Marekani yafuta msaada wa dola milioni 300 kwa jeshi la Pakistan

Pakistanis protest against Donald Trump's accusations that their country harbours militants, 25 August 2017

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Pakistan imekana awalia madai ya Marekani kuwa inawapa mazingira salama wanamgambo

Jeshi la Marekani linasema linafuta msaada wa dola milioni 300 kwa Pakistan kutokana na kile ilitaja kuwa kushindwa kwa pakistan katika kuchuyachukulia hatua makundi ya wanamgambo.

Rais Donald Trump alikuwa awali ameilaumu Pakistan kwa kuipuuza Marekani wakati inapokea mabilioni ya dola.

Msemaji wa jeshi la Marekani Luteni Kanali Koné Faulkner alisema jeshi la Marekani litatumia pesa hizo kwa masuala mengine ya dharura

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani imeilaumu Pakistan, mshirika mkuu, kwa kushindwa kukabiliana na mitandao ya kigaidi inayohudumu kwenye ardhi yake ukiwemo mtandao wa Haqqani na ule wa Talibabn.

Tangazo hilo linakuja siku chache kabla ya waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani Mike Pompeo kufanya ziara nchini Pakistan kukutana na waziri mkuu mpya Imran Khan.

Mwezi Januari serikali ya Marekani ilitangaza kuwa inafuta karibu misaada yote ya shughuli za ulinzi kwa nchi hiyo.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Pakistan na Marekani ni washirika wakubwa na uhusiano umedorora hivi karibuni

Marekani na wengine kwa muda mrefu wamelalamika kuwa Pakistan ni mazingira salama kwa mitandao ya kigaidi inayowaruhusu kuendrsha mashambulizi kwenye nchi jirani kitu ambacho Pakistan inakana.

Hakukuwa na tamko lolote kutoka Pakistan kuhusu hatua hiyi ya hivi punde ya kufuta misaada.

Ni wanamgambo wapi Pakistan inalaumiwa kuwaunga mkono?

Mtandao wa Haqqani ni kundi la wanamgambo ambalo huendesha shughuli zake kwenye taifa jirani la Afghanistan ambalo limelalamika kwa miaka mingi kuwa Pakistan huruhusu kundi hilo kuendesha oparesheni zake kutoka ardhi yake.

Kundi hilo lina uhusiano na kundi la Taliban nchini Afghanistan ambalo ni tisho kubwa kwa serikali ya Afghanistan.