Madeni Afrika: Je, ni kweli China itatwaa uwanja wa ndege na kampuni ya umeme Zambia?

ZAMBIA DENI Haki miliki ya picha STATE HOUSE ZAMBIA
Image caption Deni la Taifa la Zambia linatazamiwa kufika $13 bilioni mwaka 2019. Takribani asilimia 30 ya deni hilo ni mkopo kutoka Uchina.

Uhusiano wa China na mataifa ya Kiafrika kwa muda mrefu umekuwa wa kupigiwa mfano, lakini katika miaka ya hivi karibuni hali imekuwa tofauti.

Serikali ya Zambia wiki hii imelazimika kukanusha taarifa za kushtusha kuwa nchi ya Uchina iko mbioni kuhodhi uwanja mkubwa wa ndege wa nchi hiyo Kenneth Kaunda International Airport (KKIA) pamoja na Shirika la kufua na kusambaza umeme (Zesco).

Taarifa zilizosambaa mitandaoni ni kuwa Zambia imeshindwa kutimiza masharti ya mkopo wake hivyo itaipatia KKIA na Zesco kwa serikali ya Uchina ili iendeshe mashirika hayo kibiashara na kuchukua faida kama sehemu ya kulipa madeni.

Kutokana na utegemezi wa mikopo ya Uchina katika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika nchi za kiafrika watu wengi barani waliguswa na hayo yaliyotajwa kuendelea nchini Zambia na kuhofia kuwa yanaweza kuingia katika nchi zao baada ya Zambia.

Kwa mujibu wa taasisi ya China Africa Research Institute iliyo chini ya Chuo Kikuu cha John Hopkins cha nchini Marekani, mikopo ya China kuelekea Afrika imekua kutoka $5 bilioni mpaka $30 bilioni kufikia mwaka 2016.

Kwa ujumla, Uchina imekopesha nchi za Afrika $136 bilioni kutoka mwaka 2000 mpaka 2017. Angola ndiyo nchi inayoongoza kwa kukopa kutoka Uchina amabapo katika miaka 17 iliyopita wamepokea jumla ya $42 bilioni.

Taarifa hizo kuihusu Zambia zimeripotiwa na jarida la Africa Confidential baada tu ya mkutano wa kimataifa wa Uchina na nchi za kiafrika ambapo serikali ya Uchina imetangaza kutoa mikopo yenye thamani ya $60 bilioni kwa nchi zote 54 za Afrika.

Image caption Mikopo ya China kwa Afrika

Kupitia msemaji wake mkuu Bi Dora Siliya serikali ya Zambia imesema haijashindwa kulipa madeni yake na kutaka taarifa hizo kupuuzwa.

Bi Siliya amesema laiti kungelikuwa na hatua kama hizo, basi ni baraza la mawaziri la nchi hiyo ndilo lingelifikia uamuzi huo, na kuwahakishia raia wa nchi hiyo kuwa hakuna kitu kama hicho.

Deni la Taifa la Zambia linatazamiwa kufika $13 bilioni mwaka 2019. Takribani asilimia 30 ya deni hilo ni mkopo kutoka Uchina.

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaonya kuwa Zambia inaingia kwenye mtego wa madeni ya kimataifa na yaweza kupata tabu kulipa kama itaendelea kukopa kwa kasi.

Hofu ya uhimilivu wa deni la taifa pia limeyakumba mataifa mengi Afrika ikiwemo Tanzania.

Mpaka kufikia Juni 2017, deni la Tanzania ni Sh46 trilioni. Katika deni hilo, Sh13.34 trilioni sawa na 29 ni deni la ndani na Sh32.75 trilioni sawa na asilimia 71 ni deni la nje.

Serikali ya Tanzania inasema Deni hilo lote ambalo ni sawa na 31% ya Pato la Taifa ni himilivu.

Kwa upande wa Kenya, deni limefikia Sh4.5 trilioni na ukuaji wake kwa miaka 10 iliyopita ni wa kasi ya juu. Kama ilivyo kwa upande wa Tanzania serikali ya Kenya inasema deni hilo ni himilivu na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii