Je ni kweli mifuko ya plastiki inasababisha saratani?

  • Lulu A. Sanga
  • BBC Swahili
Picha ya BBC
Maelezo ya picha,

Mifuko ya plastiki laini hupatikana kwa bei rahisi Tanzania

Mara nyingi mifuko laini na miepesi ya nailoni au Rambo kama inavyojulikana na wengi Tanzania imekuwa ikitumiwa na baadhi ya wananchi katika kufungashia chakula na hasa vyakula vya haraka kama chips au wali kwa wale wenye migahawa midogo kabisa.

Hata hivyo kuna baadhi ya familia wao huchana mifuko ya nailoni na kuitumia kufunikia vyakula pale wanapokua wakipika kwa Imani kuwa inasaidia kuivisha chakula haraka, kwani hufunika vizuri na kuganda kwenye sufuria hivyo mvuke wote hubaki ndani, mfano kufunikia wali, wakati wa kuchemsha mahindi, viazi au mihogo.

Tofauti na mifuko, kumekuwa na matumizi makubwa ya vyombo vya plastiki katika familia nyingi hapa Tanzania.

Na vyombo hivyo kama vikombe sahani na hata majagi vimekuwa vikitumika sana kuhifadhia chakula tena mara nyingi ni cha moto.

Kwa mujibu wa taasisi ya kilimo na sera ya biashara IATP, plastiki zote zinaundwa kwa kemikali ambayo inauwezo wa kuharibu afya ya mtu.

Baadhi ya kemikali hizo ni BPA na DEHA, na zinatajwa kuhusika na mabadiliko ya tishu, kuharibiwa kwa vina saba, kuharibu mimba, matatizo wakati wa uzazi na mabadiliko ya homoni.

Wakati kwa watoto kemikali hizo zinatajwa kuharibu kinga yao ambayo inatakiwa kuongezeka hali inayosababisha homoni kubadilika na kusababisha matatizo katika tabia .

Kwa Tanzania kupitia mitandao ya kijamii kumekuwa na taarifa mbali mbali zinazo eleza juu ya madhara ya kuweka chakula katika vyombo vya plastiki na zaidi ni mifuko laini ya plastiki.

Baadhi ya ujumbe unoa sambazwa katika mitandao ya kijamii hasa whatsapp zimebeba ujumbe unao onya kuwa plastiki ina aina hamsini na mbili za saratani.

Na kuonya watu wasiweke kitu cha moto kwenye kitu chochote cha plastiki.

Mfano: ' Jumuiya Ya Madaktari Wa Marekani Imetoa Majibu Ya Vyanzo Vya Cance'

1.Usinywe Chai Kwenye Vikombe Vya Plastic Kuanzia Sasa

2.Usile Chochote Chenye Moto Kilicho Ndani Ya Mfuko Wa Plastic Mfano Chipsi

3.Usipashe Chakula Kwenye Microwaves Kwakutumia Vyombo Vya Plastic

ANGALIZO:Kumbuka Plastic Ikikutana Na Joto Kali Inatoa Kemikali Inayosababisha Aina 52 Za Cancer Kwahiyo Wafahamishe Wote Uwapendao Ili Waepukane Na Madhara Haya".

Chanzo cha picha, Daktari Heri Tungaraza

Maelezo ya picha,

Daktari Heri Tungaraza kutoka katika hospitali ya taifa Muhimbili kitengo cha Saratani

BBC imefanya mazungumzo na Daktari Heri Tungaraza, kutoka katika hospitali ya taifa Muhimbili kitengo cha Saratani ili kupata ufafanuzi zaidi juu ya kuhusika kwa plastiki na maradhi ya saratani.

"Kwa ishu ya saratani bado hatuna uhakika sana kwamba BPA au kemikali nyezake inaweza kusababisha saratani, lakini kama unavyojua tafiti nyingi hufanyika kwa wanyama. Kwa hiyo BPA na kemikali nyingi ambazo zinatoka kwenye plastiki zimesha jaribiwa kwenye wanyama sanasana Panya na ikaonyesha kuna uhusiano na saratani," dokta Tungaraza anaiambia BBC.

