Wanafunzi wa kike walala uwanjani baada ya kufukuzwa shule kutokana na karo na matokeo mabaya Kenya

Darasa ambalo halina wanafunzi Kenya

Wasichana 34 wa shule ya upili ya Nasokol katika kaunti ya Pokot magharibi nchini Kenya walifukuzwa shule siku ya Jumanne kutokana na matokeo mabaya ya mtihani.

Waschana hao ambao wengi wao ni wachezaji kandanda walifukuzwa na mwalimu wa shule hiyo.

Walikuwa wakipiga kambi katika uwanja wa maonyesho ya kilimo ya Kitale siku ya Jumanne alfajiri.

Wanafunzi hao wa kidato cha kwanza na cha pili ambao ni wachezaji waliopo katika mpango wa masomo ya ufadhili walilazimika kulala katika uwanja huo.

Walifurushwa na mwalimu mkuu mpya ambaye alifutilia mbali sera ya mtangulizi wake ambaye alikuwa akiwahurumia wanamichezo kuhusiana na karo ya shule na matokeo ya masomo.

Mmoja wa wanafunzi hao aliambia kituo cha habari cha Nation kwamba mwalimu huyo mpya amekuwa akilalamika kuhusu matokeo mabaya ya wanafunzi waliobora katika michezo.

''Mwalimu mkuu amekuwa akituambia kwamba tutafute shule nyengine ambapo michezo inapatiwa kipaumbele ikilinganishwa na masomo''.

Walikosana Mwalimu mkuu

Wazazi hao wanasema kuwa mwalimu huyo mkuu mpya aliwataka kuwasili katika shule hiyo siku ya Jumatatu na kuwaelezea kuhusu sera hiyo mpya ambayo inawahitaji wanafunzi wote kulipa karo ya shule, ikiwemo wale walio katika ufadhili wa michezo.

''Tuliwasili katika shule alfajiri lakini ni nyakati za jioni ndiposa mwalimu mkuu alituarifiu kwamba ni sharti tulipe karo za shule la sivyo tuwapeleke watoto wetu kwa shule nyengine'', alisema Thomas Wabomba mzazi kutoka Kakamega.

Wengi wa wanafunzi walioathirika walichukuliwa katika shule nyengine kwa talanta yao ya soka na wamekuwa wakisoma bila kulipa karo.

''Tulijaribu kuafikiana mkataba na mwalimu mkuu kuhusu utaratibu wa kuanza kulipa karo lakini hakutaka kutusikiza, akisema kuwa tuko huru kuwapeleka watoto wetu shule nyengine'', alisema bwana saulo Tukoi ambaye ni mzazi.

Baada ya kukosana na usimamizi wa shule hiyo kuhusu mwelekeo , baadhi ya wazazi waliamua kuwahamisha wanafunzi wao na wakaagizwa kuondoka mara moja katika shule hiyo siku ya jumatatu jioni.

Ilimlazimu msamaria mwema kuingilia kati na kuwasafirisha hadi kitale wazazi na wanafunzi waliokuwa wamekwama nje ya lango la shule hiyo.

"Nilikodisha matatu mbili ambazo ziliwasafirisha hadi Kitale baada ya kugundua kwamba wamekwama. Tulijadiliana na usimamizi wa uwanja wa maonyesho ya Kitale kuwahifadhi kwa usiku mmoja katika uwanja huo'', alisema Moses Ngeiywa.