Mbunge Bobi Wine asindikizwa na polisi baada ya kuwasili Uganda

Bobi Wine
Image caption Bobi Wine akiwa uwanja wa ndege JKIA

Mwanamuziki na mbunge nchini Uganda Bobi Wine ameshikwa na polisi baada ya kuwasili nchini Uganda kutoka Marekani ambapo alikuwa akipata matibabu.

Awali Wine alisema kuwa alihofia kurudi Uganda "kutoka na vile serikali ilikuwa ikiendesha shughuli zake".

Aliyasema hayo kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi kabla ya kuabiri ndege kwenda Uganda

Bobi Wine, ambaye jina lake kamili ni Robert Kyagulanyi anakabiliwa na mashtaka ya uhaini kutokana na kupigwa mawe msafara wa Rais Yoweri Meseveni wakati wa kampeni ya uchaguzi mdogo.

Mapema nduguye Wine Eddy Yawe na naibu msemaji wa chama cha Democratic party Waiswa Alex Mufumbiro, walikamatwa na vikosi vya usalama na kuzuiwa kwenye kituo cha polisi uwanja wa Entebbe.

Image caption Wine akiwa nyumbani kwake

Ripoti pia zinasema kuwa kila mtu wa familia aliyewasili uwanja wa Entebbe alikamatwa, licha ya polisi kusema awali kuwa watawaruhusu watu wa familia kumkaribisha Bobi Wine.

Tangu atangaze kurudi Uganda, makamanda wa polisi mjini Kampala wamekuwa wakifanya mikutano tangu Jumatatu kujiandaa kurudi kwa mbunge huyo.

Taarifa za polisi zilisema kuwa vikosi vya kupambana na ghasia vimepelekwa kwenye barabara ya Entebe, katikati mwa mji wa Kampala, Kamwokya (alikokulia Bobi Wine na Kasangati.

Kiwango kikubwa cha polisi kimepelekwa kwenye barabara ya kutoka Kampala kwenda Entebbe ambapo watu wanaweza kukusanyika kumuona Bobi Wine.

Polisi wanasema Bobi Wine hajapewa kibali cha kufanya mkutano au shughuli yoyote.

Msemaji wa polisi mjini Kamapala Luke Owoyesigyire, alionya kuwa yeyote ambaye atashiriki kwenye shughuli yoyote inayomhusu Bobi Wine atakamatwa

Haki miliki ya picha Bobi Wine/ Twitter
Image caption Bobi Wine akiondoka Marekani

Kwenye video aliyochapisha kwenye mtandao wa Facebook, Bobi Wine anasema serikali inapanga kuzua ghasia ili kuwalaumu wafuasi wa chama cha People Power.

Kulinganga na Bobi, baadhi ya watu wanachapisha shati nyekundu za wafuasi wa People Power na kuwapa majangili wa serikali ili wapate kuzua ghasia ndio waonekane kuwa wao ni wafuasi wake.

Bobi Wine amekuwa nchini Marekani kwa muda wa siku 18, baada ya kuruhusiwa kwenda kupata matibabu tarehe 31 Agosti.

Anadai aliteswa vibaya baada ya kukamatwa kutoka Hoteli ya Pacific mjini Arua alikokuwa akifanya kampeni ya uchaguzi.

Alifikishwa baadaye mbele ya mahakama ya kijeshi huko Gulu kwa kumiliki silaha kinyume na sheria mshataka ambayo yalifutwa baadaye.

Akiwa nchini Marekani Bobi Wine alifanya mikutano kadhaa na waandishi wa habari, akahojiwa na vituo vingi vya televisheni za kimtaifa na kuhudhuria misa na raia wa Uganda wanaoishi huko Boston.

Mada zinazohusiana