Je, nini kiwe kipimo cha adhabu shuleni?
- Esther Namuhisa
- BBC Swahili

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna madhara makubwa ya viboko
Walimu wawili nchini Tanzania leo wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba na kusomewa shtaka la mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Msingi Kibeta Sperius Eradius mwenye umri wa 13,ambaye walimshutumu kuiba mkoba.
Hatua hiyo ya walimu Respicius Patrick Mtazangira na Herieth Gerald kupelekwa mahakamani imeibua mjadala mzito katika mitandao ya kijamii, ikiwa wengine wakipinga adhabu hiyo ya viboko shuleni na wengine kutaka utaratibu ufuatwe.
Dr.John Kalage ambaye ni mkurugenzi wa asasi ya Haki Elimu anasema hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya kuwafikisha walimu waliotuhumiwa kupiga mpaka kuua ni hatua nzuri ingawa kuna uhitaji wa kuwa na suluhisho la kudumu.
Taasisi ya Haki Elimu Tanzania inasema tukio hilo la mtoto kuuwawa halikuwashangaza sana kwa sababu sio mara ya kwanza kwa matukio kama hayo kutokea .
"Sheria zipo lakini hakuna uangalizi,hivyo ni wakati muafaka sasa sheria hizo kuzingatiwa na vilevile jamii inapaswa kuzifahamu kwa sababu watu wengi hawazijui hizo kanuni ndio maana matatizo yanaendelea kuepo" Dr.Kalage alieleza.
Wapo watu ambao bado wanaunga mkono adhabu ya viboko na wanaopinga desturi hiyo.
Utamaduni wa viboko unadaiwa kuepo enzi na enzi lakini ikumbukwe kuwa mataifa mengine wameacha kutumia utaratibu huo.
Na Dr.Kalage aliendela kusisitiza kwamba hakuna mfumo mzuri wa utoaji adhabu ambao unajulikana na wazazi,walimu ,watoto na wadau wa elimu.
Ripoti ya Unicef ya mwaka 2011 iliainisha ukatili mkubwa katika shule pamoja na usalama wao upo kwa asilimia 50.
Inawezekana kuna walimu ambao hawajui sheria inamtaka afanye kazi vipi au atoe adhabu ipi na wazazi wanapaswa kuongeza jitihada katika kuimarisha malezi kwa watoto,mmomonyoko wa maadili na jukumu la malezi ni changamoto.
Hakuna mifumo thabiti ya ulinzi wa watoto ,sheria na adhabu hazitolewi kwa utaratibu.Hivyo kama matukio kama hayo hayatachukuliwa hatua basi asasi kama zao zitaendelea kuzungumza kwenye vyombo vya habari kila tukio litakapotaarifiwa.
Mwanafunzi mwingine kupigwa mpaka kuzimia
Licha ya Tanzania kuridhia mikataba ya kimataifa ya haki za watoto ,Tanzania bado inatumia adhabu ya viboko.
Waraka wa sheria ya elimu Tanzania unapingana na katiba na sera ya watoto.
Ananastazia Rugaba ,meneja utetezi wa asasi ya TWAWEZA anasema wao wanapingana na adhabu ya viboko lakini wanaamini kwamba kuna adhabu mbadala ya viboko.
Nidhamu shuleni inapaswa kuzingatia utu wa watoto, Mtu anayetoa adhabu viboko mara nyingi anakuwa anajiridhisha yeye mwenyewe binafsi na sio kutoa fundisho.
Kuna adhabu mbadala ambazo wao pamoja na wadau wengine wa elimu walishawahi kutoa mapendekezo.
Serikali ilihaidi kutoa adhabu mbadala lakini mpaka leo hakuna utekelezaji.
"Hakuna kanuni au kumbukumbu juu ya taarifa ya namna ya kutoa adhabu shuleni.
Kuna kanuni inayokataza walimu kutembea na fimbo lakini hakuna mtu anayefuatilia.
Mwalimu mkuu ndio mwenye mamlaka ya kuruhusu kimaandishi na viboko visivyozidi vinne ndio vitumike kwa makosa makubwa na viandikwe katika kitabu cha kumbukumbu lakini hakuna ufuatiliaji wa hilo"Annastazia alieleza.
Chanzo cha picha, TONY KARUMBA
Wanafunzi wa kike hawaruhusiwi kuchapwa na mwalimu wa kiume
Vilevile waraka unaelekeza mwanafunzi wa kike haruhusiwi kuchapwa na mwalimu wa kike tu au mwalimu mkuu.
Bi.Annastazia alisisitiza kwamba uchapaji wa fimbo mara nyingi unaridhisha hasira ya mwalimu binafsi na sio kufuata utaratibu.
