Melania Trump: Mke huyo wa rais Trump ameiorodhesha Kenya kuwa miongoni mwa mataifa anayozuru Afrika

Melania Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Melania Trump

Mke wa rais wa Marekani bi Melania Trump ametangaza mpango wake wa kuzuru mataifa manne ya Afrika ikiwemo Ghana, Malawi, Kenya na Misri oktoba mosi.

Melania amesema kuwa amechagua mataifa hayo kwa sababu yamefanya kazi na shirika la misaada la Marekani USAID na washirika wake ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazokumba jamii.

Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa baraza kuu la umoja wa mataifa unoendelea mjini New York, bi Melania amesema''Najivunia sana kufanya kazi na mataifa haya kupitia USAID na wadau wengine na nina tazamia kuendeleza mbele kampeini ya 'Be Best' katika mataifa mengine barani Afrika'

Mchango wa USAID Afrika

Melania ameongeza kuwa Ghana kwa mfano kwa ushirikiano na shirika la USAID inajishughulisha na masuala ya afya kwa kusaidia mikakati ya kuimarisha afya ya kinamama na watoto wachanga pamoja na kuwahamasisha kinamama hao umuhimu wa kuzingatia lishe bora.

Pia ameipongeza Malawi kwa kuonyesha ishara kwamba elimu ni moja ya nguzo muhimu itakayoweza kukabiliana na umasikini na kustawisha jamii.

Haki miliki ya picha Reuters

Akizungumzia kwa kina mipango ya ziara hiyo barani Afrika , Melania amesema kuwa ziara hiyo inaandaliwa na shirika la kimataifa la misaada ya Marekani kama sehemu ya kampeini yake inayojulikana kama 'Be Best' ambayo inalenga kuboresha hali ya watoto hasa masuala ya uraibu wa mitandaoni.

"Kila mmoja wetu anatokea taifa lililo na changamoto zake lakini naamini moyoni mwangu kwamba sote tuna nia ya kukuza kizazi ambacho kina furaha, afya na kuwajibika siku za usoni''

Elimu na Wanyama Pori

Katika kanda ya afrika mashariki, Melania amesema kuwa atatembelea Kenya kutokana na juhudi za nchi hiyo za kuimarisha elimu na kuhifadhi wanyama pori kwa ushirikiano na shirika la USAID.

Haki miliki ya picha IKULU, KENYA

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema ziara ya hivi majuzi ya kihistoria ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta huenda imechangia pakubwa uamuzi wa Bi Melania kuja Kenya hasa ikizingatiwa rais Kenyatta alifanya mashauri ya ana kwa ana na Rais Trump.

Melania Trump na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta walifanya mashauri ya faragha katika chumba cha masuala ya kidiplomasia katika upande wa Magharibi wa Jengo la White House.

Je ziara ya rais Uhuru Marekani ilichangia zaira ya Melania Kenya?

Kwa mujibu wa ikulu, ya Kenya mashauriano hayo kati ya Rais Kenyatta na Rais Trump yaliangazia zaidi nguzo nne ya ajenda kuu ya maendeleo ya Rais Kenyatta pamoja na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi nchini humo.

Haki miliki ya picha IKULU, KENYA

Viongozi hao wawili pia walijadiliana kuhusu safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York zitakazoanza mwezi Oktoba mwaka huu.

Walikubaliana kwamba safari hizo za ndege zitaimarisha zaidi utalii na biashara kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Walitoa mfano wa Mkataba wa Nafasi na Ustawi wa Afrika maarufu kama Mkataba wa AGOA kama moja wapo wa nyanja zitakazonufaika na safari hizo za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi.

Bi Melania anatarajiwa kukamilisha ziara yake barani Afrika nchini Misri.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii