Sheria mpya kuwasaidia wanawake Morocco dhidi ya udhalilishaji na unyanyasaji wa kingono

ndoa mapema Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jamii hulaumiwa kwa kuchangia kuongezeka kwa msukumo wa mabinti kuolewa

Sheria mpya ambayo inafanya unyanyasaji wa kingono na Udhalilishaji kuwa ni Uhalifu itaanza kutekelezwa nchini Morocco hivi karibuni.

Sheria hiyo ambayo inajumuisha upigaji marufuku wa ndoa za kulazimishwa, inafuatia kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika miaka ya hivi karibuni juu ya kiwango cha udhalilishaji wanawake.

Utafiti mmoja uliofanywa nchini humo, umeonesha kuwa wanawake sita kati ya 10 nchini Morocco wamepitia manyanyaso hayo.

Matukio ya ubakaji ya hivi karibuni yametangazwa sana katika mitandao ya kijamiii.

Mwandishi wav BBC mjini Rabat amesema sheria hiyo mpya imepokelewa vizuri lakini pia imekosolewa kwa sababu haitoi maana kamili ya unyanyasaji majumbani au marufuku katika vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wale wote watakaotiwa hatiani kwa makosa ya kudhalilisha kingono hadharani iwe kwa kutumia maneno, ama ishara yoyote ya kudhalilisha kijinsia atakabiliwa na hukumu ya kifungo kuanzia mwezi mmoja mpaka sita gerezani na pia faini ya fedha taslimu

Mashirika ya haki za binadamu yanasema kuwa wanawake wengi nchini Morocco wamekuwa ni wahanga wa matukio ya unyanyasaji kingono.

Haki miliki ya picha ABDUL WAHID AL SAADI
Image caption Picha hii ni ya mwanamke aliyebakwa na kulazimishwa kuchorwa michoro mwilini na wabakaji

Katika ripoti yake ya mwaka 2015, Shirika la Haki za Binadamu nchini humo limearifu kuwa zaidi ya asilimia 20 ya wanawake nchini Morocco wamekumbwa na matukio ya unyanyasaji wa kingono japo mara moja katika maisha yao

Katika siku za hivi karibuni polisi nchini humo iliwakamata vijana 12 kwa tuhuma za kumbaka msichana wa miaka 17 na kumtesa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Duniani kote inakadiriwa kuwa wasichana milioni 51 waliyo chini ya umri wa miaka 18 wameolewa.

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, ndoa za umri mdogo zimekithiri Afrika Mashariki na Asia ya Kusini .

Inakadiriwa kuwa kufikia muongo mmoja ujao zaidi ya wasichana milioni 100 watakuwa wamekumbwa na ndoa za umri mdogo.

Ni Sababu zipi zinazochangia ndoa za lazima?

  • Jamii nyingine zinachukulia ndoa kama suala la kifamilia. Wazazi au jamaa wa msichana wanaamua ni wakati gani binti yao anastahili kuolewa na wanafanya hivyo bila kumhusisha.
  • Kumlinda mwanamke. Baadhi ya familia zinadai kuwa binti yao anastahili kulindwa asiingie katika familia asiyoijua na huwaoza mapema ili kuhakikisha usalama wao.
  • Kuilinda hadhi ya familia.
  • Dini, baadhi hufuta maagizo au maandiko kama sehemu ya kutekeleza wajibu wa dini yao
  • Ndoa ya lazima hutumiwa kama mbinu ya kumdhibiti mwanamke kingono.
  • Jamii nyingine hutumia aina hii ya ndoa kujinufaisha kiuchumi. Kutokana na hali ngumu ya maisha baadhi ya familia hutumia mabinti zao kama kitega uchumi.
  • Ndoa ya lazima pia hutumika kumuadhibu msichana aliyepata mimba akiwa nyumbani kwa wazazi wake.

Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazochangia kuenea kwa ndoa za lazima katoka jamii.

Kwa mujibu wa watetezi wa haki za binadamu ndoa za lazima ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Ndoa za aina hii kwa kawaidi huhusisha 82% ya wasichana au wanawake ambao wanalazimishwa na wazazi au familia zao kuolewa.

