Sheria ya Takwimu: Ni kweli Benki ya Dunia imezuia msaada wa $50m kwa Tanzania?

Rais John Magufuli Haki miliki ya picha IKULU, Tanzania
Image caption Tanzania imekuwa ikisifiwa mara kwa mara na Benki ya Dunia kuhusu uchumi wake

Kumekuwepo na taarifa kwamba Benki ya Dunia imezuia msaada wa Dola 50 milioni za Marekani ambao ulikuwa utolewe kwa serikali ya Tanzania.

Sababu iliyotolewa ni kwamba benki hiyo imeghadhabishwa na mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa kwenye Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Je, ni kweli?

Taarifa za kushikiliwa kwa msaada huo ambao ni sawa na takriban Sh112 bilioni za Tanzania zilitokea mara ya kwanza kwenye mtandao wa Eye on Global Transparency Jumatatu ambapo walinukuu taarifa kutoka kwa benki hiyo.

Lakini chanzo kinaonekana kuwa makala kwenye mtandao wa Center for Global Development, shirika ambalo linalijieleza kama asasi yenye kufanya utafiti maeneo mbalimbali duniani.

Azma kuu ya shirika hilo inaelezwa kuwa kupunguza umasikini duniani na kuboresha maisha ya watu kupitia utafiti katika fani ya uchumi na kuchangia utoaji wa sera mwafaka na kufanywa kwa maamuzi ya busara.

Image caption Jiji la Dar es Salaam

Mwandishi wa makala hiyo inayoitaka Benki ya Dunia kutotoa fedha hizo ni Justin Sandefur, ambaye kabla ya kujiunga na shirika hilo alihudumu kama mshauri wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) kwa miaka miwili, na pia aliwahi kuhudumu kama mtafiti katika kituo cha Utafiti wa Uchumi wa Mataifa ya Afrika, katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani.

Tanzania yalinganishwa na Argentina

Sandefur kwenye makala yake ameilinganisha Tanzania na Ugiriki na Argentina, ambapo anasema mataifa hayo yaliharamisha aina zozote za kukosoa takwimu za serikali kuhusu uchumi na masuala ya kijamii.

Anasema kuna tatizo kwamba serikali za mataifa mbalimbali hushawishika kuongeza chumvi kwenye takwimu rasmi ndipo waoneshe kwamba wanafanikiwa na kufanya kazi.

Mwandishi huyo anasema tatizo linakuwa mbaya zaidi pale asasi za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinatumia takwimu hizo kama taswira halisi ya hali nchini.

"Watanzania wa kawaida huenda karibuni wakakutana na takwimu zinazotolewa na Benki ya Dunia na IMF kuhusu taifa lao ambazo hawawezi kuzitilia shaka, kwa kuogopa kuchukuliwa hatua za kisheria," anasema.

Takwimu muhimu kuhusu Tanzania

6.5%

Kiwango cha wastani cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania 2004 hadi 2014

  • 28.2 % Kiwango cha umaskini kitaifa kufikia mwaka 2012

"Takwimu za serikali zilizoongezwa chumvi huendeleza dhana potofu kwamba viongozi wa kiimla huhakikisha ā€˛mambo yanatekelezwa," kwamba wanachapa kazi, na kwamba viongozi kama vile Dkt John Magufuli wa Tanzania wanafaa kwa maendeleo ya kiuchumi.

"Kanuni rahisi inafaa kufuatwa: ikiwa takwimu za serikali hazifai kukosolewa, basi haziwezi kuaminika. Kwa kanuni hii, Benki ya Dunia na IMF hawafai kunukuu takwimu za serikali ya Tanzania au kuzikubali kama za kuaminika - na wanafaa kuondoa mara moja mpango wao wa kutoa msaada kwa Tanzania kuisaidia kuandaa takwimu ambazo raia wake hawawezi kuzikosoa," amesema mwandishi huyo.

Nchini Ugiriki, mkuu wa takwimu wa zamani Andreas Georgiu alishtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za kupotosha kuhusu mapungufu kwenye bajeti la taifa hilo, akiwasilisha ripoti kwa Umoja wa Ulaya mwaka 2010.

Argentina pia iliwafuta kazi maafisa wa serikali waliokataa kutoa ushirikiano katika juhudi za kuchakachua takwimu rasmi za mfumko wa bei miaka ya 2000. Shirika moja huru la utafiti pia lilitozwa faini kwa kutoa takwimu za mfumko wa bei ambazo zilikuwa sahihi zaidi.

