Makontena yenye sakata yakosa mnunuzi kwa mara ya tatu katika mnada Tanzania

Makontena bandarini

Jaribio la tatu la kupiga mnada makontena 20 yalioingizwa nchini Tanzania na kamishna wa jimbo la Dar es Salaam Paal Makonda yamekosa mnunuzi siku ya Jumamosi.

Hatua hiyo inajiri baada ya waliohudhuria mnada huo kushindwa kuafikia bei iliowekwa.

Kulingana na gazeti la the Citizen nchini Tanzania, mnada huo ulifanyika katika eneo la ndani la kuweka makasha ICD chini ya usimamizi wa wakala Yono Auction Mart ambaye amepewa kandarasi na mamlaka ya ushuru nchini Tanzania TRA kuchukua jukumu hilo.

Baadhi ya bidhaa zilizopatikana katika makasha hayo ni pamoja na samani za afisini kama vile viti, meza na kabati.

Kulingana na ripoti iliowekwa wazi kwa umma na Makonda, bidhaa hizo ziliagizwa na marafikize kutoka nchini Marekani ili kukabidhiwa shule za mjini Dar es Salaam.

Ripoti kutoka eneo la mnada huo zinasema kuwa waliotaka kununua vitu hiyo walitoa kati ya sh.15 milioni na sh.30 milioni fedha zilizokuwa chini ya bei iliotolewa ya Sh60 million.

Mmoja ya wanunuzi hao amesema kuwa bei ya vitu hivyo ni ghali mno.

Maswali mengi pia yaliibuka juu ya mzigo huo wa samani baada ya kusambaa mtandaoni kwa barua iliyokuwa ikionesha Paul Makonda kuomba msamaha wa kodi ambao halikuridhiwa mpaka sasa.

Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

"Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.

Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo" amesisitiza Rais Magufuli.

BBC imefanya mazungumzo na mtaalamu wa masuala ya siasa Goodluck Ng'ingo, ambae anasema kila kitu ambacho kinachozua mjadala sheria yake ipo wazi.

"Waziri Mpango anasimamia sheria na kanuni na Mkuu wa Mkoa anaonekana kuweka siasa."

Kwa mujibu wa sheria ya Bodi ya Afrika Mashariki,

Mtu anaweza kusimama kama taasisi au kusimama kama mtu binafsi katika kusafirisha mzigo ukiwa unaonesha ni wa nani na umetokea wapi?

Mchambuzi huyo pia ameendelea kusema kuwa asasi za kiraia na taasisi za dini peke yake ndio zina msamaha wa kodi tena kwenye bidhaa ambazo zinahusu afya na elimu lakini vilevile msamaha huo upo kwenye bidhaa ambazo hazizalishwi nchini.

Kisheria hakuna msamaha kwa mtu mmoja na kwa vitu vinavyotengenezwa ndani ya nchi, ameongeza kusema Goodluck.