Bobi Wine: Nitarejea Uganda na kuendelea na siasa

Bobi Wine akizungumza na mwandishi wa BBC Zuhura Yunus.
Maelezo ya picha,

Bobi Wine akizungumza na mwandishi wa BBC Zuhura Yunus.

Mbunge wa Kyandodo Mashariki Bobi Wine ameiambia BBC kuwa atarudi Uganda na kuendelea na shughuli za kisiasa akimaliza matibabu yake ughaibuni.

Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi amesema hana woga wa kukabiliana na mkono wa dola katika harakati zake alizosema zinalenga kumuweka yeye na Waganda wote huru.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini Uganda kwa sasa yupo Marekani anapopatiwa matibabu baada ya kupigwa na vyombo vya dola.

Bobi Wine na wenziwe 32 walikamatwa baada ya kudaiwa kushambulia msafara wa Rais wa Yoweri Museveni mjini Arua mwezi uliopita na kuwekwa katika kizuizi cha jeshi.

Mwanzo alipandishwa katika mahakama ya kijeshi kabla ya kuhamishiwa kwenye mahakama ya kiraia na kushtakiwa kwa kosa la uhaini.

Akiongea na mwanahabari wa BBC Zuhura Yunus aliyemtembelea nchini Marekani Bobi Wine amesema alipokuwa kizuizini "askari walinipiga, walinidunda na kunifanyia mambo mengi."

Bobi Wine aliruhusiwa kuondoka Uganda Ijumaa baada ya kuzuiliwa awali na ameiambia BBC kuwa punde tu madaktari wake watakapomruhusu atarudi Uganda kuendelea na harakati za kisiasa.

"Nimekuja hapa kupata matibabu, lakini nitarudii nyumbani kwasababu Uganda ni nyumbani kwangu," amesema Bobi Wine na kuongeza, "Mimi ni kiongozi, baada ya matibabu nitarudi kuendelea na mambo ya siasa."

Chanzo cha picha, Getty Images

Alipoulizwa kama hana woga baada ya kupigwa na kudundwa,amesema: "Siwezi kuogopa kwasababu kila kitu wamefanya wanaweza kufanya lakini mimi siogopi."

Serikali ya Uganda imekuwa ikikanusha toka mwanzo ripoti kuwa Bobi Wine amepigwa na kuumizwa. Raisi Museveni alivinyooshea vidole vyombo vya habari kabla ya mbunge huyo kuachiwa akidai vinapotosha umma.

Hata baada ya kuachiwa na kuruhusiwa kwenda nje kwa matibabu serikali ya Uganda imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hawakumtesa.

"Hawa watu (serikali) wanajua mambo ya kudanganya tu. Wanaweza kufanya kitu halafu wanaongea kitu kingine. Lakini ukweli upo wazi," amesema.

Ndoto za Urais

Chanzo cha picha, Getty Images

Baadhi ya wachambuzi wanaona vuguvugu linaloendelea Uganda linaweza likwa chanzo cha kumng'oa Museveni Madarakani. Lakini je Bobi Wine ana ndoto za kuwania urais.

"Sina ndoto za kuwa rais kwa sasa. Sasa hivi nataka kuwa huru, na watu wa Uganda wanataka huwa huru bila kujali nani ni rais," amesema na kuongeza, " Haijalishi kama mtu yupo upande wetu (upinzani) au wa Museveni, wala mambo yetu si ya kumtoa Museveni. Tunataka kuwa huru katika nchi yetu."

Kwa mujibu wa Bobi Wine hata kuachiwa kwake na kuruhusiwa kwenda Marekani kwa matibabu si kielelezo cha uhuru wa mahakama ambayo iliamuru hivyo bali nguvu ya umma.

"Ilikuwa presha ya watu wa Uganda na nje ya Uganda iliowalazimisha serikali kutuachia. Bila presha ile sidhani kama wangetuachia. "