Je kwa nini Kenya iko njia panda kiuchumi?

  • Hezron Mogambi
  • Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
Maelezo ya picha,

Rais Uhuru Kenyatta na Rais wa China Xi Jinping

Ni bayana sasa kwamba Kenya inajikuta katika hali ya kung'ang'aniwa na mvutano wa kibiashara na kiuchumi kati ya baadhi ya nchi tajiri za magharibi na mataifa yanayochipuka kiuchumi kama vile Uchina.

Katika siku za hivi karibuni, viongozi wa nchi za Marekani na Uingereza wameonekana kuwa makini katika kuboresha uhusiano wao na Kenya, katika kuchukuwa tahadhari kuhusu uuiano mwema wa kiuchumi wa muda mrefu kati ya Nairobi na Beijing.

Katika kile kinachoonekana kama juhudi za Marekani na Uingereza kuuongeza ufadhili wake na uhusiano wa miradi mbali mbali ya kibiashara na viwanda, rais Uhuru Kenyatta amejikuta katika mfulilizo wa ziara kuelekea mataifa hayo, jambo ambalo linadhihirisha na kuonyesha jinsi nchi hizi zinavyoidhamini Kenya katika ukanda huu na Afrika kwa jumla.

Majuma mawili yaliyopita, rais Uhuru Kenyatta alifanya ziara mjini Washington DC na kujadiliana na mwenyeji wake Donald Trump, katika kile kilichoonekana kama juhudi za Marekani kujaribu kutafuta ushawishi zaidi nchini Kenya kupitia kwa miradi mbalimbali na bishara.

Ziara hii ilimfanya Rais Uhuru Kenyatta kiongozi wa pili kutoka bara la Afrika kukaribishwa Marekani na kiongozi wa taifa lenye uwezo mkubwa duniani.

Kiongozi wa Nigeria Muhammadu Buhari ndiye aliyekuwa wa kwanza kukaribishwa ikulu ya White House. Mbali na mazungmzo na Trump, Kenyatta alikutana na viongozi wa kampuni mbalimbali za Marekani chini ya mwavuli wa Business Council for International Understanding.

Mkutano huo ulilenga kuzungumzia kushiriki kwa kampuni za Marekani katika ajenda kuu nne za maendeleo za Rais Kenyatta kama inavyoelezwa katika makubaliano yaliyotiwa saini mwezi Juni mwaka huu.

Maelezo ya picha,

Ujenzi wa reli ya kisasa uliofadhiliwa na China Kenya

Itakumbukwa kuwa Kenya ni mshirika wa karibu wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi na usalama wa kanda, jambo ambalo lilikuwa mojawapo wa masuala makuu katika mkutano wa marais hao mjini Washington DC.

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa ziara hiyo ya Marekani ilifanywa katika wakati ambao Rais Uhuru Kenyatta anatafuta uungwaji mkono wa kifedha ili kuzitekeleza ajenda zake nne kuu na hivyo kuwashawishi wawekezaji kutoka Marekani.

Ajenda hizo kuu ambazo kiongozi wa Kenya ametilia maanani ni pamoja na kuimarisha sekta ya viwanda, afya, makaazi kwa bei nafuu na chakula.

Ingawa tayari Hazina ya kitaifa ya matibabu nchini Kenya (National Hospital Insurance Fund) imeshaanza kutekeleza afya kwa umma, fedha kwa ajenda hizo nyingine bado ni changamoto kwa serikali.

Madeni ambayo serikali inahitajika kulipa yamekuwa mengi na pesa za kulipia madeni hayo zinaendelea kupungua.

Ni kutokana na sababu hii ndio Kenya inaripotiwa kugeukia serikali ya Uchina kufadhili nusu ya gharama ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Mkutano wa Beijing Ijuma iliyopita ulifanyika miezi miwili kabla ya Shirika la ndege la Kenya Airways kuanza safari za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York.

Tayari kampuni ya KQ imeanza kuuza tiketi za safari hiyo ya kihistoria, ambapo wasafiri watahitajika kulipa Sh89, 000 kwenda na kurudi.

Baada ya kurudi kutoka Marekani, Rais Kenyatta alimkaribisha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May katika Ikulu ya Nairobi, hii ikiwa ziara yake ya kwanza barani Afrika baada ya kuchukuwa hatamu za uongozi. Waziri mkuu May pia alizuru Afrika Kusini na Nigeria

Maelezo ya picha,

Rais Kenyatta alipokutana na Rais Trump Ikulu Marekani

Katika mazungumzo ya Waziri Mkuu May na Rais Kenyatta, makubaliano yalitiwa baina ya nchi hizi mbili ambayo yatawezesha mali ya ufisadi yaliyofichwa nchini Uingereza, pamoja na milioni 470 ambazo ziltwaliwa na mahakama za Uingereza, kurudishwa nchini Kenya.

Waziri Mkuu wa Uingereza pia alisemna katika mkutano huo na Kenyatta kuwa nchi yake itaendelea kuisadia Kenya na majeshi yake yaliyoko nchini Somalia katika kupigana dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Aidha, aliahidi kutangaza mpango mpya wa kufadhili muungnao wa wanajeshi wa bara la walioko nchini Somalia (AMISOM).

Viongozi hawo wawili pia walijadiliana jinsi nchi ya Kenya na bidhaa zake zinaweza kupata masoko zaidi nchini Uingereza wakati London itakapokuwa imejiondoa kutoka umoja wa ulaya mnamo Machi 2019.

Baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Rais Kenyatta alipanda ndege na kuelekea Uchina kuhudhuria mkutano wa ushirikiano kati wa Uchina na mataifa ya Africa maarufu kama FOCAC.

