Ni kwa nini wanasiasa wanavihama vyama vyao nchini Tanzania

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania
Rais wa Tanzania John Magufuli

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania John Magufuli

Hatua ya madiwani na wabunge kuhama vyama vya upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania imekuwa gumzo baada ya kushuhudia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiwapoteza madiwani 8 ndani ya siku 7 kuanzia Agosti 21 hadi 26 mwaka huu.

Madiwani waliohama Chadema na kwenda CCM katika kipindi cha siku 7 ni Kata Hazina (Dodoma), Kata ya Namilembe (Ukerewe mkoani Mwanza), Kata ya Kingori (Arumeru), Kata ya Mabatini (Nyamagana mkoani Mwanza), Kata yaNdumet (Siha mkoani Kilimanjaro),Kata ya Korongoni (Moshi, mkoani Kilimanjaro), Kata ya Masama Rundugai (Hai, mkoani Kilimanjaro) na Kata ya Kikwe (Arumeru).

Zaidi ya madiwani 146 wanatajwa kuvihama vyama vya upinzani. Hadi sasa madiwani waliojiuzulu Chadema na kujiunga CCM wamefikia 137, huku wale waliotoka Chama cha Wananchi (CUF) ikifikia 9.

Tangu kuingia kwa utawala mpya wa Rais John Magufuli mwaka 2015 hadi sasa umeshuhudia wabunge watatu wa Chadema, Dk. GodwinMollel (Siha), Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli) ambao wamehamia CCM ambako ameteuliwa tena kugombea majimbo hayo katika uchaguzi mdogo ujao.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa chama cha CCM

Wabunge wengine ni Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Mohamed (Liwale) wote kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao wamehamia CCM. Mtulia ni mbunge wa jimbo hilo hilo alilohama lakini sasa amepitia chama kipya alichohamia CCM.

Kwa mujibu wa vifungu vya 37 (1)b na 46(2) vya sheria ya uchaguzi inaipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini kutangaza jimbo kuwa wazi na kuitisha uchaguzi mdogo.

Taarifa kutoka Tume hiyo zimesema kuwa uchaguzi mdogo unatarajiwa kufanyika Septemba 16, utakaojumlisha kata 23 Tanzania Bara na mwingineOktoba mwaka huu hususani jimbo la Liwale mkoani Lindi pamoja na Kata mbalimbali.

WANANCHI WAMEGAWANYIKA

Hama hama ya wanasiasa kutoka vyama vya upinzani kwenda CCM imezua mjadala mkali nchini Tanzania huku zikitolewa sababu mbalimbali ambazo zimegawanyika katika makundi manne ambayo yanakinzana kwa kiasi kikubwa huku yakikubaliana kwa sehemu ndogo sana.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Aliyekuwa mgombea urais wa chama cha (CHADEMA) Edward Lowasa

Kundi la kwanza: Ni lile linaloamini kuwa wanasiasa hao wamenunuliwa. Kwamba wanasiasa hao wamekubali kununuliwa kama bidhaa sokoni kutokana na kuwa wepesi kupokeafedha, jambo ambalo halijathibitishwa hadi leo kwa nyaraka zozote rasmi au kauli.

Kundi la pili; Duru za kisiasa zinasema kuwa hotuba ya Rais Magufuli Julai 28 mwaka huu wakati akitangaza uteuzi wa Makatibu tawala,wizara na wakuu wa wilaya alisema haiwezekani awateua yeye halafu kwenye matokeo ya uchaguzi wawatangaze washinde kutoka upande wa upinzani.

Katika hotuba hiyo alitangaza makatibu tawala wafuatao; Abubakar Musa (Dar es Salaam), David Kafulila(Songwe), Denis Bandisa (Geita), Happy William (Iringa), Abdallah Malela (Katavi), Rashid Chatta(Kigoma), Masaile Mussa (Manyara),Carolin Mpapula (Mara), Dk. Jerry Mareko (Mtwara), Christopher Kadio (Mwanza), Eric Chitindi (Njombe), na Riziki Salas(Ruvuma).

Makatibu wa Wizara; Andrew Masawe (Ofisi ya Waziri Mkuu), Elissante Gabriel (Wizara Uvuvi na Mifugo), Dk. Jimmy James(Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi), Edwin Muhede (Wizara Viwanda Biashara na Uwekezaji). Na Wakuu wa Wilaya, Jerry Murro (Arumeru, Patrobas Katambi (Dodoma), Jokate Mwegero (Kisarawe).

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa CHADEMA

Hatua hiyo inatafsiriwa kwakuwa yeye ni Mwenyekiti wa CCM, maana yake anataka kuona washindi wanaotangazwa ni wale wanaotokana na chama chake sio kinyume.

Kundi hili ambalo lina mashabiki wengi kutoka chama tawala ambao wanaamini Mwenyekiti yuko sahihi kwa kauli hiyo kwakuwa ndiye mteule wao, ikizingatia nafasi za katibu tawala na mkuu wa wilaya ni za kisiasa ambazo wengi wao wanaoteuliwa sasa ni makada wa CCM.

