Msaada: Jamii yatakiwa kuacha unyanyapaa kwa watu wanaojaribu kujitoa uhai

kujitoa uhai Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Wataalamu wa afya wanasema kujitoa uhai ni ugonjwa na siyo hatia.

Shirika la Afya Duniani (WHO) sasa linaonya kwamba kujitoa uhai ni changamoto ya dunia.

Kukabiliana na changamoto hiyo, jamii zinaombwa kushirikiana pamoja na kuzuia watu wengi kujiua. Takwimu zinaonyesha kwamba vifo vingi miongoni mwa vijana kati ya umri wa miaka 15- 29 vinasababishwa na kujitoa uhai.

Sababu kuu ya watu kujitoa uhai imetajwa kama matatizo ya kiakili, kumpoteza mpendwa au kupata hasara ya aina moja au nyingine.

Wataalamu wa afya wanasema kujitoa uhai ni ugonjwa na siyo hatia. Hii ni kwa sababu katika baadhi ya mataifa ya Afrika kujitoa uhai ni hatia kisheria. Hali hii pamoja na unyanyapaa unaowaandama wanaojaribu kujitoa uhai imewafanya wengi ambao ni wagonjwa kutotafuta matibabu.

Roselyne Omondi kutoka Kenya ameambia BBC kwamba alijaribu kujiua mara nne. ''Nilikunywa dawa nyingi kwa mpigo nikitaka kulala milele kwenye mauti. Nilihisi kwamba nilikuwa mzigo kwa wazazi na wanangu ambao walikuwa wadogo.Nilikata tamaa ya maisha.Licha ya kuponea kifo mara ya kwanza, nilijaribu tena kujiua mara tatu.Mara ya mwisho nilijipata katika chumba cha wagonjwa mahututi,'' wakati huu wote hakuwahi kumuambia yeyote wakiwemo wanawe ambao kwa sasa ni watu wazima.

''Niliona aibu sana, sikutaka mtu hata mmoja kujua hali yangu. Nilihofia kuhukumiwa na watu ambao wangefahamu kwamba nilijaribu kujitoa uhai''.

Jamii nyingi barani Afrika zinaendelea kuwalaani wale wanaojitoa uhai pamoja na kuzitenga familia zao. Wale wanaojaribu kujitoa uhai pia hawaepuki ghadhabu hiyo. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya akili watu wengi hawachukulii hali hiyo kama ugonjwa huku baadhi ya watu wakichukulia kama hatua ya kumkosea Mungu na kwamba ni dhambi kubwa. Wale wenye dhana hizi katika harakati ya kumtafutia matibabu muathiriwa huamua kumpeleka kwa viongozi wa kidini ili wapate kuombewa. Jamii pia huchukulia matatizo ya kiakili kama laana na jamaa ya muathiriwa hufanya kila juhudi kuficha ukweli kuhusu kile anachougua mpendwa wao.

Nini kinachangia mtu kutaka kujiua?

Haki miliki ya picha Getty Images

Wanasikololojia wamefanya utafiti na kugundua kuwa baadhi ya watu huchukulia wazo la kujitoa uhai kama kitendo cha kulipiza kisasi kwa mtu,yeye binafsi au kwa mtu mwingine. Mtu aliye na mawazo ya kujitoa uhai mara nyingi hutingwa na mawazo ya kujiona mkosaji. Kwa mfano huenda akajishutumu kwa kujisababishia maisha magumu pengine kwa kushindwa kukabiliana na changamoto zinazomkabili maishani. Kuna yule pengine anadaiwa na ameshindwa kulipa deni,hali ambayo imemfanya kushindwa kukidhi mahitaji ya familia na kutokana na hali hiyo anaishi kwa tabu.

Kwa upande wa jamii mtu mwenye mawazo ya kutaka kujitoa uhai,anahisi kuwa yeye ndiye chanzo cha masaibu yanayomkabili,kwa mfano anaona aibu kwa kushindwa kufikia malengo ya maisha,hivyo basi hapendwi na watu na wala hawamjali. Hali hizi humfanya muathiriwa kupata msongo wa mawazo na hatimaye kujihisi mpweke.

Jamii inaweza vipi kuzuia watu kujitoa uhai?

-Kufahamu dalili ambazo zinaweza kumfanya mtu akajitoa uhai.

-Kuwaonyesha upendo wale ambao wana matatizo ya akili.

-Kuhamasisha wale ambao hawajaelewa kwamba huu ni ogonjwa na siyo laana, au hatia.

-Kusitisha suala la unyanyapaa dhidi ya kujitoa uhai.

Kando na unyanyapaa unaowakabili watu wanaojaribu kujitoa uhai changamoto nyingine ni sheria kali ambayo inawafanya wagonjwa kutotafuta matibabu. Hata hivyo Bi Omondi, ambaye amejaribu kujitoa uhai mara nne,anasema alipoanza kuzungumzia wazi wazi hali yake alipata faraja baada ya kuona kwamba si yeye peke yake aliyekuwa anakumbwa na tatizo hilo. Jamii ina jukumu la kumsaidia mtu aliye na mawazo ya kujitoa uhai kwa kumpeleka kwa mshauri ambaye atamsaidia kujieleza bila kuhijihisi kwamba ataeleweka visivyo.

Nchi nyingi barani Afrika zinaharamisha jaribio la kujitoa uhai

Wataalamu wa afya sasa wanasema wakati umewadia kwa mataifa kubadilisha sera dhidi ya kujitoa uhai. Dk Catherine Mutisya,daktari wa magonjwa ya akili nchini Kenya anasema,''Kenya ukijaribu kujiua utakuwa umevunja sheria na utashitakiwa.Utapitia mchakato mzima wa sheria hadi pale hakimu au jaji atakapoamua kwamba wewe unastahili matibabu.''

Dk Catherine pia anasema watu walioshtakiwa kwa madai ya kujaribu kujitoa uhai huwapewi matibabu kama wagonjwa wa kawaida bali hupelekwa huspitali kama wafungwa wenye matatizo ya kiakili. anasema ipo haja ya kufanyia marekebisho kifungu cha sheria inayoangazia afya ya akili ili kuondoa kipengele cha uhalifu katika sheria hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchi masikini na zile zinazoendelea hususan barani Afrika ndizo zilizo na idadi kubwa ya watu wanaojitoa uhai. Nchi hizo pia zinakabiliwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo uhaba wa vifaa na watalaamu wa kushughulikia watu wanaohitaji matibabu.