Ushoga: Mahakama ya Upeo ya India yaruhusu mapenzi ya jinsia moja

Wapigania haki za ushoga walilipuka kwa furaha na wengine walishindwa kuyazuia machuzi pale hukumu hiyo ilipokuwa ikisomwa.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Majaji wote watano wa Mahakama ya Upeo hiyo wakiongozwa na Jaji Mkuu wa India Dipak Misra walikubaliana kuwa ushoga sio kosa la jinai.

Mahakama ya Upeo nchini India imefanya maamuzi ya kihistoria, toka leo, kushiriki mapenzi ya jinsia moja si kosa la jinai nchini humo.

Hukumu ya leo inatengua maamuzi yaliyofanywa mwaka 2013 ambayo yalidumisha matumizi ya sheria ya kikoloni, maarufu kama kanuni ya 377 ambayo ilitia hatiani vitendo vya ushoga.

Mahakama sasa imeamua kuwa kuwabagua watu kutokana na mahusiano yao ya kimapenzi ni ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Maelezo ya picha,

Ramani ya wapenzi wa jinsia moja

Wapigania haki za ushoga walilipuka kwa furaha na wengine walishindwa kuyazuia machuzi pale hukumu hiyo ilipokuwa ikisomwa.

Ijapokuwa maoni ya wengi kwenye miji mikubwa ya India yamekuwa yakiunga mkono ushoga, kuna upinzani mkali kutoka katika makundi ya kidini na wahafidhina hasa maeneo ya vijijini.

Majaji wote watano wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji Mkuu wa India Dipak Misra walikubaliana kuwa ushoga sio kosa la jinai.

Jaji Misra amesema kutia hatiani mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha katiba ya India. Jaji mwengine wa mahakama hiyo Indu Malhotra, amesema anaamini historia inabidi iiombe radhi jamii ya mashoga kwa kuwanyanyapaa.

Chanzo cha picha, Reuters

Jaji DY Chandrachud amesema serikali haina haki juu ya maisha binafsi ya mashoga na kuwanyima haki yao ya kufanya mapenzi ni sawa na kuwanyima faragha.

Hukumu hiyo sasa inaruhusu mashoga kufanya mapenzi kwa faragha.

Kanuni ya 377 ilipitishwa na wakoloni wa Kiingereza miaka 157 iliyopita na kutia hatiani matendo yote ya ulawiti, mapenzi ya jinsia moja na kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo.

Vuguvugu la kuiondoa kanuni hiyo lilianza mwaka 2001 na mwaka 2009 suala hilo lilitua mahakamani jijini Delhi ambapo mahakama kuu ya jiji hilo iliamua kuifuta kanuni hiyo.

Hatahivyo makundi ya kihafidhina, na kidini yakidini yaliweka msukumo kwa kurudishwa kwa sheria ya kuharamisha ngono ya watu wa jinsia moja na mwaka 2013 mahakama ya upeo ikarudisha kanuni 377.

Hatua hiyo haikuwavunja moyo wanaharakati wa haki za mashoga ambapo waliiomba mahakama ya upeo kupitia upya maamuzi yake wakisema hyakuwa ya haki. Mwaka 2016 mahakama hiyo ilikubali ombi hilo na leo maamuzi ya mwisho yameamuliwa.

Mwanaharakati Harish Iyer ameiambia BBC kuwa: "Nina furaha isiyokifani. Ni kama tumeshinda mapambano ya pili ya ukombozi na hatimaye tumeiondosha sheria ya Mwingereza nchini mwetu…"