Vitimbi vilivyotokea katika uchaguzi mdogo wa Korogwe Vijijini, ambapo mgombea wa Chadema kuambiwa amechelewa kuwaisilisha fomu hivyo mgombea wa CCM Timothea Mzava kutangazwa kupita bila kupingwa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu baada ya kujikuta pekee yake ametimiza sharti la kurudisha fomu muda wa mwisho Agosti 20, 2018. Tukio hilo limelalamikiwa na Chadema wakidai mgombea wao Amina Ally alifanyiwa hila.

Sababu za hila hizo kuchelewa muda wa mwisho kurudisha fomu ambao ni saa 10 jioni. Mazingira yanaonyesha kulikuwa na mambo yasiyo ya kawaida hadi kusababisha fomu ya Amina Ally Saguti kutopolekewa kwa muda sahihi, kwa sababu msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo Dk George Nyaronga hakuwa na sababu nyingine yoyote kutopokea fomu hiyo.

Hali hiyo imeibua mgawanyiko kwa sababu wananchi wapo makundi tofauti hivyo kila upande unapata waungaji mkono na kuwa chanzo cha minyukano.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wananchi wakisubiri kupiga kura Tanzania

Kundi la tatu: Linaamini ni vuguvugu la kisiasa linalotokea ndani ya vyama tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi. Kundi hili linatolea mfano uamuzi wa aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu wa zamani, Augustine Mrema aliyeihama CCM na kujiunga chama cha NCCR-Mageuzi mwaka 1995, kasha kutikisa katika uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na madiwani mwaka huo.

Aidha, linatolea mfano wa mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye ambao walihama CCM na kwenda Chadema miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani mwaka 2015 pamoja na wimbi la wanasiasa waliohamia upinzani mwaka huo.

Vilevile linajenga hoja kuwa katika utawala wa marais mbalimbali nchini Tanzania, kumekuwa na wimbi la wanachama wapya wanaopokelewa ndani ya CCM ingawa halikuwa jambo maarufu kama ilivyo sasa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Tume ya Uchaguzi Tanzania

Kundi la nne; Linatazama hama hama hizo kuwa ndani ya vyama vya upinzani kuna migogoro ambayo huchochea baadhi ya wanasiasa kuhama.

Duru za kisiasa zinasema ndani ya chama kikuu cha upinzani hali si shwari kutokana na mgawanyiko wa makundi mawili; kundi la Chadema asilia ambalo ndio wenyeji ambao wanahisi kutengwa, huku kundi la pili Chadema academia likichukua hatamu katika fursa za uongozi. Chadema Academia ni kundi la wanasiasa waliohamia chama hicho wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015 likiongozwa na wafuasi wa Edward Lowassa, ambalo sasa linaonekana kukiteka zaidi chama na kuwa na ushawishi mkubwa kuliko kundi la kwanza la Chadema asilia ambao wanajiona kupoteza nguvu na ushawishi ndani ya chama walichokipigania kwa hali na mali.

Aidha, mgogoro wa Chama cha CUF ulisababisha kumeguka makundi mawili ya Katibu Mkuu Maalim Seif na Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba. CUF ya Maalim Seif imekataa kumtambua Lipumba kwa kile ilichoeleza kujiuzulu mwenyewe mwaka 2015 , hivyo hakuna kikao kilichoidhinisha yeye kurejea madarakani ndani ya chama hicho.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Shughuli ya upigaji kura

Mgogoro huo umesababisha CUF kupoteza wabunge 8 wa viti maalumu baada ya kambi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba na Kaimu Katibu Mkuu Magdalena Hamisi Sakaya kumwandikia barua Spika wa Bunge Job Ndugai mwaka jana kuwa wamefukuzwa unachama. Wabunge hao ni Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed.

Kwa mujibu wa kifungu cha 67(1)(b) cha Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977 na kifungu 37(3) cha Sheria ya Uchaguzi Sura 343 ya Mwaka 2015, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alifanya uteuzi mpya wa wabunge 8 wa viti maalumu kuwakilisha Cuf.

Hali hii imechochea vurugu ndani ya chama na kusababisha baadhi viongozi wa kambi ya Maalim Seif kuhamia CCM akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Muda ya Cuf, Julius Mtatiro.

MASLAHI BINAFSI

Hatua ya Rais Magufuli kuwapa madaraka baadhi ya wanasiasa waliotoka vyama vya upinzani imetajwa na wachambuzi kuwa kiini cha hama hama hiyo kwani wanaichukulia kama fursa inayoweza kupatikana kwao kulikowakibaki upinzani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Katibu mkuu wa chama cha (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad

Wanasiasa waliohamia kutoka upinzani na kupewa vyeo ni mbunge wa zamani wa Kigoma kusini, David Kafulila (Katibu Tawala Mkoa wa Songwe), Patrobas Katambi (MkuuwaWilayaya Dodoma) na Moses Machali(Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mtwara). Pamoja na baadhi yao waliotanguliwa kupata uteuzi, kama vile Anna Mghwira(Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro) na Profesa Kitila Mkumbo (Katibu Mkuu wizara ya Maji).

Chama tawala ni tofauti na upinzani kwa sababu zipo fursa nyingi ambazo zinawindwa na wanasiasa, ndiyo kusema hawawezi kuacha kuhamia huko na kusisitiza kuwa wanamuunga mkono Rais Magufuli kama kete yao ya kusikika.

Aghalabu wanasiasa wanapokubali kuunda umoja wowote wa kisiasa sababu kubwa ni masilahi. Kama masilahi hayo yakikosekana au wenginekupunjwa, kutengwa au uonevu lazima migogoro itaibuka ndani ya chama au muungano wa kisiasa.

Wapo wanasiasa waliohama CCM kwenda upinzani kwasababu ya kusaka fursa, mara zilipokosekana huko waligeuza shingo kurudi walikotoka ili kutafuta masilahi.

GHARAMA ZA UCHAGUZI MDOGO

Akizungumzia gharama za uchaguzi mdogo Mkurugenzi wa NEC, Dk. Athumani Kihamia aliliambia gazeti moja kuwa gharama zinategemea na ukubwa wa eneo husika (Kata na Jimbo) pamoja na idadi ya wagombea.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Makaratasi ya kupigia kura

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima, mapema Novemba mwaka jana alikaririwa na gazeti moja la kila siku wakati wa uchaguzi mdogo wa kata 43 kuwa ungegharimu Sh bilioni 2.5.

Aidha, alisema baadhi ya Kata ingetumia Shilingi milioni 20 kutokana na idadi ndogo ya vituo vya kupigia kura na vyenye idadi kubwa hugharimu Shilingi milioni 150.

ANGUKO LA ITIKADI

Augustine Mrema aliyehama CCM mwaka 1995 hakuonekana kuwa na itikadi nyingine zaidi ya ile aliyolelewa ya CCM. Kwa hiyo alipohamia NCCR-Mageuzi hakukuwa na msingi wowote wa kiitikadi zaidi ya kasumba zilizozoeleka. Vilevile wanasiasa Lowassa, Sumaye,Mwita Waitara, Julius Kalanga, Dk. Godwin Mollel walihamia vyama vyenye itikadi tofauti na walivyolelewa

Dk.Jonathan Floyd wa Chuo Kikuu cha Bristol katika kitabuchake cha "Is Political Philosophy Impossible?:Thoughts and Behaviour in Normative Political Theory," ameandika kwamba ni vigumu kwa mwanasiasa, chama cha siasa na siasa kuepuka misingi ya falsafa na itikadi yake kwa sababu kuna kanuni na taratibu zinazowekwa n akufuatwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanamke akitafuta kwenye sajili ya wapiga kura

Ameongeza ni vizuri kupima pia tabia zao kuliko nini wanachokifikiri. Matendo ya wanasiasa yanazungumza zaidi kuliko sauti zao zinavyosikika kila mara mbele ya wananchi, ameandika Dk.Jonathan Floyd katika kitabu hicho.

MTAZAMO WANGU

Wanasiasa kuhama vyama ni jambo linalofahamika vema, lakini kuna yale yanayokuwa si ya kawaida kama inavyotokea sasa nchini Tanzania. Iwe wananunuliwa au hawanunuliwi, msingi wa kwanza wa mwanasiasa katika siasa ni kutafuta madaraka, jambo ambalo linawafanya wahangaike huku na huko pamoja na kutumia kila mbinu iwe nzuri au chafu kuhakikisha wanapata kile wanachotaka bila kujali kama wamewaumiza wengine katika safari yao ya kushika madaraka.

Sura halisi ya mwanasiasa inaonekana pale anapotaka madaraka kwa namna yoyote ile. Madhara ya hama hama hii kwa upande wa madiwani na wabunge ni taifa kutumia bajeti za chaguzi ndogo kila mara badala ya kuendeleza miradi ya maendeleo katikati ya taifa ambalo linategemea wahisani kutekeleza bajeti zake.

Suluhisho ni kubadili Katiba katika maeneo hayo, kwamba diwani au mbunge anayekihama chama chake na kwenda kingine hataruhusiwa kugombea ubunge katika jimbo husika hadi kipindi cha miaka mitano kimalizike.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Baada ya kupiga kura

Kwa mfano, wabunge ambao walichaguliwa mwaka 2015 vipindi vyao vinamalizika mwaka 2020. Kwahiyo mbunge akijitoa chama cha upinzani au tawala wakati huu, hataruhusiwa kugombea kwenye uchaguzi mdogo hadi kipindi chake kimalizike mwaka 2020 ambapo anaweza kugombea tena.

Bila kubadili sheria hizi, taifa letu litakuwa linatanga tanga kuomba fedha za wahisani wakati tunachezea fedha kwa chaguzi ndogo ndogo huku wananchi wanaishi kwenye umasikini wa kutisha.

Suala hili haliwezi kuishia katika kipindi hiki cha Rais Magufuli pekee, badala yake hama hama ya wanasiasa itaendelea katika vipindi mbalimbali vijavyo, kitakachobadilika ni sababu za kuhama kwao kutoka CCM kwenda upinzani au upinzani kwenda CCM.