati ya wanne - Binti Mfalme Anne, Mwana Mfalme Andrew, pamoja na Prince Charles.

Lakini yeye hakupenda kuzungumzia maisha ya kibinafsi ya watu. Mwaka 1994 aliambia mwandishi wa habari kuwa hajawahi kufanya hivyo siku zilizopita na hakunuia kuanza kufanya hivyo wakati huo.

Kuzeeka kwake hakukupunguza kasi yake ya maisha yake. Aliendelea kusafiri kwa marefu na mapana. Alisafiri kuchangisha fedha kwa mpango wa WWF na alisafiri pia na Malkia wakati wa ziara zake ng'ambo.

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Prince Philip alipenda sana mbio za magari ya kubururwa na farasi

Alifanya ziara takatifu ya kibinafsi jijini Jerusalem kutembelea kaburi la mama yake mwaka 1994. Ombi la mamake la kutaka azikwe Jarusalem lilikuwa limetimizwa

Kulikuwa na tukio jingine muhimu kwake wakati wa kusherehekea siku ya ushindi katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, miaka 50 baadanya kumalizika kwa vita hivyo, sherehe zilizofanyika mwaka 1995.

Mwanamfalme Philip alikuwa kwenye meli ya kivita kwenye Ghuba ya Tokyo wakati Japan iliposalimu amri, na siku ya kuadhimisha siku hiyo, alijiunga na wanajeshi wa zamani walioshiriki vita hivyo Mashariki ya Mbali katika msafara mbele ya Malkia katika barabara ya The Mall jijini London.

Hisia za upendo

Wakati huo pia alieleza masikitiko yake kwa wafungwa za zamani wa Japan ambao walikuwa mejaribu lakini wakashindwa, kuwasamehea watekaji wao kwa sababu ya maovu waliyofanyiwa.

Kuongea kwake kwa kiburi kulipunguka baadaye maishani kufuatia shutuma kali dhidi ya ukoo wa kifalme hasa baada ya kufariki kwa Princess Diana, Princess of Wales.

Mwaka 2007 barua kati ya Prince Philip na Princess Diana katika juhudi za kuonyesha kuwa Prince Philip hakuwa na chuki dhidi ya mke wa mwanawe mkubwa zilichapishwa

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

Alimuunga mkono sana Diana, Princess of Wales

Katika barua hizo zilizopewa jina Dear Pa (Mpendwa Baba), Prince Philip alionekana kuwa mshauri na alimliwaza Princes Diana. Barua za Princess Diana zilionekana kuandikwa kwa heshima na mapemzi maalumu.

Katika uchunguzi wa mahakama wa kifo cha Princess Diana, baba wa mpenzi wake wa mwisho, Dodi, Mohammed Al Fayed, alisema kuwa Princess Diana aliuawa kutokana na maagizo ya Prince Philip. Dai hilo lilikanushwa vikali na Daktari bingwa wa ukaguzi wa maiti.

Prince Philip aliyejulikana kama Duke of Edinburgh, alikuwa mtu mkakamavu na mwenye mawazo huru aliyejikuta katikati mwa maisha ya jamii ya Uingereza.

'Mtu mwenye msimamo mkali'

Alizaliwa na tabia za kuwa kiongozi lakini kutokana na hali yake ya kimaisha alijikuta akishikilia nafasi ya pili.

Alikuwa mtu mbishi anayekasirika kwa upesi lakini ikabidi ajizuie mambo mengi ili kuhakikisha maisha yake hayahitilafiani na hali yake ya kimaisha.

"Nimefanya kile naamini kuwa sawa kwa kadiri ya uwezo wangu," aliambia BBC wakati mmoja. "Siwezi kuamka siku moja tu na kuanza kufanya mambo tofauti. Hivyo ndivyo nilivyo."

Maoni hayo yaliungwa mkono na David Cameron, aliyekuwa Waziri Mkuu wakati wa maadhimisho ya miaka 90 tangu kuzaliwa kwa Prince Philip. Maadhimisho hayo yalifanywa Juni mwaka 2011.

Waziri Mkuu Cameron alisema: "Yeye amekuwa akifanya vitu kwa njia yake mwenyewe, kwa njia ya kawaida, bila kujali chochote, kwa njia ambayo inawavutia raia wengi wa Uingereza."

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha,

Malkia alimweleza kama nguvu na ngome yake

Kustaafu kutoka kwa shughuli za umma

Duke Philip alistaafu kutoka kwa maisha ya umma Agosti mwaka 2017. Alijondoa katika kazi nyingi za hadhara baada ya miongo kadhaa ya kumuunga mkono Malkia na kuhudhuria hafla nyingi mashirika kadhaa ya kutoa misaada kwa umma na mashirika yake mwenyewe.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Buckingham Palace, Prince Philip, alihudhuria shughuli rasmi 22,219 tangu mwaka 1952. Waziri Mkuu Theresa May alimshukuru kwa "kufanya kazi nzuri ya kuvutia kwa umma."

Philip alifaulu kutumia nafasi yake kufanya mabadiliko makubwa katika jamii ya Uingereza na alishiriki katika kusaidia Ufalme wa Uingereza kutambua kubadilika kwa mawazo ya kijamii kadiri miaka ilivyosonga.

Hata hivyo jambo alilofaulu zaidi kati ya yote hayo ni bidii na juhudi zake za kujitolea kumuunga mkono Malkia kutekeleza wajibu wake muhimu kwa jamii ya Uingereza katika utawala wake.

Alimweleza mwandishi wa habari za maisha yake kuwa kazi yake kubwa ilikuwa kuhakikisha kuwa Malkia anatawala.

Katika hotuba aliyoitoa wakati wa kuadhimisha miaka 50 tangu ndoa yao kuanza, Malkia Elizabeth alimpongeza mumewe, ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa mume au mke wa Malkia au Mfalme aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Uingereza.

"Ni mtu ambaye hapendi kusifiwa ovyoovyo, lakini amekuwa lakini amekuwa mhimili wangu mkuu, nguvu na ngome yangu, na msaidizi wakati huu wote. Na mimi, na familia yake yote, na taifa hili na mataifa mengine mengi tunalo deni kubwa kwake ambalo haitakuwa rahisi kulilipa na wala mwenyewe hawezi kukadiria wala sisi wenyewe kulifahamu kiasi chake."

Chanzo cha picha, PA

Picha zote zina hakimiliki.