Kimbunga Florence: Tahadhari ya uharibifu mkubwa Marekani yatolewa na watu milioni kulazimishwa kuhama Marekani

Wateja wakiwa katika duka la kuuza gesi ya kupikia Myrtle Beach, South Carolina Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wateja wakiwa katika duka la kuuza gesi ya kupikia Myrtle Beach, South Carolina

Kimbunga Florence - ambacho kinatarajiwa kuwa kimbunga kikali zaidi kupiga maeneo la Carolina nchini Marekani katika kipindi cha miongo mitatu kinaendelea kuongeza nguvu, watabiri wa hali ya hewa wanasema.

Maafisa wametahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mafuriko na maji ya bahari kujaa kiasi cha kutishia maisha ya watu.

Watu takriban milioni moja wametakiwa kuhama makwao.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kufika pwani ya Mashariki ya Marekani kufikia Alhamisi.

Florence ni kimbunga kilicho na upepo unaovuma kwa kasi ya maili 140 kwa saa (225km/h), na kimeorodheshwa kama kimbunga cha ngazi ya nne.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kupiga maeneo ya Wilmington, North Carolina kwanza.

Majimbo ya Virginia, Maryland, Washington DC, na North na South Carolina yote yametangaza hali ya tahadhari.

"Kimbunga hiki ni jinamizi," gavana wa North Carolina Roy Cooper aliwaambia wanahabari Jumanne.

"Ni kikali sana na hatari."

Kimbunga Florence kimefika wapi sasa?

Kimbunga hicho kilikuwa kimefikia maili 670 (1,078km) kusini mashariki mwa Cape Fear, North Carolina, kufikia saa 23:00 saa za kawaida eneo la Atlantiki Jumanne, ambazo ni sawa na saa 03:00 GMT Jumatano kwa mujibu wa taarifa za karibuni zaidi kutoka Kituo cha Taifa cha kufuatilia Vimbunga.

Taarifa za karibuni zaidi zinaeleza kwamba kimbunga hicho ambacho kinaelekea kaskazini magharibi kwa kasi ya maili 17 kwa saa (28km/h) -kinatarajiwa kuongeza nguvu usiku wa Jumanne na leo Jumatano.

"Kinatarajiwa kupungua nguvu kidogo Alhamisi, lakini kinatarajiwa kuwa hatari sana kufikia wakati wa kufika kwake maeneo ya bara," kituo hicho kimesema.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu Alhamisi na baadaye Ijumaa.

Kinaweza kusababisha uharibifu wa aina gani?

Idara ya Taifa ya utabiri wa hali ya hewa inasema kimbungahicho kinaweza kusababisha mawimbi ya urefu wa hadi futi 13 (4m) ambayo yatapiga maeneo ya pwani.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Watu wanaokimbia makwao wakitafuta hifadhi Wilmington, North Carolina

Mtaalamu wa utabiri wa hali ya hewa wa WCBD-TV South Carolina, Rob Fowler, ameambia BBC kwamba kimbunga hicho huenda kikazidi kimbungwa kwa jina Hugo, ambacho kilisababisha uharibifu wa $7bn (£5.3bn) na kuwaua watu 49 mwaka 1989.

Kimbunga hicho huenda kikaathiri kiwanda cha nyuklia cha Brunswick eneo la Southport, North Carolina. Kiwanda hicho kinapatikana maili kadha kutoka eneo ambalo kimbunga hicho kinatarajiwa kufika bara kwanza.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Watu wakifunga madirisha ya nyumba zao Wrightsville Beach wakijiandaa kuhama

Trump amesema nini?

Rais wa Marekani Donald Trump ameidhinisha matangazo ya hali ya dharura katika majimbo la North na South Carolina, kuwezesha kutolewa kwa pesa na rasilimali za dola kusaidia juhudi za kuwaokoa watu.

Akiongea ikuluni Jumanne, alisema serikali itatumia kila juhudi kuwasaidia wananchi.

Mwaka uliopita, kimbunga Maria kiliwaua watu 2,975 na kusababisha uharibifu mkubwa katika jimbo la Puerto Rico linalomilikiwa na Marekani.

Kuna kimbunga kingine?

Maafisa katika jimbo la Hawaii wamewatahadharisha wakazi kuhusu kimbunga kingine kwa jina Olivia.

Watabiri wa hali ya hewa wanasema Olivia - kimbunga chenye upepo unaovuma kwa kasi ya maili 65 kwa saa, kitafikia maeneo ya bara Jumatano asubuhi na kusababisha mvua kubwa.

Mada zinazohusiana