Sakata ya makontena: Je serikali ya Tanzania inampendelea Paul Makonda?

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania
Magufuli
Maelezo ya picha,

Rais John Pombe Magufuli

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli anasifika kwa kuchukua maamuzi magumu, kukemea, kufuatilia na kuwaondoa viongozi wasiomridhisha kiutendaji au namna yoyote ile katika serikali tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.

Wapo viongozi wengi waliokumbana na makali ya Magufuli. Kuanzia mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na wakurugenzi.

Lakini, hali hiyo ni tofauti inapokuja kwenye utendaji wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda.

Makonda anakabiliwa na kibarua kigumu kujisafisha na sakata la kutaka kutoa makontena bandarini bila kulipa kodi.

Makontena hayo 20 yenye jina lake yanatajwa kuwa yamebeba vifaa vya walimu vilivyochangiwa na Watanzania wanaoishi nchini Marekani.

Makonda aliomba msamaha wa kodi kwa makontena hayo na kukataliwa na Waziri wa Fedha wa Tanzania Dk. Philip Mpango ambaye kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo ndiyo mwenye mamalaka ya kuamua nani ama nini kipatiwe msamaha wa kodi.

Mwezi Machi mwaka huu, Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitangaza kusudio la kupiga mnada makontena hayo kutokana na kutotolewa bandarini kama sheria inavyoagiza.

Tangazo hilo likazaa mjadala na malumbano baina ya viongozi hao wawili ambao wote ni wateule wa Magufuli.

Wengi walitarajia kuwa Rais angezungumzia jambo hilo kwa kina au angechukua hatua kali ya kumwondoa mmojawapo.

Hatahivyo ilichukua muda kidogo hadi pale Rais alipotoa kauli yake Agosti 24 akiwa katika mkutano na madiwani wa wilaya ya Chato mkoani Geita.

Maelezo ya video,

Rais Magufuli azungumza kuhusu sakata ya makontena

Magufuli alimtaka Makonda kulipa kodi, na kumkingia kifua Mpango akisema ndiye mwenye mamlaka juu ya suala hilo kwa mujibu wa sheria.

Kwa jinsi Magufuli anavyofahamika kwa kuwaondoa viongozi wote wanaokwenda kinyume cha taratibu ama kutomridhisha, wengi walitarajia rungu lake lingemshukia Makonda, la hasha!

Kutochukuliwa hatua kwa Makonda kunaamsha mjadala wenye swali moja kuu, je, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam anapendelewa na mkuu huyo wa nchi?

Itakumbukwa Aprili 2016 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango-Malecela aliondolewa madarakani siku 26 pekee toka kuanza kazi hiyo.

Mama Malecela ambaye ni mke wa Waziri Mkuu wa zamani John Malecela aliadhibiwa baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake haukuwa na watumishi hewa. Uchunguzi wa Ikulu baadae ulionesha kuwa walikuwepo, 45.

Mawaziri walivyotoswa

Chanzo cha picha, Nchemba/Facebook

Mwezi Mei 2016, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga alifutwa kazi kwa tuhuma za kuingia Bungeni akiwa amelewa.

Mawaziri wawili Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) George Simbachawene (Ofisi ya Rais) walifutwa kazi kufuatia sakata la mchanga wa madini (makinikia) wa kampuni ya Acacia.

Mwigulu Nchemba ni waziri aliyeondolewa hivi karibuni katika wizara ya Mambo ya Ndani, ambapo kauli za Rais Magufuli zinaonyesha kutoridhishwa na utendaji wake.

Julai mosi mwaka huu Mwigulu Nchemba alitolewa kwenye nafasi ya uwaziri wa Mambo ya Ndani. Rais Magufuli alitaja sababu 13 kumwondoa Mwigulu ikiwemo ajali za barabarani

na matumizi mabaya ya fedha za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.

Ni Upendeleo?

Aliyekuwa waziri wa Habari Nape Nnauye pia alikutana na rungu la Rais Magufuli. Lakini kuna ushiriki wa Makonda katika kuondoka kwa Nape.

Mwezi Machi 2017 Makonda alivamia Kituo cha Televisheni cha Clouds akiwa na askari wenye silaha akitaka kipindi anachotaka yeye kirushwe hewani.

Nape akiwa kama waziri mwenye dhamana, akaitisha uchunguzi huru wa tukio hilo. Ripoti ya uchunguzi huo ilimtia lawani Makonda.

Nape aliahidi kuifikisha ripoti hiyo kwa Rais, lakini hatimaye alifutwa kazi, na badala yake Magufuli, mbele ya hadhara akamsihi Makonda " piga kazi" na kusema yeye Rais hapangiwi nini cha kufanya.

Hapo ndipo chimbuko la hoja ya Makonda kupendelewa ilipozaliwa, na hili la kutoadhibiwa kwa kufanya jaribio la kukwepa kodi kinyume cha sheria za nchi ni muendelezo tu.

Iwapo Rais Magufuli alichukua hatua kali dhidi ya Mwigulu Nchemba, Profesa Muhongo, Anne Kilango-Malecela, George Simbachawene, Mwigulu Nchemba na Nape Nnauye, ni kwanini imekuwa vigumu dhidi ya Paul Makonda?

Kwamba iwapo Paul Makonda ametazamwa upande chanya, je wengine walioondolewa madarakani hawakuwa na uwezo wowote wa kutimiza wajibu wao kama wangetazamwa kwa upande chanya?

Tafsiri yangu

Kwa jicho la kisiasa naweza kutafsiri hatua iliyopo hadi sasa (kama hataondolewa siku zijazo) kwamba Rais ameonyesha upendeleo kwa kiasi fulani dhidi ya wateule wake, huku baadhi wakionekana wenye 'damu ya kunguni' yaani hawapendwi.

Kusema hivi sio kumchukia Makonda bali kusisitiza utawala wa sheria nchini pamoja na kudumisha utamaduni wa kujiuzulu ambao ungeliweza kufanywa na Makonda ili kuonyesha uwajibikaji pamoja na kumsaidia Rais Magufuli kwa njia hiyo.

Aidha, suala hili linaweza kuongeza ufa, kwa kuwa baadhi ya wateule wameshaondolewa kwa makosa ya wazi lakini mwingine hajaondolewa.

Mshikamano katika serikali pia utakuwa hafifu, huku wengi wa watendaji wanaweza kumtazama Makonda kwa jicho la chuki na kumnyima mshikamano wa kiutendaji. Litakuwa jambo gumu kushikamana katika mazingira ambayo baadhi ya wateule wanafanya makosa ya wazi huku wakitetewa, lakini wengine wakitimuliwa mamlakani.

Muda utaongea.