Rais wa Moldova Igor Dodon apata ajali mbaya ya barabarani

Moldova President Igor Dodon

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Rais wa Moldova Igor Dodon

Rais wa Moldova Igor Dodon amejeruhiwa kwenye ajali mbaya ya barabarani kaskazini magharibi mwa mji mkuu Chisinau.

Vyombo vya habara vinasema ajali hiyo ilitokea wakati lori lililokuwa likitoka upande wa mbele lilipita gari lingine na kugonga msafara wa rais karibu na mji wa Straseni.

Moja ya magari kwenye msafara wa rais lilipinduka. Rais Dodon alipelekwa hospitalini.

Anaripotiwa kupata majeraha madogo lakini ripoti zinasema kuwa mama yake yuko hali mbaya.

Rais huyo mwenye miaka 43 ameliongoza taifa hilo lililokuwa la Usovieti tangu Disemba mwaka 2016.

Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijami zilionyesha gari lililokuwa limepinduka likiwa kando ya barabara.

Ajali hiyo inatokea saa kadhaa baada ya Genady Gagulia, waziri mkuu wa Abkhazia, Jamhuri inayoungwa mkono na Urusi iliyojitenga kutoka Georgia miaka ya tisini kufa kwenye ajali ya barabarani.