Haki miliki ya picha HISANI

Hali ikoje Tanzania:

Kwa mujibu wa chama cha waandishi wanawake nchini Tanzania, TAMWA, taifa hilo ni moja ya nchi zilizokithiri ndoa za umri mdogo duniani.

Kwa wastani, wasichana wawili kati ya watano huolewa kabla ya kutimiza miaka 18.

Mnamo 2010, 37% ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 walioolewa kabla ya kufikia miaka 18.

Hatahivyo hali hiyo imebadilika huku takwimu zinzonyesha kwamba visa vimepungua kwa 10% tangu mwaka 2004 ambapo viwango vilikuwa 41%.

Betty Masanja, wakili na mwanaharakati wa masuala ya kijamii nchini Tanzania anasema ''Ndoa za lazima zipo sana miongoni mwa jamii ya watanzania. Kuna baadhi ya jamii zinahisi mtu asipoolewa anakosa heshima fulani.Sasa wazazi wanajihisi vibaya kama biti yao ametimiza umri wa kuolewa na bado yuko nyumbani''.

Betty pia anasema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 haiwalindi wasichana dhidi ya kuolewa mapema.

''Sheria hii imekuwa ikipigiwa kelele ifanyiwe marekebisho kwa mda mrefu. Sheria hii inaruhusu wasichana wenye miaka 14 kuolewa kwa ( ruhusa maalum ya wazazi), inaruhusu wasichana wenye umri kuanzia miaka 15 kuolewa iwapo umbile lao linaonekana kubwa. Hali hii ina athari kwa maendeleo ya Taifa''.

Wanaharakati wa masuala ya kijamii wanasema ndoa za umri mdogo ni aina ya ubaguzi wa kijinsia ambao unawagusa wasichana wadogo na kuwafanya wasiendelee na elimu.

Ubaguzi huo unawafanya wawe waathirika wa kuambukizwa virusi vya ukimwi kwa urahisi wakilinganishwa na wenzao ambao hawajaolewa; na hakuna uwezekano wa wasichana hao walioolewa kupanga uzazi.

Ndoa za umri mdogo ni suala la afya pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu, kwani wasichana walioolewa katika umri mdogo wana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na maradhi ya fistula na vifo vya kina mama kwani miili yao inakuwa bado haijawa na uwezo wa kuhimili mzigo wa kuzaa.

Haki miliki ya picha ALBERT GONZALEZ FARRAN

Hali katika mataifa mengine Duniani

Serikali ya Uingereza iliharamisha ndoa ya lazima nchini humo mnamo 2012.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kumlazimisha mtu kuoa au kuolewa bila ya hiari yao ni uhalifu Uingereza, Wales na Ireland ya Kaskazini.

Inakadiriwa kuwa kuna kati ya waathiriwa 5000 - 8000 waliolazimishwa kuoa au kuolewa nchini Uingereza.

Wasichana wengi wanaolazimisha kuolewa wana umri wa chini ya miaka 21 lakini kuna ripoti kuwa wasichana wa hata umri wa miaka 15 hulazimishwa kuolewa.

Familia nyingi zinazotuhumiwa kutekelaza uhalifu huo zinatoka mataifa ya bara Asia hususan taifa la Pakistan.

Katika baadhi ya majimbo nchini Marekani, ndoa ya lazima ni uhalifu. Katika majimbo hayo watu wanaomlazimisha mtu kuoa au kuolewa huwa wamekiuka sheria, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji majumbani ukiwemo wa kingono, utekaji nyara na kadhalika.

Nini kifanyike kupambana na ndoa za lazima

Umoja wamatiafa unasisitiza umuhimu wa kuzingatia elimu endelevu kwa kutumia vyombo vya habari, utafiti, mabadiliko ya sheria na mikutano ya kijamii.

Kadhalika ipo haja ya kuhamasisha viongozi wa kijamii kuhusu athari za ndoa za lazima na sheria zilizopo.

Sekta ya afya inmetaja kuwa na jukumu kuu la kuwahamasisha wananchi kuhusu athari za ndoa za umri mdogo.

Kuwahusisha katika mjadala huu viongozi wa dini katika kuielimisha jamii, na pia wazazi, katika kushirikiana na serikali kukomesha ndoa za aina hii.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii