Ubaguzi: Kenya yamtimua Mchina aliyemtukana rais Uhuru Kenyatta na raia

Mchina huyo amesema Kenya inanuka na yupo hapo kutengeneza pesa tu

Chanzo cha picha, You Tube

Maelezo ya picha,

Mchina huyo amesema Kenya inanuka na yupo hapo kutengeneza pesa tu

Kenya imemkamata na kumrudisha kwao mfanyabiashara mmoja raia wa China, baada ya mkanda wa video kusambaa katika mitandao ya kijamii, ukimuonesha akitoa matamshi ya ubaguzi wa rangi.

Liu Jiaqi, alirekodiwa wakati alipokua akizozana na mmoja wa wafanyakazi wake raia wa Kenya, na akamtukana Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Wakenya wote kwa kuwaita nyani, masikini na wajinga.

Polisi ilimtia nguvuni mfanyabiashara huyo siku ya Jumatano baada ya kusambaa kwa video hiyo mitandaoni. Video hiyo ilipokewa kwa ghadhabu na Wakenya wengi.

Bw Liu ni muuza pikipiki na ameonekana kwenye video hiyo akimwambia mfanyakazi wake kuwa naichukia Kenya kwa sababu "inanuka."

Mfanyakazi huyo alipomuuliza kwanini yupo Kenya akajibu kuwa yupo hapo kwa kutafuta pesa tu.

Video hiyo ilirekodiwa kwa usiri na mfanyakazi huyo ambaye alikuwa akitishiwa kufutwa kazi.

Bw Liu na washirika wake hawajazungumzia chochote kuhusu video hiyo ambayo ubalozi wa Uchina jijini Nairobi unasema ilirekodiwa mwezi Juni mwaka huu.

Msemaji wa ubalozi huo Bw Zhang Gang ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Bw Liu tayari ameshaadhibiwa na kampuni yake na amemwomba radhi aliyemtolea matamshi hayo.

"Mazungumzo na hisia binafsi za za kijana huyu haziakisi mawazo ya watu wa Uchina kwa ujumla wao," amesema Gang.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Wafanyakazi wa raia wa Kenya katika mradi wa reli ya kisasa SGR waliripoti kwa wingi vitendo vya kibaguzi kutoka kwa Wachina.

Japo hii ni mara ya kwanza kwa mtu kufurushwa kwa ubaguzi, kumweripotiwa visa vingi vya ubaguzi kutoka kwa raia wa Uchina wakati wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Mombasa mpaka Nairobi.

Mwaka 2015, kuliripotiwa kisa cha kukataliwa Wakenya kuingia kwenye mgahawa mmoja wa Kichina jijini Nairobi ifikapo usiku. Mmiliki wa mgahawa huo alipandishwa kizimbani kwa kosa la kutokuwa na leseni ya kuuza pombe na si ubaguzi.