Hata hivyo Daktari huyo amesisitiza kuwa bado hakuna ushahidi juu ya utafiti uliofanyika kwa binadamu unao thibitisha kuwa plastiki inaleta saratani. Lakini ametaja kuwepo kwa baadhi ya madhara ikiwepo kuvuruga homoni iliyothibitishwa na tafiti na changamoto hiyo hupelekea tatizo la ugumba.

"Madhara yapo na ambayo yamesha thibitishwa ni yale madhara ambayo yanaendana na zile kemikali ambazo zinatumika kutengeneza hiyo plastiki kufanya iwe plastiki. Na inayo julikana zaidi na imefanyiwa utafiti ni BPA. Madhara yake makubwa ni kwamba inafanana na homoni za binadamu kwa hiyo ukiweka chakula cha moto au ukafanya chochote ambacho kikafanya ile plastiki iwe ya moto au wakati wa kusafisha ukatumia dawa ambayo ni kali au ukakwaruza na kufanya ile BPA itoke na kuingia kwenye mwili wa binadamu huenda kufanya kazi kama vile homoni na kuvuruga homoni," anasema dokta Tungaraza.

Maelezo ya picha,

Karatasi za plastiki za zimepigwa marufuku katika baadhi ya nchi Afrika mashariki

Dokta Tungaraza anatoa ushauri wa kiafya kwa watu wanao tumia mifuko ya plastiki kuwekea chakula cha moto mara kwa mara.

"Mifuko ya plastiki au kuweka chakula katika mifuko ya plastiki si kitu kizuri kwa hiyo ni vyemamtu akajiepisha kwasababu ya kemikali nyingi ambazo zinatoka kwenye hiyo mifuko, na huo mfuko hauja andikwa na watu wengu watanzania hatupendendi kuangalia leble, ni vyema kwa sasahivi kuacha kutumia mifuko na kutumia contena ambazo zenyewe kidogo hazitotoa kemikali kwenda kwenye chakula," dokta Tungaraza anaiambia BBC.

Daktari huyo ameongeza kuwa watu wajitahidi kutumia glass au vyombo vilivyotengenezwa na malighafi ya ceramic na vyombo husika lazima vihakikishe kwamba hizo bidhaa ambazo watu wanatumia za plastiki zina kiwango, lakini kisiwe kiwango cha juu sana kuweza kusababisha saratani kwa binadamu au kupelekea hatari ya mtu kuwa na saratani.

Hata hivyo si tanzania pekee inayopambana kakabiliana na matumizi ya plastiki, baadhi ya nchi za Afrika zimefanikiwa katika kupambana na matumizi ya plastiki kwa sababu za kiafya na kimazingira.

Mwaka 2017 Kenya ilipiga marufuku mifuko hiyo, na imeorodheshwa miongoni mwa mataifa 50 yaliochukuwa hatua hiyo katika ripoti ya Umoja wa mataifa inayopendekeza kuwa serikali duniani zinahitaji kufikiria kupiga marufuku au kuidhinisha kodi kubwa kwa watengenezaji mifuko hiyo ya plastiki.

Sheria ya mwaka 2009 ya fedha Uganda inapiga marufuku "uingizaji, utengenezaji, uuzaji na utumiaji wa mifuko na magunia ya plastiki kuanzia mwaka 2010. Na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, hivi karibuni aliamrisha maafisa wa usalama nchini humo kuhakikisha kuwa marufuku ya kutumia mifuko ya plastiki inatekelezwa.

Ripoti hiyo ya Umoja wamataifa inasema kumeshuhudiwa matokeo tofuati katika sera za kupambana na taka za palstiki. Na kwa upande wa Cameroon, mifuko ya plastiki imepigwa marufuku na watu majumbani hulipwa kwa kila kilo ya taka za plastiki wanazokusanya, lakini bado mifuko hiyo huingizwa kwa njia za kimagendo.