Urusi yazindua zoezi kubwa la kijeshi kuwahi kufanyika tangu enzi ya vita baridi

Gari la vitaT-80 likirusha makombora, Agost 23 mwaka 2017 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Urusi ikiimarisha zoezi la kivita kwa vikosi vyake vyake vya ulizi - licha ya gharama

Urusi leo imeanza mazoezi makubwa ya kijeshi, mashariki mwa Siberia yanayotajwa kuwa ni makubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya taifa hilo.

Katika mazoezi hayo vikosi hivyo vya kijeshi vitaonyesha michezo ya kivita ,ambapo wanajeshi laki tatu watashiriki pamoja na magari ya kijeshi 36,000 na meli 8 za kivita.

Uchina itatuma wanajeshi elfu tatu mia mbili ambao watashiriki katika zoezi maalumu linalofahamika kama "Vostok-2018".

Mongolia pia inatarajiwa kutuma baadhi ya vitengo vya jeshi lake katika zoezi hilo.

Mara ya mwisho Urusi ilifanya zoezi kbwa kama hili ilikuwa mwaka 1981, wakati wa vita baridi lakini zoezi la mwaka huu linahusisha vikosi vingi vya kijeshi.

Zoezi hilo ambalo litaendelea kwa wiki moja linakuja wakati kumekuwa na ongezeko la mvutano kati ya Urusi na vikosi vya muungano wa kujihami kwa mataifa ya magharibu NATO.

Kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, rais wa Urusi, Vladimir Putin,amekutana na mwenzake wa Uchina Xi Jinping, katika kongamano lilillofanyika katika mji wa mashariki wa Vladivostok, ambapo alielezea kuimarika kwa uhusiano kati ya mataifa hayo hasa katika masuala ya siasa usalama na ulinzi.

Uhusiano kati ya Urusi umedorora tangu Urusi iliponyakua jimbo la Crimea kutoka nchini Ukraine mwaka 2014. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, amesema zoezi hilo ni muhimu hasa ikizingatiwa uhasama unaoelekezwa kwa Urusi.

Nini kitafanyika katika zoezi hilo?

Siku ya Juma nne na Jumatano itakuwa ya maandalizi huku zoezi lenye likitarajiwa kuanza siku ya Alhamisi na kuendelea kwa siku tano.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema zoezi hilo litaendeshwa katika vituo vitano ya mafunzo ya kijeshi,ardhini,angani na majini. Wizara hiyo pia imethibitisha kuwa zoezi hilo halitafanyika karibu na kisiwa cha Kuril kinachozozaniwa kaskazini mwa Japan.

Kwa mujibu wa kitengo cha habari cha wizara ya Ulinzi ya Urusi vikosi vitatu vya wanajeshi wa angani vya nchi hiyo vitaendelea na jukumu muhimu la kutoa ulinzi karibu na mipaka ya Uchina na Mongolia.

Image caption Ramani ya Urusi na jirani yake Mongolia.

Kwa nini Uchina inahusika katika zoezi hili?

Wizara ya ulizi ya Uchina imezungumzia kuimarika kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya mataifa hayo mawili.

Imesema ushirikiano huo utaboresha uwezo wa pande zote mbili kukabiliana na tishio lolote la kiusalama.

Ijapokuwa Uchina haikubainisha ni tishio la aina gani,wiziri wa wa ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu amesema makundi ya itikadi kali yaliyo na makao yao maeneo ya kati barani Asia ni tishio kubwa kwa usalama wa nchi hiyo

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wanajeshi wa Uchina na Urusi wakifanya mazoezi ya pamoja mashariki mwa Urusi mwaka uliyopita

Uchina imewekaulinzi mkali katika eneo la Xinjiang linalokaliwa na waumini wengi wa dini ya kiislamu.

Eneo hilo limekumbwa na ghasia za mara kwa mara kufuatia msako ambao umedumu kwa miaka kadhaa sasa.

Uchina inawalaumu wanamgambo wa makundi yanayotaka kujitenga kwa kusababusha ghasia hizo.

Hali hiyo inalinganishwa na miaka ya vita baradi wakati USSR na China zilikuwa ziking'an'gania uongozi wa kimataifa wa kikomunisti na hatimaye wakaishia kukabiliana katikana mpaka wa mashariki

Kauli ya shirika la Nato ni ipi ?

Msemaji wake Dylan White, amesema Nato imearifiwa kuhusiana na na zoezi la Vostok-2018 mwezi Mei na kwamba itafuatilia.

Amesema "Mataifa yote yana haki ya ya kufanyisha mazoezi vikosi vyao,lakini cha msingi ni kuhakikisha zoezi lenyenyewe linafanywa kwa njia ya uwazi''

Kwanini uhasama kati ya Urusi na Nato umeongezeika?

Uhasama kati ya shirika la kujihami la Nato umeongezeka baada ya Urusi kuvamia kijeshi Ukraine mwaka 2014, kwa kuunga mkono wanamgambo waliyotaka kujitenga kwa jimbo la Cremea.

Nato ilijibu uvamizi huo kwa kupeleka vikosi zaidi mashariki mwa Ulaya na kutuma wanajeshi 4,000 katika eneo la Baltic.

Urusi inasema Nato haikustahili kuchukua hatua hiyo ya uchokozi. Inasema mabadiliko makubwa yaliyoshuhudiwa nchini Ukraine kati ya mwaka 2013 na 2014 yalikuwa mapinduzi yaliyopangwa na mataifa ya magharibi

Hatua ya hivi karibuni ya Nato dhidi ya Urusi ni ile ya wanadiplomasia wa Urusi kufurushwa kutola mataifa wanachama wa muungano wa Nato kufuatia sakata ya shambulizi la sumu ya neva, dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi nchini Uingereza, Sergei Skripal na binti yake, Yulia, w kusini mwa England mwezi machi.

Uingereza inailaumu Urusi kwa kuhusika na shambulizi hilo,madai ambayo Moscow imekanusha.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii