Adhabu ya viboko yasababisha kifo cha mwanafunzi Tanzania

viboko
Maelezo ya picha,

Adhabu ya viboko itakoma lini Tanzania

Mwanafunzi mmoja wa darasa la tano katika shule ya Msingi Kibeta,manispaa ya Bukoba mkoani Kagera nchini Tanzania amedaiwa kupigwa na mwalimu wake mpaka kufariki kwa tuhuma ya kuiba mkoba wa mwalimu huyo.

Mara baada ya tukio hilo Waziri wa Elimu nchini Tanzania, Joyce Ndalichako amewataka watu wawe watulivu hadi upelelezi wa tukio hilo utakapomalizika.

"Shule ni sehemu salama sasa isitokee mtu aondoa hiyo dhana,hiyo ni bahati mbaya iliyotokea na isitafsiriwe kuwa shule sio mahali salama, Serikali itawashughulikia wale wote ambao wanahatarisha amani na usalama"Waziri Ndalichako aeleza.

Maelezo ya picha,

Shule ni mahala salama

Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa na shirika la habari Tanzania,TBC iliripoti juu ya wazazi kususia kuzika mwili wa marehemu kwa kudai kuwa ripoti iliyotolewa na daktari iliyosemwa kwamba mwanafunzi huyo alikuwa ana majeraha ya siku mbili kabla ya kupigwa na walimu huyo sio ya kweli.

Ripoti hiyo ambayo iliwashangaza na kupelekea mtoto huyo kufanyiwa uchunguzi mara ya pili ,na sasa uchunguzi wa pili umekubaliwa na wazazi wa mtoto huyo ingawa ripoti ya pili haijatajwa hadharani bado kwamba ni nini chanzo cha kifo cha mtoto huyo.

Mwalimu aliyedaiwa kuhusika kumpiga mtoto huyo bado anashikiliwa na polisi mpaka sasa na wengine wawili.

Simulizi ya tukio hilo la kuiba mkoba

Baadhi ya wanafunzi walisimulia tukio hilo kuwa wakati mwalimu wao wa nidhamu alipofika shuleni, kuna wanafunzi ambao walimpokea mizigo yake wakati aliposhuka na bodaboda.

Lakini baada ya mwalimu huyo kuingia ofisini kwake alibaini kuwa hauoni mkoba wake na kuanza kuuliza kila mwanafunzi na kutangaza upotevu huo katika mkusanyiko wa wanafunzi wote.

Baadae mwalimu huyo akamuhoji marehemu kwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na tabia ya kupokea walimu mzigo yao mara kwa mara na alipoulizwa akakana ndipo akaanza kupigwa viboko.

Dereva wa bodaboda badae alirudi na kusema mwalimu alisahau mkoba katika pikipiki wakati mtoto ameshazimia.