Mwaka 2013, IMF ilichukua hatua dhidi ya Argentina na kukataa kukubali takwimu zake rasmi kuhusu mfumko. Hatua hiyo iliifanya serikali ya Argentina kufanyia marekebisho takwimu zake kuhusu mfumko mwaka 2014 na ikabainika kwamba kiwango hicho kilikuwa kimeongezeka maradufu.

"Hilo ni funzo linaloweza kutumiwa ukiangazia kisa cha Tanzania," anasema Sandefur.

Benki ya Dunia imesema nini?

Benki hiyo imetoa taarifa ikisema imesikitishwa sana na marekebisho ya sheria yanayopendekezwa kufanywa kwenye Sheria ya Takwimu ya 2015.

Benki hiyo inasema sheria hizo haziendani na viwango vya kimataifa vilivyowekwa kuhusu takwimu.

"Tumeifahamisha serikali ya Tanzania kwamba marekebisho hayo, iwapo yatatekelezwa, huenda yakaathiri sana kuandaliwa kwa takwimu rasmi na zisizo rasmi, ambazo huwa muhimu sana kwa ustawi wa taifa lolote lile," benki hiyo imesema.

"Ni muhimu sana kwa Tanzania, sawa na taifa jingine lolote, kutumia sheria za takwimu kuhakikisha takwimu rasmi ni za kiwango cha juu zaidi na za kuaminika na pia kulinda uwazi na uwajibikaji katika matumizi yake, kuendeleza mjadala kwa manufaa ya raia."

Kutokana na hilo, benki hiyo imesema: "Benki ya Dunia inajadiliana na serikali kuhusu utoaji wa msaada zaidi katika kujenga mifumo ya takwimu endelevu unafaa kwa wakati huu."

Ingawa benki hiyo imesema mashauriano yanaendelea na kwamba wameeleza wasiwasi wake kuhusu sheria hiyo ya takwimu, haijasema wazi kwamba imesitisha mradi huo.

Kadhalika, kiasi hicho cha $50 milioni bado kimeorodheshwa kwenye tovuti ya benki hiyo kama msaada unaopangiwa kutolewa kwa Tanzania, ingawa mpango huo bado haujaidhinishwa, bado upo kwenye utaratibu.

Benki ya Dunia ilikuwa imetumia kiasi cha $ 63.18 milioni kama msaada kuimarisha uwezo wa mfumo wa takwimu wa serikali Tanzania kufikia Juni 30,2018 chini ya mradi ambao ulikuwa umeidhinishwa mwaka 2011.

Agosti, waliidhinisha kiasi kingine cha $ 8.56 milioni.

Serikali imekiri kunyimwa fedha?

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James aliliambia gazeti la Mwananchi kwamba hawatambui kuwepo kwa msaada wa aina hiyo.

"Serikali haijawahi kuomba wala kuwa kwenye mchakato wa kukopa Dola 50 milioni kwenda kwenye kazi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Mimi kama Katibu Mkuu nasema hatujawahi kuandika barua kuomba hizo fedha," Bw James alisema.

Sheria ya takwimu Tanzania inasemaje?

Mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Takwimu ulipitishwa Septemba 10 na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao, pamoja na mambo mengine, unakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu rasmi za serikali.

Adhabu ya kufanya hivyo ni faini ya Dola 6,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Kadhalika, mswada huo wa marekebisho ya sheria unapendekeza kila mtu, taasisi, shirika au kampuni binafsi inayokusudia kukusanya takwimu nchini Tanzania lazima ipate kibali cha Serikali kabla ya kuzichapisha.

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema ni kweli sheria hiyo ina kasoro nyingi na kwamba serikali haina nia njema.

"Hiyo sheria imetungwa na Serikali na kupelekwa bungeni, wabunge wakaipitisha, ni sheria mbaya. Ni mbaya kwa sababu sheria na takwimu zozote zitakazotolewa na Serikali ni msahafu."

Huwezi kusikiliza tena
Fatuma Karume: Tutaendelea kuikosoa serikali na kutetea haki Tanzania

Amesema Serikali haina nia njema na huenda kuna kitu inakificha nyuma ya sheria hiyo.

"Maana yake sasa Serikali itakuwa inatoa takwimu zisizopingwa. Kwa nini sheria na takwimu ziwe neno la Mungu?" aliambia gazeti la Mwananchi.

"Utaikosoaje Serikali bila kuwa na takwimu mbadala?."

Mada zinazohusiana