Victoire Ingabire: Alizuiliwa kugombea uraisi wa Rwanda kufuatia mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.

Victoire Ingabire atabasamu baada ya kuachiliwa huru

Victoire Ingabire Umuhoza alizaliwa oktoba tarehe tatu mwaka 1968.

Ni mke na mama wa watoto wa tatu.

Amesomea Sheria na masuala ya uhasibu na hatimaye kufuzu kwa shahada ya uchumi na biashara nchini Uholanzi.

Tangu mwaka 1997, Ingabire amejihusisha na harakati za upinzani nchini Rwanda akiwa mafichoni Uholanzi.

Aliteuliwa na muungano wa kundi la viongozi wa upinzani ambao una wanachama nchini Rwanda, barani Ulaya, Marekani na Canada.

Mnamo mwezi Januari mwaka 2010 Bi Ingabire alirejea Rwanda kutoka mafichoni nchini Uholanzi baada ya kutajwa kuhusika kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ili kugombea uchaguzi wa urais.

Mwezi Aprili mwaka 2010, aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani.

Alikamatwa baadaye na kufikishwa mahakamani ambapo yeye na washirika wake wanne, (Kanali Tharcisse Nditurende, Luteni kanali Noel Habiyaremye, Luteni Jean Marie Vianney Karuta na Meja Vital Uwumuremyi), walifunguliwa mashataka ya uhaini.

Alizuiliwa kugombea uraisi wa Rwanda kufuatia mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.

Wakuu wa mashtaka wa Rwanda walimfungulia kesi kwa tuhuma za kuunda kundi lenye lengo la kusambaratisha nchi, kulazimisha vitendo vya ugaidi, na kuwachochea raia kuasi dhidi ya serikali.

Mashtaka ambayo alikanusha na kusema kuwa yalichochewa kisiasa.

Oktoba 30 2012, mahakama kuu mjini Kigali ilimhukumu kifungo cha miaka minane jela baada ya kumpata na hatia ya kupanga njama dhidi ya serikali kupitia vitendo vya ugaidi na vita.

Disemba mwaka 2013, mahakama ya juu zaidi nchini Rwanda ilidumisha hukumu ya mahakama kuu dhidi yake na kumuongezea kifungo gerezani kutoka miaka minane hadi miaka 15.

Bi Ingabire, ni mwanachama wa jamii ya Wahutu na alihoji kwa nini makumbusho rasmi ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda hayakujumuisha Mhutu yeyote.

Wengi wa watu 800,000 waliouawa walikuwa Watutsi lakini baadhi ya Wahutu waliowaunga mkono Watutsi waliuawa na Wahutu wenye misimamo mikali.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii