Uzazi wa Mpango: Utitiri wa watoto na kupaa kwa umasikini Afrika

Mama na wana nchini Ghana Haki miliki ya picha Getty Images

Katika jamii nyingi za kiafrika, kupata watoto ni jambo linalochukuliwa kama baraka. Baadhi ya jamii huchukulia kuwa na watoto wengi kama ishara ya utajiri na fahari. Ni jambo ambalo pia hupigiwa chapuo.

Nchini Ghana, wenyeji wa kiasili wa Mji Mkuu wa Accra ni kabila la Ga, mwanamke anapojifungua mtoto wake wa 10 huzawadiwa kondoo mzima. Desturi hiyo hufahamika "nyongmato".

Ukizunguka Jijini Accra leo, kwenye mabenki, vyombo vya usafiri, mitaani na kwengineko ni nadra kukutana na mama mwenye watoto zaidi ya wanne. Yawezekana Accra sio sehemu sahihi tena ya kutafuta familia yenye watoto 10 na kuendelea.

Miezi miwili iliyopita mwandishi wa BBC nchini Ghana Elizabeth Ohene alihudhuria mazishi ya rafikiye wa toka shule ya msingi ambaye ameacha familia ya watu 44. Marehemu ameacha watoto nane,wajukuu 26 na vitukuu 8.

Uzazi usiopangwa na ongezeko kubwa la watu ni moja ya sababu kuu inayotajwa kuchochea umaskini barani Afrika.

Nchi ya Ghana ilikuwa na watu milioni 5 wakati ikipata uhuru mwaka 1957, miaka 60 baadae leo hii kuna watu milioni 30. Norway katika kipindi hichohicho wametoka kuwa na watu milioni 3.5 mpaka milioni 5.3.

Afrika Mashariki

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kwamujibu wa takwimu rasmi za serikali zilizotolewa mwezi Februari 2018, Tanzania kuna watu milioni 54, na ongezeko la watu linakadiriwa kufikia milioni 1.6 kila mwaka.

Kinachoendelea Ghana kinaakisi sehemu nyengine za Afrika ikiwemo ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwamujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) idadi ya watu imeongezeka mara mbili nchini Kenya katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Idadi ya watu nchini Kenya hivi sasa inafikia milioni 50.9, na kwamujibu wa UN kama hatua stahiki hazitachukuliwa basi ongezeko hilo litapaa kwa watu milioni moja kila mwaka na nchi hiyo itafikisha idadi ya raia milioni 90 kufikia mwaka 2051.

Utafiti:Hakuna pombe isiyokuwa na madhara

Kama ilivyo kwa Ghana, Kenya pia inapambana na umasikini ambao unaathiri walio wengi. Takwimu zinonesha kuwa takriban 50% ya wananchi wa Kenya wanaishi katika lindi la umasikini.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ghana ilikuwa na watu milioni 5 wakati ikipata uhuru mwaka 1957, miaka 60 baadae leo hii kuna watu milioni 30.

Akinadi sera ya serikali yake ya kutoa elimu bure nchini Tanzania, Rais John Magufuli alinukuliwa mara kadhaa akiwaambia wananchi wasiogope kuzaa na kutumia msemo "fyatueni tu" na serikali itawasomesha.

Hatahivyo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu baadae alijitokeza na kuweka mambo sawa akisisitiza kuwa serikali bado inawaasa wananchi watumie uzazi wa mpango na kuzaa watoto ambao wataweza kuwahudumia kikamilifu.

Kuhusu kauli ya Rais Magufuli, Bi Ummy alisema rais alikuwa akiwafanyia utani watania zake wa kabila la Wazaramo ambao ni wenyeji wa Jiji la Dar es Salaam.

Kanisa linalotukuza unywaji pombe Afrika Kusini

Kwamujibu wa takwimu rasmi za serikali zilizotolewa mwezi Februari 2018, Tanzania kuna watu milioni 54, na ongezeko la watu linakadiriwa kufikia milioni 1.6 kila mwaka.

Katika kupambana na ongezeko hilo kubwa la watu, Kenya wamefanikiwa kuongeza matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambapo kwa sasa 53% ya wanandoa walikuwa wakitumia uzazi wa mpango kufikia mwaka 2014 kutoka 39% kwa mwaka 2008/2009.

Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikiwekeza katika kuchagiza matumizi ya uzazi wa mpango ambapo kwa mwaka 2018/19 imetenga shilingi bilioni 22 kwa ajili hiyo.

Nchini Ghana, katika jitihada za kudhibiti ongezeko kubwa la watu Mkurugenzi wa Baraza la Idadi ya Watu Dkt Leticia Adelaide Appiah anapendekeza kuwekwa kikomo cha uzazi kwa kila mwanamke kuwa watoto watatu. Na ikitokea mtu akaongeza basi adhabu yake iwe kutopata msaada wowote kutoka serikalini. Pendekezo hilo bado halijapita lakini ni dhahiri kuwa litazua mjadala mkubwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii