MV Nyerere: Hatimaye shughuli ya kukinyanyua Kivuko cha MV Nyerere yakamilika Tanzania

kivuko Haki miliki ya picha Stephen Msengi
Image caption Kivuko cha Mv Nyerere chanyanyuliwa

Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo amesema jitihada za kukiinua kivuko zimefanikiwa leo mnamo saa saba na nusu mchana na sasa hivi kipo wima (Upright),

Kwani mwanzo kilikua kimelala kifudi fudi, kisha jana kikalala ubavu na leo wamefanikiwa kukiinua na kuwa wima kazi iliyobaki ni kuondoa maji kwenye kivuko ili kiweze kuelea moja kwa moja ili kivutwe na kurudi nchi kavu.

Jenerali Venance anapongeza vyombo vya ulinzi na usalama katika ngazi zote, pia kampuni ya Mv Mkombozi kwa kuleta meli yao, GGM wameongeza nguvu ya vifaa, Songoro Marine na Orioni 2 Pamoja na wananchi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ametoa idadi ya watu waliopoteza maisha na miili iliyopatikana leo ni mwili wa mtoto mmoja na kufanya idadi ya watu 228 kufariki kutokana na ajali hiyo.

Aidha waziri amesema kuwa bado wapo kwenye eneo la ajali Ukara wakiendelea na uokoaji wa miili itakayopatikana ikiwa na chombo hiki kugeuza.

Kivuko cha MV Nyerere chanasuliwa Ukerewe Tanzania

Japhet Masele Mtendaji Mkuu mpya wa TEMESA amewasili mpaka jioni wameendelea kuangalia uwezekano wa kurejesha huduma katika eneo hili na wamepata injini inayoendelea kufungwa katika kivuko cha Mv. Ukara.

Mv Ukara yenye uwezo wa kubeba watu 70, itaanza mazoezi tayari kwa kuanza kutoa huduma wakati wanasubiri huduma ya kudumu na wananchi kuweza kuendelea katika shighuli zao za kiuchumi.

Haki miliki ya picha TANZANIA

Wadau mbalimbali wanaoendelea kutoa rambi rambi leo hii waliotoa ubani ni pamoja na TPA wametoa Milioni 20, TPB Benki wametoa milioni 5.

Michango Kufikia saa 2 asubuhi ni Milioni 764 za kitanzania.

Fedha iliyotumika ni milioni 266 za kitanzania na fedha iliyobaki benki ni milioni 498 kitanzania.

Haki miliki ya picha Steve Msengi

Kivuko cha MV Nyerere kilizama Alhamisi adhuhuri kikitokea bandari ya Bugolora katika kisiwa cha Ukerewe kuelekea katika kisiwa cha Ukara na kusababisha vifo vya watu wapatao 228 na wengine 40 kuokolewa.

Magufuli achukua hatua kali dhidi ya wahusika

Tayari rais Joh Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na majini SUMATRA Mhandisi Dkt. John Ndungura .

Taarifa ya Ikulu iliotolewa siku ya Jumatatu na kusainiwa na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Gerson Msigwa, ilisema kuwa kiongozi huyo pia aliivunja bodi hiyo .

Magufuli alichukua uamuzi huo kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere na msururu wa ajali za barabarani ambazo zimesababisha vifo, ulemavu na kuharibu mali.

Siku ya Jumapili Magufuli alifutilia mbali bodi ya ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme TAMESA na kumfuta kazi mwenyekiti wake John Ndunguguro kwa sababu kama hizo.

Abiria wana haki

Akizungumza na BBC Mwenyekiti wa chama cha kutetea abiria Hassan Mchanjama anasema abiria wanaotumia feri wana haki sawa na za abiria yeyote ambaye anaweza kutumia usafiri kama wa barabara na wale waliopoteza maisha wanastahili kufidiwa.

Anasema kwa kuwa vyombo vya majini mara nyingi havina bima lakini chombo cha MV Nyerere kinamilikiwa na serikali kwa hivyo anayestahili kuwajibika zaidi ni hapa serikali yenyewe.

Ameongeza kusema kuwa kutokana na kuwa vyombo vya majini havina bima, serikali inastahili kuhakikisha kuwepo mfuko maalum wa kuwafidia abiria wanaopata madhara kama hayo, kuweza kufidiwa kwa kuwa mara unapata watu hawa wengi ni tegemeo kwenye familia, kwa hivyo bila ya kufanya hivyo umaskini utaendelea.

Mada zinazohusiana