Katazo la Spika Ndugai la kucha, kope bandia bungeni lakosolewa

Kucha bandia

Uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai kukataza wanawake wenye kope na kucha bandia kuingia Bungeni umezua mjadala huku watumiaji wengi wa mitandao wakionesha kushtushwa.

Jana Jumatatu Spika Ndugai alitangaza katazo hilo bungeni na baadae kuithibitishia BBC kuwa katazo hilo linaanza kazi mara moja.

Mara tu baada ya tangazo hilo, mjadala umeibuka mitandaoni ambapo wengi wameonesha kutokuunga mkono hatua hiyo.

Mlimbwende na mwanamityindo wa kimataifa kutoka Tanzania mwenye maskani yake nchini Marekani Flaviana Matata alieleza hisia zake kupitia ukurasa wake wa Twitter. Bi Matata anaona Tanzania inachangamoto nyingi za kujadili badala ya kujadili suala hilo ambalo anaamini kuwa ni chaguo binafsi la mtu.

Bi. Matata pia ni mjasiriamali anayejihusisha na biashara ya urembo. Katika ujumbe mwengine wa Twitter amesema kuwa siku hizi kuna kope na kucha bandia ambazo huonekana kama halisi "sasa sijui watajuaje zipi ni extensions (bandia) na zipi siyo."

Mwanaharakati Carol Ndosi nae alitumia ukurasa wake wa Twitter kuonesha masikitiko yake juu ya uamuzi huo akisema: "Unajua vitu vingine tusishadadie tu sababu ni vioja. Kweli Bunge ni la kukaa kujadili kucha na kope bandia? Na yote haya yanayoendelea nchini? Na changamoto zote hizi? Na wabunge wanacheka??"

Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Oxfam Bi Winnie Byanyima pia kupitia Twitter amemtaka Rais Magufuli kuamka akidai hali inayoendelea ni sawa na uongozi wa mwalimu mkuu wa shule ya msingi.

"Tanzania pia imepiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii wakati wa kazi. Watumishi wa umma wameonywa kuwa umbea kazini utapelekea kufutwa kazi. Hii ni namna ya uongozi wa mwalimu mkuu wa shule ya msingi.Ufanisi katika utendaji huja kwa kuwezesha, kuhamasisha na kuwaamini watendaji. Amka Rais Magufuli."

Naye mbunge wa Arusha Mjini kupitia chama cha Upinzani Chadema Godbless Lema amesema: "Mamlaka ya Spika yanapaswa kuwa na nguvu na uwezo kwa kuisimamia Serikali ktk mambo ya msingi. Mh Lissu hajawahi kupata hadhi ya Ubunge toka aliposhambuliwa kwa risasi.Lakini leo tumeona mamlaka ya Spika yakiweza kuwa imara katika vita ya kucha na kope za Wanawake Wabunge."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii