Rédoine Faïd: Jambazi aliyetumia helikopta kutoroka jela alivyokamatwa akiwa anavalia kama mwanamke

Picha ya Redoine Faid Haki miliki ya picha IBO/SIPA/REX/Shutterstock
Image caption Rédoine Faïd, picha ya mwaka 2010

Jambazi sugu aliyekuwa akisakwa nchini Ufaransa alifuatiliwa nyendo zake na polisi kwa njia ya simu na alikuwa akitumia burqa kujiificha, waendesha mashtaka wameeleza.

Redoine Faïd, 46, alikamatwa siku ya Jumatano baada ya kujificha kwa miezi mitatu kwenye mji ambao alikulia kaskazini mwa Paris, watu wengine sita pia wamekamatwa.

Alitoroka jela tarehe mosi Julai, akitumia helikopta iliyokuwa ikiendeshwa na rubani aliyekuwa ametekwa nyara.

Alitoroshwa gerezani huko Réau, kusini mashariki mwa Paris na watu watatu waliokuwa wamejihami vikali. Alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 25 kwa kupanga wizi uliofeli mwaka 2013 ambapo polisi mmoja aliuawa.

Alikamatwa muda mfupi baada ya saa kumi siku ya Jumatano kwenye mji wa Creil. Watu wengine watatu kwenye nyumba hiyo walikamatwa na wengine watatu wakakamatwa kwingine.

Mhalifu huyu alishikwa kwa njia gani?

Mwendesha mashtaka nchini Ufaransa alifichua kuwa polisi wamekuwa wakichunguza mawasiliano ya simu ya baadhi ya wanachama wa genge lililohusika katika kumtorosha gerezani. Pia polisi walikuwa wakifuatilia mawasiliano ya mwanamke mmoja huko Creil, ambapo Faïd alikulia.

Wikendi iliyopita mwanamke huyo alimuruhusu mtu aliyekuwa amevaa vali za wanawake wa Kiislamu burka ambaye maumbile yake yalionekana kuwa ya mwanamume aingie gari lake.

Siku ya Jumanne, mtu huyo kisha akatoka kwa gari na kuingia nyumba ya mwanamke huyo akifuatiwa baadaye na mtu mwingine ambaye pia alikuwa amevaa burka.

Polisi mara moja walishuku wawili hao waliokuwa wamevaa burka walikuwa Rédoine Faïd na ndugu yake Rachid.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rédoine Faïd aifuatwa hadi jengo hili lililo Creil

Mwendo wa saa 10:20 siku ya Jumatano kikosi cha polisi cha BRI kilivamia jengo hilo na kuwakamata ndugu hao wawili, akiwemo mpwa wao na mmliki wa nyumba hiyo.

Mpwa mwingine na washukiwa wengine wawili walikamatwa kwingine.

Picha zimeibuka za mtoro huyo akiwa ameketi kitandani akizungukwa na polisi huki bunduki ikiwa sakafuni.

Rédoine Faïd ni nani?

Ni mhalifu sugu aliyekulia kwenye mtaa ulio karibu na mji mkuu Paris miaka ya sabini na themanini. Faïd alipata umaarufu mkubwa nchini Ufaransa miaka ya hivi karibuni licha ya kuhusika katika uhalifu.

Miaka ya 1990 aliongoza genge lililohusika kwenye visa vya wizi wa kutumia nguvu na ulaghai na kusema kuwa filamu za Hollywood kama vile Scarface ya mwigizaji maarufu Al Pacino, zilichangia kwa maisha yake hayo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rédoine Faïd alirodheshwa kama mtu aliyekuwa akitafutwa sana na polisi wa Interpol mwaka 2013

Wakati wa shambualo la mwaka 1997 dhidi ya gari la maafisa wa usalama, yeye na washirika wake walitumia kofia za kipa wa mpira wa magongo wakiiga genge la Robert de Niro kwenye filamu ya Heat.

Baadaye alikuja kusema kuwa alikuwa ametazama filamu mara miaka kadhaa na wakati mmoja alimuambia mwelekezi wake wakati wa tamasha ya filamu huko Paris kuwa "Ulikuwa mshauri wangu wa kiufundi".

Umaarufu wake ulisaidiwa na kitabu cha mwaka 2009 kilichoelezea maisha yake akiwa mdogo kwenye mitaa ya Paris na jinsi aliingia katika maisha ya uhalifu.

Baada ya uvamizi uliofeli kwa gari la ulinzi lililokuwa linasafirisha pesa mwaka 2010 ambapo polisi mwanamke aliuawa, alirudi gerezani lakini akatoroka mwaka 2013 kwa kuwateka nyara polisi wanne walinzi wa gereza na kilipua milango na vilipuzi. Wakati huo alikaa mafichoni kwa muda wa wiki sita.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Faid alitoroka kutoka gereza la Sud-Francilien nje ya Paris

Maisha ya Redoine Faid

  • Maisha ya Faid ya kufungwa jela na kutoroka yalianza mwaka 1998 kutokana na makosa ya wizi wa kutumia nguvu na kupora benki.
  • Mwaka 2009 aliachiliwa kwa msamaha akiapa kuwa alikuwa amebadilika lakini ilipofika mwaka 2011 alikuwa amekiuka makubaliano ya kuachiliwa kwake na akarudishwa korokoroni.
  • Mwaka 2017 Faid alihukumiwa miaka 10 baada ya kutoroka jela ya Séquedin, mwaka 2013 nje ya mji wa Lille. Pia alihukumiwa miaka 18 kwa kupanga wizi mwaka 2010 ambapo polisi mmoja Aurélie Fouquet, aliuawa.
  • Faid alishindwa katika rufaa aliyoikata na Aprili mwaka 2018 alihukumiwa kifungo zaidi cha miaka 25 kwa wizi. Alikuwa akitumikia kifungo hicho wakati wa kisa cha hivi majuzi cha kutoroka jela
  • Alizaliwa mwaka 1972 na kukulia maeneo yenye visa vya uhalifu mjini Paris.
  • Miaka ya 1990 aliongoza genge lilohusika kwenye wizi na kupora watu mjini Paris.
  • Mmoja wa wasimamizi wa hivi punde wa Faid gerezani alisema - hakuwa na mzozo wowote na walinzi lakini tulikuwa na hofu kila wakati.
Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Helikopta iliyotumiwa na Faid baadaye ilipatikana vichakani Gonesse, kaskazini mwa Paris

Usalama zaidi waahidiwa

Kwa mamlaka za Ufaransa visa vya Faïd kutoroka jela vimekuwa ni aibu na waziri wa sheria Nicole Belloubet amesema hilo haliwezi kufanyika tena. Tutamweka eneo lenye ulinzi mahala ambapo atakuwa akitazamwa kwa karibu sana.

Taarifa za kukamatwa kwake zilijiriu wakati wa taarifa za kujiuzulu kwa waziri wa mambo ya ndani Gérard Collomb ambaye alitangaza uamuzi huo wake Jumane usiku.

Hatua hiyo inaonekana kama pigo jipya kwa rais Emmanuel Macron ambaye umaarufu wake umeshuka wiki za hivi karibuni.

Kwa nini raia wanapenda wahalifu nchini Ufaransa?

Wakati Rédoine Faïd alitoroka jela mwezi Julai, mwanafilamu Béatrice Dalle alifurahia sana.

"Mungu akulinde wewe Rédoine," aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram. Ufaransa yote iko na wewe. Nitacheza ngoma kwa saa kadhaa kusherehekea."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wakati Rédoine Faïd alitoroka jela mwezi Julai, mwanafilamu Béatrice Dalle alifurahishwa.

Mwanafilamu huyo aliyafuta hayo tena wakati ilitangazwa kuwa shujaa wake alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 25 kwa wizi ambapo polisi aliuawa kwa kupigwa risasi.

Lakini hata hivyo, nchini Ufaransa kawaida kuna kitu fulani kuhusu uhalifu. Hasa kwa yule ambaye hupenda kutoroka jela. Na pia kwa mwenye hufanya uhalifu wake akiiga filamu za Hollywood.

Hususan kwa yule ambaye atapiga hatua zaidi za kuandika kitabu na kupata umaarufu kwenye televisheni.

Rédoine Faïd alifanya hayo yote.

Wengine waliopata umaarufu kama Jacques Mesrine, Tany Zampa, François le Belge hawakuwa tu wezi wa benki bali pia wauaji.

Labda ya hili limetokana na historia ya Ufaransa ya mapinduzi ambayo yalihalalisha vitendo vya kuwapora matajiri.

Rédoine Faï si mhalifu wa kwanza kuonyesha tabia za Robin Hood aliye msafi lakini anayeendesha ghasia wakati unaohitajika.

"Hakuna kujeruhiwa, hakuna kuua," yalikuwa maneno yake, wakati mtu hajeruhiwi, unajua unafanya kazi yako vizuri, aliandika kwenyr kitabu chake.

Wafaransa wana utamaduni wa filamu za za uhalifu. Kwa mfano zile Rififi, Classe Tous Risques, Touchez pas au Grisbi, Les Tontons Flingueurs - na ya hivi punde zaidi Masrine.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii