Matumizi ya Bangi: Kinywaji cha Coca-Cola kitakachokuwa na bangi kitalewesha?

Medical cannabis Haki miliki ya picha Getty Images

Kampuni maarufu ya vinywaji ya Coca-Cola ni maarufu zaidi kwa kutengeneza soda, lakini sasa inapanga kufanyia majaribio aina mpya ya kinywaji.

Kinywaji ambacho kitakuwa na bangi. Lakini je, kitalewesha?

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa BNN Bloomberg, kampuni hiyo itashirikiana na kampuni mwenyeji ya kutengeneza bangi kwa jina Aurora Cannabis.

Lengo kuu la kuwa na kinywaji hicho litakuwa ni kupunguza maumivu na si kuwalewesha watu.

Kampuni hiyo bado haijazungumzia hadharani mpango huo lakini imekiri kwamba inafuatilia kwa karibu matukio katika sekta ya vinywaji vyenye bangi.

"Kwa pamoja na wadau wengine wengi katika sekta hii ya vinywaji, tunafuatilia kwa karibu ukuaji wa soko la vinywaji vyenye bangi aina ya cannabidiol visivyolewesha kama kiungo katika vinywaji vya kuboresha afya maeneo mengi duniani," taarifa ya Coca-Cola imesema.

Cannabidiol, ni moja ya viungo vinavyopatikana ndani ya bangi, na inaweza kusaidia kupunguza kuvimba, maumivu na kuganda kwa misuli.

Lakini huwa haiwezi kulewesha.

Hatua ya Coca-Cola inajiri huku Canada ikijiandaa kuyafuata baadhi ya majimbo ya Marekani ambayo majuzi yameidhinishwa matumizi ya bangi kwa sababu za kujiburudisha, baada ya kukubali matumizi ya bangi kwa sababu za kimatibabu kwa miaka mingi.

Hatua hiyo imechangia kuibuka kwa biashara kubwa ya ukuzaji wa bangi, pamoja na kuundwa kwa ushirikiano wa kampuni kubwa katika biashara hiyo.

Mapema mwaka huu, kampuni kubwa ya utengenezaji wa bia ya Molson Coors Brewing ilitangaza kwamba itakuwa ikitengeneza vinywaji vyenye bangi kwa ushirikiano na kampuni ya Hydropothecary, huku kampuni inayotengeneza bia ya Corona, Constellation Brands, ikiwekeza zaidi ya $4bn zaidi katika kampuni ya bangi ya Canopy Growth.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Makundi mengi yamekuwa yakitetea kuhalalishwa kwa bangi

Ushirikiano kati ya Coke na Aurora utakuwa ni kisa cha kwanza kabisa kwa kampuni kubwa ya uzalishaji wa vinywaji visivyolewesha kujiingiza katika biashara hiyo ya bangi.

'Kinywaji chenye kuponya'

BNN Bloomberg, wakinukuu wadokezi ambao hawakutaka kutajwa, wamesema Coca-Cola wanafanya mazungumzo "yenye uzito" na Aurora lakini kufikia sasa hawajapata maafikiano yoyote.

"Mazungumzo yamepiga hatua sana" na maafikiano yanakaribia kupatikana, mdokezi mmoja alinukuliwa akisema.

"Itakuwa ni katika kitengo cha 'vinywaji vya kuponya' (au kumpa mtu ahueni)," mdokezi huyo ameongeza.

Aurora, kupitia taarifa wamesema hawataki kuzungumzia mipango yao ya kibiashara hadi ikamilishwe.

Lakini aliongeza: "Aurora wameeleza hamu yao kuu katika kutumia fursa ya kibiashara katika vinwyaji vyenye kuongezwa vileo, na tunakusudia kuingia katika soko hilo."

Hisa za Coca-Cola zilipanda bei kiasi mapema Jumatatu.

Bangi ni nini hasa?

Bangi, kwa Kiingereza Cannabis, ni moja ya dawa za kulevya zinazotumiwa kwa wingi duniani.

Hutokana na mmea wa bangi na huwa na kemikali ana ya tetrahydrocannabinol (THC), ambayo huathiri akili za mtu na kumfanya ajihisi vyema, jambo linalowafanya baadhi kuitumia wakiamini itawasaidia kupunguza mawazo.

Lakini inaweza kuwafanya watu kuwa na njozi na kuwa na wasiwasi usio wa kawaida. Husababisha uraibu, na asilimia 10 ya watumiaji wa kawaida wa bangi huwa waraibu.

Bangi mara nyingi huvutwa kama sigara, lakini hupatikana kwa aina tatu kuu:

  • Hash - ambalo ni kama tonge la kitu kinachonata
  • Marijuana - ambayo ni majani na maua ya bangi
  • Mafuta - ambayo muonekano wake ni kama wa asali

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kilimo cha bangi, uzalishaji, usafirishaji na matumizi yake bado ni changamoto kubwa katika nchi nyingi za bara la Afrika zikiwemo Tanzania, Nigeria na Ghana.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Bangi mara nyingi huvutwa kama sigara

Mataifa mengi yamehalalisha matumizi ya bangi kwa sababu ya kimatibabu, zikiwemo Marekani, Ujerumani, Italia na Uholanzi.

Bunge nchini Canada miezi kadha iliyopita liliidhinisha matumizi ya bangi kwa ajili ya kujiburudisha.

Uruguay iliidhinisha matumizi ya bangi kujiburudisha mwaka 2013 na kuwaruhusu watu kukuza hadi mimea sita ya bangi kwa matumizi ya nyumbani.

Nchini Uhispania, inaruhusiwa kukuza bangi kwa matumizi ya kibianafsi katika maeneo ya kibinafsi.

Matumizi ya bangi Uholanzi kimsingi yameharamishwa lakini mtu binafsi anaruhusiwa kuwa na gramu 5 za bangi za matumizi ya kibansfi ingawa polisi wanaweza kumpokonya mtu bangi hiyo. Matumizi ya bangi yanaruhusiwa katika migahawa maalum.

Bangi ni dawa?

Cannabis pia huwa na cannabidiol (CBD), ambacho ndicho kiungo Coca-Cola wanatarajiwa kutumia.

Wanasayansi wamekuwa wakichunguza matumizi ya kiungo hicho kama dawa.

Tiba za kutumia CBD zimeonyesha mafanikio makubwa katika kupunguza athari za kifafa, hasa kwa watoto.

Majaribio mengi yamefanywa yakiangazia jinsi inaweza kutengenezwa katika viwanda, lakini baadhi ya wazazi wenye watoto wenye kifafa wamekuwa wakinunua mafuta ya bangi yenye CBD na THC.

Kufikia sasa, hakuna ushahidi sana wa kisayansi kuhusu usalama na kufanikiwa kwa mafuta haya kama tiba ya kifafa, ingawa ni kweli huwa yana viungo vilivyobainishwa kusaidia kutibu athari za ugonjwa huo.

Sativex, ambayo ni dawa ya kufukizia yenye bangi, imekuwa ikitumia kwa ushauri wa madaktari kisheria Uingereza tangu 2006.

Hutumiwa kutibu kuganda na kushikamana kwa misuli pamoja na mkazo wa ghafla wa misuli kwa watu wenye ugonjwa wa kukacha kwa seli au tishu kwa Kiingereza multiple sclerosis.

Madaktari wakati mwingine huwashauri wagonjwa kuitumia kwa sababu nyingine, lakini nje ya matumizi yaliyoruhusiwa kisheria.

Kuna dawa nyingine iitwayo Nabilone inaoruhusiwa kutumiwa. Huwa na aina ya kemikali ya THC ya kuundiwa kwenye viwanda na inaweza kuwasaidia wanaougua saratani kupunguza kichefuchefu wakati wanapopokea tibakemikali.

Madhara yanayotokana na kutumia bangi

• Kuongezeka kwa ugumu wa kukumbuka mambo

• Upotovu wa fikira na mtazamo, na kuwa na mawazo yaliyotiwa chumvi au yasiyokuwa na mantiki

• Njozi

• Wazimu

• Wasiwasi

• Mfadhaiko

• Upungufu wa kudumu wa kiwango cha mtu kufikiria na kufahamu mambo, baada ya kutumia kwa muda mrefu

Baadhi ya dalili anazoonyesha mtu anayetumia bangi:

• Kuonekana kuwa na kizunguzungu au kutokuwa na msimamo

• Kuonekana mjinga na kuchekacheka bila sababu

• Kuwa na macho mekundu sana, macho yaliyo na rangi ya damu

• Kuwa na wakati mgumu kukumbuka mambo ambayo yametokea muda mfupi uliopita

Kama mtu anatumia bangi mara nyingi, anaweza:

• Kuwa na harufu kwenye nguo na katika chumba cha kulala

• Kutumia uvumba na viondoa harufu vingine katika eneo la kukaa

• Kuongeza matumizi yao ya manukato, Cologne au nana za pumzi

• Kutumia matone ya macho, katika kujaribu kupunguza wekundu wa macho

• Kuvaa nguo au kujitia au kuwa na mabango ya kuendeleza matumizi ya dawa za kulevya

• Kuwa na matumizi yasiyoelezeka ya fedha au anaweza kuiba fedha

• Kuwa na vitu vinavyotumika pamoja na dawa za kulevya kama vile mabomba, bongs, mizani, karatasi za kukunja, butu ya kufungia au kalamu ya mvuke.

Chanzo: Mwongozo wa wazazi wa kuzuia matumizi ya bangi uliotayarishwa na Seattle Children's Hospital Adolescent Substance Abuse Program

Coca-Cola ina uhusiano na Kokeini?

Coca-Cola ni moja ya kampuni maarufu duniani, ambayo hutengenezwa soda maarufu ya Coke na vinywaji vingine vya soda. Lakini, ilikuwaje hadi ikawa na jina hilo?

Labda umewahi kusikia kwamba Coca-Cola wakati mmoja ilikuwa na kiungo cha kusisimua ambacho kiliwafanya wateja kulipenda sana. Hii ni moja ya vilivyochangia jina lake.

"Coca", kwa Kiswahili koka, ni jina la jani la mmea wa koka, moja ya viungo ambavyo mvumbuzi wa kinywaji hicho, mwanakemia wa Atlanta John Stith Pemberton, alichanganya na shira kutengeneza kinywaji chake.

Majani ya koka hutumiwa kutengeneza kokeini.

Wakati huo, mwishoni mwa karne ya 19, ilikuwa kawaida kwa majani ya koka kuchanganywa na divai na kuwa kinywaji cha kuchangamsha mwili.

Kinywaji kipya alichotengeneza Pemberton kilikuwa njia nzuri ya kukwepa sheria zilizoharamisha uuzwaji wa pombe.

Sehemu hiyo nyingine ya jina Coca-Cola inatokana na kiungo kingine chenye nguvu, ingawa si maarufu sana.

Kiungo hiki ni kola.

Unaweza kusoma zaidi: Coca-Cola ilivyopata jina lake

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii