Bobi Wine awasili Marekani kupata matibabu

Bobi Wine in a wheelchair just prior to his departure at Entebbe International Airport, Uganda, 31 August 2018

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bobi Wine, wakati akiondoka nchini Unganda

Mwanamuzi na mbunge nchini Uganda Bobi Wine amewasili Marekani kwa matibabu kufuatia madai kuwa aliteswa na kupigwa wakati akizuliwa na wanajeshi.

Wine aliruhusiwa kuondoka nchini Uganda mapema lakini aliruhusiwa kuondoka Ijumaa.

Yeye na wanasiasa 32 wa upinzani walishtakiwa na shtaka la uhaini wiki iliopita kufuatia madai ya kuupiga mawe msafara wa rais Yoweri Museveni.

Bobi Wine mapema aliachiliwa kwa dhamana lakini akaambiwa kwamba hawezi kuondoka Uganda.

Siku ya Ijumaa , maafisa wa polisi walithibitisha kwamba alikuwa ameruhusiwa kuondoka nchini humo kwa matibabu maalum baada ya serikali kutuma kikosi cha madaktari tisa kumchunguza hali yake.

Wakili wa Bobi Wine mapema alikuwa amesema kuwa mwanamuziki huyo alikuwa amekamatwa kwa nguvu akiwa katika uwanja wa ndege siku ya Alhamisi, ijapokuwa jaji alikuwa amemruhusu kupata pasipoti yake kwa sababu alihitaji kuondoka nchini humo kwa sababu za kimatibabu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bobi Wine wakati wa maandamano

Alikamatwa kwa nguvu na kutupwa katika ambulensi ya polisi.

Msemaji wa polisi alisema katika ujumbe wake wa Twitter kwamba Bobi Wine alikuwa akifanyiwa uchunguzi kutokana na madai ya kupigwa.

Pia walisema kuwa mbunge mwengine wa upinzani Francis Zaake alikuwa akijaribu kuelekea Ulaya kwa matibabu , alikuwa akijaribu kutoka Uganda lakini akakamatwa.

Wakati huohuo wafuasi wa Bobi Wine wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Kampala.

Ni kipi kilisababisha mashtaka ya uhaini?

Kabla hajakamatwa, Bobi Wine, alichapisha picha ya dereva wake ambaye alisema alipiwa risasi na kuuliwa na polisi waliodhani kuwa aliyekuwa ni yeye.

Bobi Wine alikamatwa tarehe 13 Agosti baada ya mkutano wa kampeni kaskazini-magharibi kwenye mji wa Arua ambapo kuna madai kuwa msafara wa rais ulitupiwa mawe.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa Bobi Wine waliandamana Kampala wiki iliyopita

Mwanamuziki huyo mwenye miaka 36 awali alishtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi kwa makosa ya umiliki wa silaha kinyume cha sheria, mashtaka ambayo yalifutwa baadaye. Kisha akafunguliwa mashtaka ya uhaini kwenye mahakama ya kiraia.

Bobi Wine ni nani hasa?

Nyota huyu wa mtindo wa Afrobeats aliingia katika taaluma ya muziki katika miaka ya 2000, na anaelezea kipaji chake kuwa ni cha kuelimisha na kuburudisha. Mojawapo ya vibao vyake vya awali Kadingo, inahusu usafi wa mwili.

Alizaliwa 12 Februari 1982, Bobi Wine na alikuwa na miaka minne pekee Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986.

Jina lake rasmi Wine, ni Robert Kyagulanyi Ssentamu.

Alilelewa katika mtaa duni wa Kamwokya kaskazini mashariki mwa Kampala na alianza kujihusisha katika muziki mapema miaka ya 2000.

Nyimbo zake za mtindo wa dansi za 'Akagoma' na 'Funtula' zilikuwa maarufu sana miongoni mwa vijana.

Ana shahada ya muziki, dansi na uigizaji kutoka Chuo Kikuu cha Makerere ambapo alihitimu mwaka 2003.

Aprili 2018 alifuzu na stashahada ya masuala ya kisheria kutoka Kituo cha Maendeleo ya Sheria, Kampala.

Alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka 2017 wilayani Kyadondo mashariki, Uganda ya kati.

Aliwashinda wagombea kutoka chama tawala National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).

Baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.

"Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki...Ninataka siasa zitulete pamoja... jinsi muziki ufanyavyo."