Wakenya walalamika kuhusu ongezeko la bei ya mafuta kwa 16%

Tayari nauli nauli za usafiri katika sekta ya uchukuzi wa umma imepanda

Chanzo cha picha, Hindustan Times/Getty Images

Maelezo ya picha,

Tayari nauli za usafiri katika sekta ya uchukuzi wa umma zimepanda

Wakenya wameelezea kutoridhishwa na hatua ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta nchini.

Serikali ya Kenya kupitia tume ya nishati siku ya Jumamosi iliidhinisha 16% ya tozo la kodi kwa bidhaa za mafuta nchini.

Hatua hii inajiri siku kadhaa baada ya bunge kusitisha kuidhinishwa kwa muda hatua hiyo hadi Septemba mwaka 2020.

Kodi hii imeidhinishwa kufuatia mapendekezo kutoka shirika la fedha la kimataifa IMF miaka miwili ya nyuma katika jitihada za kuziba pengo la bajeti.

Tayari nauli za usafiri katika sekta ya uchukuzi wa umma imepanda kufuatia kuanza kuetekelezwa kwa hatua hiyo.

Hivi sasa lita moja ya mafuta ya petroli inauzwa kwa takriban $1.27 huku dizeli ikiuzwa kwa &1.15 na mafuta ya taa $0.96 - hii ikiwa ni ongezeko la shilingi 14 za Kenya.

Kufikiwa mwishoni mwa Juma, baadhi ya raia kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa shinikizo kwa rais Uhuru Kenyatta na serikali yake kuchelewesha kutia saini marekebisho hayo ya sheria yatakaochelewesha kuidhinishwa kwa tozo hilo la ushuru.

Chanzo cha picha, WALTER ASTRADA/Getty Images

Maelezo ya picha,

Hivi sasa lita moja ya mafuta ya petroli inauzwa kwa takriban $1.27

Rais Uhuru Kenyatta aliondoka kuelekea kwenye mkutano wa Uchina na mataifa ya Afrika pasi kusema lolote kuhusu hatua hiyo ya serikali.

Kuongezwa kwa ushuru kunaonekana pia kuchangia ongezeko la bei za bidhaa muhimu.

Mambo muhimu kuhusu 16% Tozo la kodi kwa bidhaa za mafuta Kenya

  • Iliidhinishwa mnamo 2013.
  • Bunge lilipitisha mswada wa tozo la kodi ulioidhinisha kupandishwa kwa bei za bidhaa za mafuta.
  • Imenuiwa kukusanya pato la takriban $ milioni 338 kwa mwaka.
  • Wizara ya fedha mnamo 2016 ilisimamisha hatua hiyo kwa miaka miwili ya ziada.
  • Imelenga kutatua nakisi ya bajeti ya serikali na kupunguza deni la taifa.
  • Rais Uhuru Kenyatta bado hajasaini mapendekezo yaliowasilishwa ya marekebisho ya sheria.

Chanzo cha picha, Pool/Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Uhuru Kenyatta

Ni nani wa kuwaokowa Wakenya dhidi ya kodi?

Wakenya katika mtandao wa kijamii Twitter wameanzisha mjadala mkali kuonyesha kutoridhishwa kwao na hatua hiyo ambayo baadhi wanaitaja kuwa hatua ya makusudi.

Kupitia #PunguzaBeiYaMafuta baadhi ya raia walieleza:

Mvutano huu umevutia hisia za wanasiasa tofuati nchini.

Katika kituo cha televisheni ya NTV, kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale ameeleza kwamba anayeweza kutoa njia kuhusu mvutano huu ni rais Uhuru Kenyatta pekee.

"Sheria inayotumika ni sheria iliyopitishwa bungeni mnamo 2013, na inaweza kugeuzwa iwapo tu rais ataidhinisha marekebisho ya mswada wa fedha ya mwaka huu 2018. Pasi na hivyo, sheria ya 2013 iliyositishwa kwa miaka mitatu na baadaye miaka miwili zaidi kwa mujibu wa agizo la waziri hadi mwaka huu 2018... inaanza kutumika moja kwa moja Septemba mosi 2018. Na ndio sababu ni lazima Wakenya waelewe vizuri." Duale alisema.

Chanzo cha picha, SIMON MAINA/Getty Images

Maelezo ya picha,

Kuongezwa kwa ushuru kunaonekana pia kuchangia ongezeko la bei kwa bidhaa muhimu.

Tayari baadhi ya viongozi katika muungano wa upinzani wametoa muda wa siku tatu tangu Jumapili kwa waziri wa fedha Henry Rotich kupindua agizo hilo.

Kupitia vyombo vya habari nchini, wabunge hao wametishia kuwasilisha mswada dhidi ya waziri huyo kwa kukiuka uamuzi wa bunge kuistisha tozo hilo la kodi hadi Sepetemba 2020.

Bunge lilipiga kura kuchelewesha kuidhinishwa kwa hatua hii, lakini Waziri wa fedha alitoa agizo la kutekelezwa kwa hatua hiyo kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Athari zinazotazamiwa ambazo baadhi zimeanza kudhihirika kutokana na kupandishwa kwa bei ya mafuta ni pamoja na kupanda kwa nauli za usafiri katika magari ya uchukuzi wa umma.

Kupanda kwa bei za bidhaa muhimu wakati wakulima na wachuuzi wakiathirika kwa upande wao kwa gharama kubwa ya kusafirisha chakula.

Imesalia kudhihirika mzozo huu utuchukua mkondo gani, na iwapo mkwamo uliopo utatatuliwa.