Mpaka wa Ethiopia na Eritrea wafunguliwa baada ya miaka 20

Viongozi wa Eritrea na Ethiopia Haki miliki ya picha Serikali ya Ethiopia
Image caption Rais wa Isaias Afwerki kushoto na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed walaikutana kabla ya ufunguzi wa mpaka

Viongozi wa mataifa ya Ethiopia na Eritrea wameshuhudia kufunguliwa kwa mpaka huo muhimu ambao ulikuwa umefungwa kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita kufuatia mzozo wa mpakani.

Hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, hali ambayo itaiwezesha Ethiopia kutumia bandari ya Assab.

Kituo kingine cha mpakani kilichopo karibu na mji wa Zalambessa nchini Ethiopia pia kinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Mkataba wa amani uliyotiwa saini na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki mwezi Julai umechangia kufufua uhausiano wa kidiplomasia na wa kibiashara.

Kufunguliwa kwa mpaka huo kunajiri wakati Ethiopia inasherehekea mwaka mpya.

Mapigano yaliyozuka katika eneo hilo la mpakani mnamo mwezi Mei mwaka 1998, yalisababisha vifo vya maelfu ya watu.

Vita hivyo vilimalizika mwaka 2000 baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani wa Algiers.

Hata hivyo mkataba huo haukutekelezwa kikamilifu baada ya Ethiopia kukataa kutekeleza uamuzi wa tume iliyobuniwa ya kusuluhisha mzozo huo wa mpakani

Kufunguliwa kwa mpaka huo kuna umuhimu gani?

Familia zilizotenganishwa na mapigano kati ya mataifa hayo mawili sasa zitaweza kuungana tena baada ya kutengana kwa zaidi ya miongo miwili.

Eritrea ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Ethiopia mwaka 1991 lakini jamaa za familia moja ziliendelea kuishi pande zote mbili za mpaka kati ya mataifa hayo mawili huku zikijivunia uhusiano mwema kati yao hadi mwaka 1998.

Yonas Fesseha, mkaazi wa Zalambessa ameiambia idhaa ya BBC Tigrinya kwamba anajiandaa kukutana tena kwa mara ya kwanza na mama yake pamoja na ndugu yake katika kipindi cha miaka ishirini.

Anasema watu katika mji huo wamejawa na furaha

Image caption watu walijitokeza kwa mavazi tofauti tofauti kusherehekea

Eneo la Zalambessa lipo katika ushoroba wa kaskazini unaounganisha mji mkuu wa Ethiopia na eneo la kaskazini la Tigray ambalo pia linaunganisha mji mkuu wa Eritrea, Asmara.

Kufungwa kwa ushoroba huo kuliathiri vibaya biashara katika eneo hilo huku uchumi wa baadhi ya mataifa katika kanda hiyo ukiathiriwa .

Ni kipikingine kilichobadilika kati ya mataifa haya?

Kufunguliwa kwa mpaka kati ya mataifa haya ni msururu wa mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa hususan kuhusu uhusiano kati ya Ethiopia na Eritrea.

Tangu viongozi wa mataifa hayo kutia saini mkataba wa amani mwezi Julai, huduma za mawasiliano na usafiri zimerejelewa, hatua ya hivi punde ikiwa ile ya wiki moja iliyopita ambapo meli ya Ethiopia ilitia nanga katika bandari ya Eritrea.

Mataifa hayo mawili pia yamefungua balozi zao katika miji mikuu ya pande zote mbili.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Barabara inayopitia mpakani katika eneo la Zambalessa imefungwa kwa zaidi ya miongo miwili

Nini kitakachofanyika katika kivuko cha mipaka mingine?

Kwa sasa ni mpaka wa ardhini pekee katika maeneo Zalambessa na Burre ambao utafunguliwa. Maelezo kuhusu maeneo mengine yatatolewa baadaye .

Mji wa Badme, ambao ulizozaniwa na mataifa hayo kati ya mwaka 1998-2000, uliamuliwa kuwa sehemu ya Eritrea na tume iliyobuniwa baada ya makubaliano ya amani ya Algiers.

Hadi hivi karibuni mji huo umekuwa chini ya himaya ya Ethiopia, Lakini hali hiyo imebadilika baada ya viongozi wa mataifa hayo kukutana japo Eritrea haijapewa rasmi umiliki wake.

Image caption Kuna matumaini kwamba hatua hiyo itabadilisha mengi katika kanda hiyo

Hali ilikuwa vipi mjini Zalambessa wakati wa vita?

Mji huo wa mpakani ulikuwa moja ya ngome kuu ya mapigano.

Katika kipindi cha miaka miwili ya mapigano, mji wa Zalambessa ulikuwa chini ya usimamizi wa vikosi vya Eritrea na wakati wa mapigano hayo sehemu kubwa ya mji huo iliharibiwa.

Eritrea haikuwahi kulalamika kwamba mji huo ni sehemu ya Ethiopia na kwamba umiliki wake ndio chanzo cha mgogoro kati ya mataifa hayo mawili.

Ni mabadiliko gani yameshuhudiwa katika kanda hiyo?

Uhasama kati ya Ethiopia na Eritrea uliathiri kanda nzima ya upembe wa Afrika huku mataifa hayo yakichukua misimamo kinzani kwa kila jambo.

Mataifa hayo yalichukuwa misimamo tofauti katika mzozo wa Somalia - Eritrea ikilaumiwa kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi nayo Ethiopia, ambayo ni mshirika wa Marekani ikiunga mkono serikali inayotambuliwa na jamii ya kimataifa.

Hali hiyo kwa sasa imebadilika kufuatia hatua ya wiki iliyopita ya mataifa ya Ethiopia, Eritrea na Somalia kutia saini mkataba wa ushirikiano utakaorejesha amani na ustawi katika kanda hiyo.

Eritrea na Djibouti pia zimekubaliana kuimarisha uhusiano wao baada ya mzozo wa mpakani kati yao kutishia vita kati yao.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii