Hospitali ya Muhimbili kufanya upasuaji kwa watoto 400 kwa mwezi

UPASUAJI MUHIMBILI
Image caption Watoto zaidi ya 10 sasa kufanyiwa upasuaji kwa siku katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Nchini Tanzania watoto takriban 400 wananufaika na huduma ya upasuaji kila mwezi katika hospitali kuu ya Muhimbili.

Hii ni baada ya kujengwa kwa vyumba viwili maalumu vya upasuaji kwa watoto kwa msaada wa shirika moja lenye maskani yake nchini Uingereza katika mpango wake maarufu ujulikanao kama KidOR, yaani vyumba vya upasuaji vya watoto.

Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau ametembelea moja ya vyumba hivyo na kushuhudia moja ya upasuaji wa watoto kwenye chumba hiko. Vyumba hivyo kwa Tanzania vinapatikana katika hospitali ya Muhimbile pekee.

Awali kulikuwa na msongamano mkubwa wa watoto wanaotaka kufanyiwa upasuaji. Hivyo baadhi kuwekwa katika orodha ya kusubiri kufanyiwa upasuaji kwa takriban miaka mitatu.

Lakini hivi sasa, ahueni imepatikana, wagonjwa takriban kumi wanafanyiwa upasuaji kila siku katika hospitali hii. Hivyo kupunguza muda wa kusubiri kupata matibabu hadi kufikia wiki mbili.

Dk. David Cullingham ambae ni mkurugenzi mkuu wa shirika la Uingereza linalodhamini mradi huu wa vyumba vya upasuaji kwa watoto anasema hali hii sio tu kwamba inasaidia kuokoa maisha ya watoto, lakini pia, inawapa fursa watoto wanaopata matibabu kukua salama na kutoa mchango kwa jamii zao.

"Kumfanyia upasuaji mtoto mdogo mathalan wa miaka miwili na kumuondolea ulemavu kunamuwezesha kuishi kwa afya njema kwa miaka sitini mpaka sabini mbele. Watoto hawa watachangia kukua kwa uchumi wa taifa kwa kufanya kazi," amesema Dk. Cullingham, na kuongeza, "Vyumba hivi pia vya upasuaji vitachangia katika kuwafunza madaktari wa upasuaji na kuwaongezea ujuzi. Faida yake ni kubwa sana. "

Dk. Zaituni Buhari, ni tabibu bingwa wa upasuaji wa watoto, katika hospitali ya Muhimbili na ameiambia BBC kuwa watoto wengi wanaofikishwa hospitalini hapo ni wale waliozaliwa na matatizo kama vile kukosa sehemu za siri, huku wengine wakifanyiwa marekebisho ya sehemu zao za haja kubwa.

Image caption Watoto wengi wanaofikishwa hospitalini hapo ni wale waliozaliwa na matatizo kama vile kukosa sehemu za siri, au kuhutaji marekebesho ya sehemu hizo.

"Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na vyumba vya watoto katika hospitali kubwa kama hii ya Muhimbili. Kama wanaokuja (wagonjwa) ni wengi na hatuna vyumba vya kutosha, wale watoto tunakuwa tunaweka kwenye kusubiri kwa muda mrefu. Zamani kabla ya vyumba hivi walikuwa wanasubiri miaka miwili mpaka mitatu (kufanyiwa upasuaji)," amesema Dk. Buhari.

Wazazi nao wanaonekana kupata faraja baada ya kuona watoto wao wamepata matibabu. Anastazia Charles, mama wa mmoja wa watoto aliefanyiwa upasuaji ameiambia BBC kuwa anafuraha kuona mwanae amepata matibabu na kuwa na maendeleo mazuri.

"Ninafuraha sana. Hata ukipasua moyo wangu uutaona furaha yangu kulingana na hali ya mwanangu jinsi ilivyokuwa toka tulipofika mpaka amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri kabisa. Nashukuru sana."

Tanzania na Uganda ni miongoni mwa nchi ambazo mpaka sasa tayari zimenufaika na mradi huu wa kujengewa vyumba maalumu kwa upasuaji wa watoto. Lengo kuu likiwa ni kujenga vyumba kama hivi takriban kumi na tano katika nchi kadhaa barani Afrika, ifikapo mwaka 2019.

Mada zinazohusiana