Donald Trump akana kupanga njama za mauaji ya rais wa Syria Bashar al-Assad

Bwana Trump anasema kuwa wazo hilo halikuzungumziwa na maafisa wa ulinzi.

Rais wa Marekani Donald Trump amekana madai ya mwandishi maarufu Bob Woodward katika kitabu chake kipya kwamba aliamrisha mauaji ya rais wa Syria Bashar-al-Assad.

Bwana Trump anasema kuwa wazo hilo halikuzungumziwa na maafisa wa ulinzi.

Waziri wa ulinzi James Mattis pia amekana madai ya maneno aliyotoa katika kitabu hicho. Rais Trump tayari ameshutumu kazi hiyo mpya kama 'kuwalaghai' raia na ya 'uongo'.

Woodward ni mwandishi wa muda mrefu ambaye alisaidia kuweka wazi jukumu la rais Richard Nixon katika kashfa ya Watergate 1970.

Siku moja baada ya nakala za kitabu hicho kuchapishwa katika gazeti la The Washington Post, gazeti jingine la The New York Times lilichapisha maoni yaliotolewa na afisa mwandamizi katika Ikulu ya Whitehouse akisema kuwa kiini cha tatizo la utawala wa rais Trump ni ukosefu wa 'maadili'.

Afisa huyo anasema kuwa maafisa wa serikali walioteuliwa na Trump waliapa kusitisha amri za rais Trump.

''Huenda kuna baridi nyingi wakati huu lakini raia wa Marekani ni sharti wajue kuna 'watu wazima' katika chumba hiki'', maafisa hao wanaongeza.

''Tunatambua kinachoendelea .Na tunajaribu kufanya kilicho sawa hata iwapo Donald Trump hatofanya''. Baadaye siku hiyo, bwana Trump aliambia mkutano wa maafisa wa polisi wa kieneo kwamba kitabu hicho kina aibu.

Msemaji wake Sarah Sanders alisema katika taarifa kuhusu mwandishi huyo ambaye hakutajwa. ''Huyu muoga anafaa kufanya kilicho sawa na kujiuzulu''.

Ni nini kilichosemwa kuhusu Assad?

Kitabu hicho kinasema kuwa bwana Trump aliagiza idara ya ulinzi nchini humo kupanga mauaji ya rais huyo wa Syria kufuatia shambulio la kemikali dhidi ya raia mnamo mwezi Aprili 2017 ambalo lililaumiwa kutekelezwa na serikali ya Syria.

''Twendeni. Tuwaue'', bwana Trump aliripotiwa akimwambia bwana Mattis.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Trump alivyosema kuhusu Assad: Tumuue.

Kitabu hicho kinasema kuwa bwana Mattis alitambua ombi la Trump lakini baadaye akamwambia msaidizi wake kwamba hawezi kutekeleza hilo.

lakini akizungumz na waandishi siku ya Jumatano, rais huyo alisema : Hilo alikutajwa katika mazungumzo yoyote .Aliendelea kutaja kitabu hicho kuwa 'uongo'.

Ni nini chengine alichosema rais Trump?

Bwana Trump alituma misururu ya ujumbe wa twitter siku ya Jumanne jioni akishikilia maoni yake pamoja na taarifa kutoka kwa msemaji wa Ikulu ya whitehouse Sarah Huckabee Sanders.

Bwana Trump anasema kuwa nukuu zinazodaiwa kutolewa na Mattis na bwana Kelly ni za udanganyifu na hatua ya kuwalaghai raia.

Anasema kuwa kitabu hicho kilimshusha hadhi yake kwa uongo mwingi na vyanzo vya uongo, akikana madai kwamba alitumia maneno ya 'mtu punguani' na 'mjinga' ili kumuelezea mwanasheria mkuu Jeff Sessions.

Taarifa kutoka kwa Mattis zimeelezea kitabu hicho kuwa 'kitu cha mtu aliyejaa ubunifu mwingi'.

Taarifa hiyo kutoka kwa Kelly inasema: Wazo la kumwita Trump 'mjinga' sio la kweli....''kila siku anajua msimamo wangu na yeye pamoja nami anajua kwamba habari hii ni upuzi mtupu''.

Nini chengine kilichopo ndani ya kitabu hicho?

Woodward anasema kuwa mshauri wa kiuchumi Gary Cohn na katibu wa ikulku ya whitehouse Rob Porter alitoa stakhabadhi kutoka kwa rais ili rais Trump asizitie sahihi.

Stakhabadhi hizo zingemruhusu rais kuondoka kutoka katika biashara huru na mataifa ya Marekani kaskazini pamoja na mkataba wa kibiashara na Korea Kusini.

''Hii ni sawa na mapinduzi ya kiutawala'', alisema Wooward.