Mfuko huu wa kubebea vitu vya watoto una nusuru maisha ya akina mama Nigeria

Peju Jaiyeoba amesambaza vifaa laki tano vya kujifungua vilivyosalama nchini Nigeria -mfuko ulio na vifaa muhimu ili kuhakikisha kuwa akina mama wanajifungua kwa njia salama na ilio safi
Maelezo ya picha,

Peju Jaiyeoba amesambaza vifaa laki tano vya kujifungua vilivyosalama nchini Nigeria -mfuko ulio na vifaa muhimu ili kuhakikisha kuwa akina mama wanajifungua kwa njia salama na ilio safi

"Mara nyengine mimi hutamani kwamba siku moja kazi yetu haitahitajika tena", anasema Adepeju Jaiyeoba, mwanzilishi wa wakfu wa Brown Button nchini Nigeria.

Miaka saba iliyopita , Adepeju ama Peju kwa ufupi, aliwacha kazi iliyokuwa ikimpatia mapato mazuri ya uwakili na kuanza kujifunza ukunga wa kitamaduni nchini Nigeria ili kuzalisha watoto.

Pia alitengeneza mfuko wa kuweka vifaa vya matibabu ambao umepata soko kubwa katika maeneo ya mashambani nchini Nigeria ukiokoa maelfu ya maisha.

Marafiki zake na familia walijaribu kumrai kutowacha kazi yake ,lakini kifo cha rafikiye wa karibu wakati wa kujifungua hakikumpa chaguo mbadala.

''Rafiki yangu alikuwa ana elimu ya kutosha na ilinifanya mimi kuketi chini na kufikiria kwamba iwapo mtu ambaye ana uwezo wa kifedha anaweza kufariki wakati wa kujifungua, je ni nini kinachofanyika katika maeneo ya mashambani ambapo hawana vifaa vya kuzalisha?''

''Nilikuwa sina chaguo jengine kwani sikutaka kupoteza mtu mwengine tena. Sidhani kwamba hatua ya kujifungua mtoto inapaswa kusababisha kifo cha mtu mwengine''.

Maelezo ya picha,

Mtoto anazaliwa katika mkeka kutoka kwa mfuko mmoja wa vifaa unaouzwa na wakfu wa Brown Button nchini Nigeria

Kuchukua hatua

Pamoja na nduguye wa kiume ambaye ni daktari alielekea kaskazini mwa Nigeria kujua ukweli kuhusu vile wanawake wa mashambani wanavyojifungua.

Kile alichogundua kilikuwa kinatisha.

''Tuliona wanawake wakijifungua katika sakafu , tuliwaona wauguzi wakitumia midomo yao kuvuta makamasi ya watoto wachanga ili kuzuia asphyxia'', alisema.

''Tuliwaona wahudumu wa kujifungua wakikata vitovu vya watoto kwa kutumia visu vilivyo na kutu na vigae, na hivyobasi kuwa rahisi kwa wao kupata ugonjwa wa tetanus na wengi wakifariki''.

''Vitu kama vile kuosha mikono ni tatizo na kuvaa glovu ni kitu kikubwa sana. Kila siku nchini Nigeria mimba 118 huishia katika kifo. Taifa hilo lina mojawapo ya idadi kuu za vifo wakati wa kujifungua dunia''

''Hatua hiyo ni hatari sana kulingana na Peju, kiasi kwamba imechukua mweleko wa kidini na wanawake hupendelea sana kujifungua katika kliniki za kitamaduni ambapo dawa za miti shamba hutumika sana badala ya vifaa vilovyosafishwa''.

Maelezo ya picha,

Vifaa vilivyopo katika mfuko wa peju hutumika mara moja pekee ili kupunguza viwango vya maambukizi

Peju alianzisha wakfu wa Brown Button ili kuwafunza wahudumu wa kuzalisha akina mama kuhusu mbinu mpya za kuzalisha.

Hakujua wakati huo kwamba huku akiendelea kuwafunza, wakfu huo ungetoa soko la mifuko hiyo.

