Spika Job Ndugai apiga marufuku kuingia na kucha,kope bandia Bungeni Tanzania

Job Ndugai

Chanzo cha picha, BUNGE

Maelezo ya picha,

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amesema walinzi wa milango ya Bunge watakagua na kuwazui wenye kucha na kope bandia kuingia.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amepiga marufuku wabunge kuingia bungeni wakiwa na kucha na kope bandia.

Akitoa maamuzi yake Bungeni leo asubuhi, Spika Ndugai amesema ataendelea kupokea maoni kuhusu suala la wabunge kuchibua ngozi zao.

Akiongea na BBC Spika Ndugai amesema marufuku hiyo pia itawahusu raia ambao watakaokuwa wanatembelea Bunge hilo ambalo lipo jijini Dodoma.

Ndugai ametoa maamuzi hayo baada ya Mbunge wa Viti Maalaum Bi Fatma Toufiq kuiuliza serikali juu ya athari za kiafya za matumizi ya kucha na kope bandia pamoja na uchubuaji wa ngozi.

Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania Dk. Faustine Ndugulile alilieleza Bunge kuwa matumizi ya urembo huo bandia yanaathari kubwa kwa binadamu na kutaka jamii iepukane nayo.

Kwamujibu wa Ndugulile, kwa mwaka mmoja, takribani wagonjwa 700 hupokelewa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakiwa na matatizo ya ngozi yatokanayo na kijichubua.

"Waziri ameeleza kuwa hili ni tatizo kubwa...Kuongoza ni kuesha njia hivyo sisi tumewaasa wabunge wajiepushe na kucha na kope za bandia. Hivyo ni kweli tumepiga marufuku," Ndugai ameiambia BBC.

Chanzo cha picha, Getty Images

Alipoulizwa nani atakagua zoezi hilo, Ndugai amesema: "Kuna walinzi wa mageti ya bunge ambao sio tu wataangalia nyusi na kucha lakini pia tuna kanuni zetu za mavazi ambazo huwa zinaangaliwa wakati wote. Mtu ambae anakuja na mavazi ambayo hayakubaliwi kikanuni huwa hakubaliwi kuingia. Sasa katika hayo masharti ya kikanuni limeongezeka hili la kucha na nyusi bandia."

Wakati uingizwaji wa vipodozi hatarishi kwa ngozi unakatazwa nchini Tanzania, uingizwaji wa kucha na kope za kubandika unaendela kutokana na kutokuwepo kwa sheria inayokataza.