Utoaji wa adhabu haufuati kanuni wala mchapaji hana lengo la kufundisha ila kujiridhisha yeye, lengo la adhabu inabidi liwe ni kumfanya mtu ajifunze na kujirekebisha na sio kumuumiza.
Kuna madhara mengi ambayo yanasababishwa na viboko.
Chanzo cha picha, TONY KARUMBA
Viboko vinapunguza uwezo wa kufikiri
Fimbo inauwa ubunifu,inasababisha watoto kuwa waongo na kuwafanya wawe waoga.
Mtoto anaweza kudanganya ili aweze kuepuka adhabu ya fimbo kitu ambacho sio sahihi katika makuzi ya watoto.
Viboko vinalazimisha watoto kukariri na kupunguza uwezo wa kufikiri.
Maonyo huweza kuwa maneno au vitendo elekezi na si viboko.
Asilimia 98 ya watoto wamedai kuwa wamekumbwa na adhabu ya kiboko
Hatuwezi kusema walimu hao wameua ilikuwa bahati mbaya kawa sababu kwenye kuua hakuna bahati mbaya.
Walimu huwa wanapewa mafunzo juu ya utaratibu wa kutoa adhabu sasa iweje tuone kuwa tatizo likitoa basi ni bahati mbaya.
Ufuatiliaji ndio jambo la msingi kwa sababu tunashindwa hata kujitathmini tulipotoka na tulipo.
Miezi michache iliyopita kulikuwa na video inatembea ikionyesha wanafunzi wanapigwa sana,mjadala mkubwa ulitokea lakini baada ya siku chache jambo hilo lilisahaulika na sasa limetokea kubwa zaidi hivyo lazima utatuzi wa kudumu ufikiwe.
Unaweza kukuta mwalimu anampiga mtoto kila siku kwa sababu anaandikia mkono wa kushoto,je hapo mwanafunzi ana kosa gani?
Mtoto kachelewa shule badala ya kusikilizwa tatizo lake anapigwa wakati mwalimu anajua jinsi wanafunzi wanavyonyanyaswa katika daladala.
Chanzo cha picha, Alamy
Adhabu nyingine kuna uhitaji wa kuita wazazi vilevile kuna magereza ya watoto walioshindikana.
Kujifunza kwa viboko ni mila na desturi ambayo hatutaki kukumbatia.
Meneja wa programu kutoka mtandao wa elimu Tanzania(TEN/MET) Nichodemous Shauri amesema kuna ulazima wa kuwepo kwa malengo ya muda mrefu kwa adhabu hiyo ya viboko kuondolewa.
Sheria zizingatiwe na wazazi wawe sehemu ya shule.
"Hii kesi ya mauaji ya mwanafunzi inayosikilizwa sasa ni kiashiria kidogo tu cha ukatili ambao unaendelea kufanyika dhidi ya watoto nchini Tanzania.
Wiki iliyopita nilikuwa Mbulu na nilishuhudia walimu wakitumia muda mwingi kuwaadhibu watoto zaidi ya kuwafundisha.
Sera na sheria za elimu zipo lakini utekelezaji wake ni mbaya ,kila mwalimu anatandika tu wanafunzi anavyojisikia,"Shauri alisema.
Chanzo cha picha, ROBERTO SCHMIDT
Meneja wa programu kutoka mtandao wa elimu Tanzania(TEN/MET) Nichodemous Shauri aliongeza kwa kubainisha kuwa ni shule za umma ndio zimekubuhu katika adhabu hii tofauti na shule za binafsi.
Watoto wa walalahoi ndio wanakumbana na janga hili la viboko kwa kiwango kikubwa ,na unakuta wazazi wao pia hawana elimu hivyo hawawezi au wanashindwa kufuatilia kwa karibu .
Mara nyingi katika kamati unakuta wazazi wanaochaguliwa ni wale ambao wana uwezo wa kuongea sana bila ya kuangalia uwezo wa elimu yao.
Tofauti na shule binafsi ambapo hawatumii fimbo lakini bado tunaona kuna utofauti mkubwa wa matokeo yao ya ufaulu kuwa mazuri.
Kama kuna mila na desturi ambazo tuliwahi kuwa nazo na ziliisha basi viboko pia ni wakati wake viishe,mfano mila ya tohara kwa wanawake iliisha sasa ifike mahali fimbo pia zisitishwe.
Wazazi wanapaswa kuwa karibu na shule na wawe wafuatiliaji wa maendeleo ya shule.
Fimbo zinachapwa kila mahali ,hilo ni moja tu ambalo limeibuka lakini wanafunzi wanapigwa sana hata majumbani kutoka kwa walezi na wazazi .