''Niligundua kwamba vitu tunavyonunua mjini Lagos, viko bei ghali zaidi kaskazini mwa Nigeria. Bei ya glovu kwa mfano inaweza kuwa ghali mara tatu''.

''Walinunua pakiti 30 za mwanzo huku wakijadiliana na watengenezaji wake kwa lengo la kuuziwa kwa bei rahisi, rahisi zaidi ya bidhaa zinazouzwa mjini Lagos na hata rahisi zaidi ya bei za bidhaa hizo mashambani''.

Maelezo ya picha,

Wanawake wajawazito wanajifunza kuhusu mfuko huo wakati wanapokwenda kliniki ya ujauzito kupimwa

''Watu wengine walituambia kwamba hatutaweza kugharamikia bei ya mfuko huo'', Peju anasema.

''Lakini wana kipindi cha miezi tisa kuchangisha katika mfuko huo, na iwapo kila wanapokuja kutizamwa wakiwa kwa ujauzito, basi watakapokuja kujifungua, watalipiwa.''

''Mifuko hiyo ina vifaa 13 tofauti ikiwemo, dawa ya kusafisha, glavu, na kisu cha kukatia kitovu, mkeka mdogo wa kulalia wakati wa uchungu na dawa zinazopunguza kuvuja kwa damu wakati wa kujifungua. Kila mfuko unagharimu dola nne za Marekani na idadi kuu ya vifaa hivyo hutengezewa nchini Nigeria.''

Maelezo ya picha,

Wanawake wanaweza kulipia mfuko huo wa dola nne kidogokidogo katika kipindi cha miezi tisa cha uja uzito

Katika kipindi cha miaka minne iliopita, Wakfu wa Brown Button umefanikiwa kusambaza mifuko laki tano ya kujifungulia.

Hatua inayoshirikisha kutoa mafunzo na usambazaji wa mifuko hiyo imezuia viwango vya vifo kupitia kuvuja damu wakati wa kujifungua kwa robo katika maeneo ambayo hutokea sana, kulingana na wakfu huo.

''Vifaa vinavyotumika katika kuwazalisha salama akina mama ni muhimu kwani husaidia kuzuia maambukizi kati ya mama na mtoto anapozaliwa na hilo ni wazo zuri kwa sababu maambukizi ni mojawapo ya vifo wakati wa kujifungua'', anasema Bosede Afolabi , Profesa wa Ukunga katika chuo kikuu cha mafunzo cha hospitali ya Lagos

''Iwapo una glavu safi , eneo zuri la kuzalisha na kifaa safi cha kukata kondo la nyuma na kitovu basi viwango vya kupata maambukizi hupungua''.

Maelezo ya picha,

Picha ya Peju aliyopigwa akikutana na Barrack Obama ameiweka katika meza yake ya kufanyia kazi na anajivunia sana

Obama au utapeli wa simu?

Siku moja Peju aliwasili katika afisi yake akapata ujumbe kutoka kwa mtu wa ikulu ya rais Barrack Obama huko Whitehouse Marekani.

Alienda nyumbani na kumwambia mumewe kuhusu ujumbe huo na wakakubaliana kwamba ujumbe huo ni utapeli wa simu.

''Usimpatie mtu yeyote neno lako la siri la simu ama nambari yako ya akaunti'', mumewe alimwambia.

Lakini ni kweli ulikuwa mwaliko kutoka Ikulu ya Whitehouse. Walikuwa wanawakaribisha wafanyibiashara kutoka kila bara na Peju ndiye aliyechaguliwa bara Afrika.

''Nakumbuka kuingia katika Ikulu ya whitehouse na kuhisi kama ndoto'' ,alisema. ''Tulizungumza kuhusu uwekezaji barani Afrika na huduma ya afya. Hili lilileta mafanikio makubwa katika kile nilichokuwa nikifanya''.

Maelezo ya video,

Mfuko wa uzazi unao nusuru maisha ya akina mama Nigeria

Kipindi hiki cha BBC kiliandaliwa kupitia ufadhili wa wakfu wa Bill na Melinda Gates