Ni dhahiri kuwa Uchina ilikuwa imepigwa butwaa wakati Uhuru Kenyatta alipokubali mwaliko wa Rais Trump, muda mfupi tu kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa Beijing ambao ulikuwa umepangwa kwa miezi kadhaa iliyotangulia.

Kutokana na tukio hilo, Rais Kenyatta atapata kwamba maafisa wakuu wa serikali ya Uchina watakuwa wanazichunguza hatua zake za baadaye na uhusiano wake na Marekani.

Aidha, ilibainika kuwa akiwa Uchina, Kenyatta alikutana kwenye mazumngmzo na Rais wa China Xi Jinping.

Maelezo ya picha,

Kenya hutegemea sana kilimo hasa cha Chai

Kile ambacho kimekuwa kikijitokeza ni kuwa Uchina ilikuwa imezipiku nchi za Marekani na nchi nyingine za magharibi kama taifa muhimu katika biashara na nchi za bara la Afrika.

Hii ndio sababu Rais wa Uchina Xi Jinping alitoa msaada wa $60 bilioni kwa bara la Afrika pamoja na kufutilia baadhi ya madeni kwa nchi maskini za Afrika.

Hata hivyo, pamoja na safari hizi na kung'ang'aniwa kwa Kenya na nchi za Marekani, Uingereza na Uchina, swali ambalo limekuwa likiibuka miaka ya hivi karibuni ni iwapo Kenya itaweza kujimudu kulipa madeni ambayo yamekuwa yakijilimbikiza. Cha kutisha zaidi ni kuwa nchi ya Kenya imekuwa ikikopa ili kulipa madeni ya zamani.

Mifano ni muhimu. Mwaka wa 2014, Kenya ilipewa mkopo kutoka masoko ya madeni ya kimataifa kupitia kile kilichoitwa Eurobond.

Lengo la mkopo huo lilikuwa kulipia mkopo mwingine wa milioni $600 ambao ulichukuliwa mwaka wa 2012. Aidha, sehemu ya mkopo wa mwaka wa 2014 ilikuwa na nia ya kufadhili maendeleo katika miundo msingi na kusaidia bajeti ya kuendesha serikali.

Rais Uhuru Kenyatta alisema mafanikio ya mkopo huo ilikuwa ishara kuwa wawekezaji wa kimataifa wana imani na uchumi wa Kenya.

Mkopo wa Eurobond mnamo 2016, uliibua mjadala mkali kuhusiana na matumizi yake huku kiongozi wa upinzani wakati huo,Raila Odinga, akidai kuwa fedha hizo ziliibwa na baadhi ya maafisa wakuu serikalini.

Maelezo ya picha,

Maandamano ya kupinga wizi wa fedha za umma Kenya

Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya Kenya kupitia waziri wa fedha ilitangaza kuwa imefanikiwa kupata mkopo mpya wa Sh203 bilioni wa Eurobond ambao utatumiwa katika miradi ya ujenzi wa miundomsingi na kulipia madeni mengineyo.

Kama ilivyokuwa mwaka wa 2014, mkopo wa mwaka huu wa $2 billion umepangiwa kulipia deni la mkopo wa $750 million ambao ulichukuliwa na serikali mwaka wa 2016 kwa minajili ya maendeleo ya miundo msingi na bajeti ya Kenya.

Huku haya yakijiri, wakopaji wa kimataifa kupitia kwa shirika la Moody's sovereign ratings waliishusha nchi ya Kenya katika masuala ya ukopaji.

Sababu zilizotolewa kwa hatua hiyo ni pamoja na hali ya kiuchimi isiyoonyesha matumaini kutokana na kulimbikizwa kwa madeni, kutegemea sana madeni ya kibishara na mahitaji ya kifedha mengi katika uchumi wa Kenya kutokana na miradi.

Hali hii ambayo inaonyesha ishara ya Kenya kutoweza kuyalipa madeni ni suala linalotatiza na kuzua changamoto kwa serikali na wananchi kwa jumla. Tayari hatua ya kuongezeka kwa bei ya mafuta ya petroli, ambayo inafungamanishwa na haja ya kulipa madeni kwa Kenya inazua changamoto kwa wanabishara, wananchi wa kawaida na uchumi wa Kenya.

Maelezo ya picha,

Asilimia kubwa ya watu nchini wanaishi chini nya dola moja kwa simu

Katika miaka ya hivi karibuni, jumla ya madeni ya serikali ya Kenya imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kikubwa kufikia kiwango cha $40.4 bilioni mwaka uliopita ikilinganishwa na $37.6 bilioni mwaka wa 2016.

Hii ndiyo sababu iliyomfanya rais Uhuru Kenyatta na ujumbe wake kupendekeza mfumo wa kuhusisha mashirika ya kibinafsi na umma yaani Public Private Partnership (PPP) katika kufadhili miradi ya miundo msingi.

Ni kupitia kwa mfumo huu ndipo mpango wa ujenzi wa barabara ya kilomita 30 kati ya uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na Westlands jinini Nairobi ulifikiwa na wafadhili wengine katika ziara ya nchini Uchina hivi majuzi.

Kenya sasa inatumia thuluthi moja ya mapato yake kulipia madeni, jambo linalofanya ufadhili wa shughuli za maendeleo kuwa vigumu.

Aidha, hali kama hii inatisha hadhi ya Kenya katika kukopa miaka ya baadaye, kutatiza juhudi za kuweza kukopa hali ya dharura ikijitokeza pamoja na hali ya kiuchumi na maisha kwa jumla.

Prof. Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi @ yahoo.co.uk