Je, ni kweli kwamba Magufuli anawataka wanaume Tanzania waoe wake wengi?

  • Peter Mwai
  • BBC Swahili

Kwa siku kadha sasa, taarifa zimekuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii kwamba Rais wa Tanzania John Magufuli amewataka wanaume nchini Tanzania kuoa zaidi ya mke mmoja.

Taarifa hizo zinadai kwamba kiongozi huyo amependekeza hilo kama suluhu ya kupunguza ukahaba miongoni mwa wanawake wa Tanzania.

Je, kuna ukweli wowote kuhusu madai hayo? Taarifa hizi zilianza wapi na zinadai nini?

Chanzo cha taarifa na je Wakenya wanahusika?

Taarifa ya sasa ambayo imekuwa ikisambazwa sana imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na kuchapishwa katika mtandao wa nipasheonline.com, mtandao ambao bila kuwa makini huenda ukadhani una uhusiano na gazeti la Nipashe la nchini Tanzania ambalo huchapishwa na ippmedia. Kampuni hiyo huchapisha pia gazeti la Jumapili kwa jina Nipashe Jumapili.

Hata hivyo ippmedia haina uhusiano wowote na mtandao huo. Taarifa zake za Kiswahili hupakiwa katika tovuti yeye jina ippmedia.com/sw, mtandao ambao umekuwepo tangu mwaka 1998.

Hii Nipashe basi ni ya wapi?

Uchunguzi wetu umebaini kwamba tovuti hii imesajiliwa na mhudumu wa mtandao aliyepo jijini Nairobi. Mtandao huo ulisajiliwa mara ya kwanza Agosti mwaka 2017. Hivyo basi ni mtandao ambao umekuwepo kwa mwaka mmoja hivi.

Kuna jambo la kushangaza pia kuhusu taarifa hiyo kwani haijachapishwa wiki hii.

Iliandikwa mara ya kwanza Februari mwaka huu na kusambazwa kwa kiwango fulani ingawa wakati huo watawala hawakufikia kuchukua hatua.

Uchunguzi wetu umedokeza kwamba mtandao huu wa nipasheonline.com huenda ulitafsiri taarifa hii kutoka kwa mtandao mwingine, mtandao ulio na taarifa ya mapema zaidi ukiwa mtandao wa zambianobserver.com ambao ulichapisha taarifa hiyo mnamo 10 Februari, ambapo haina hata mwandishi. Taarifa hiyo baadaye ilichapishwa na cajnewsafrica.com, ambao wanaonekana kuongeza na kutoa kidogo na baada ya hapo wengine wanaonekana kuichukua.

Taarifa iliyo katika nipasheonline.com inafanana sana na hiyo ya cajnewsafrica.com, ambao walichoacha pekee ni mstari mmoja pekee wa mwisho.

Maelezo kuhusu mtandao huo wa zambianobserver hayapatikani, kidokezo pekee kikiwa kwamba umesajiliwa na mtu ambaye anwani yake ipo Kirkland katika wilaya ya King jimbo la Washington nchini Marekani.

Kuna uwezekano kwamba taarifa ya nipasheonline.com imevma zaidi kutokana na hali kwamba iliandikwa kwa Kiswahili na kusambazwa katika majukwaa kama vile JamiiForums ambapo Watanzania wengi wanachangia.

Maswali chungu nzima kwenye taarifa

Taarifa iliyopakiwa kwenye mtandao huo ina masuala kadha ambayo yanatilia shaka uhalali wake.

Kwanza, si kawaida kwa Rais Magufuli kuzungumzia kuhusu ukahaba hadharani.

Kwa kudai Rais Magufuli alisema 'wanawake wengi ambao hawajaolewa wanalizimika kushiriki uasherati na waume za watu kwa sababu kuna ukosefu wa wanaume wa kuwaoa', utakuwa unaashiria kwamba kiongozi huyo anawahukumu raia wake.

Taarifa hiyo inadai tatizo linatokana na wingi wa wanawake ukilinganisha na wanaume, ambapo inadai kuna kuna wanawake milioni 40 kwa wanaume milioni 30.

Hiyo itaifanya idadi ya jumla ya Watanzania kuwa milioni 70. Ukweli ni kwamba makadirio yanayotumiwa kwa sasa ni kwamba idadi ya watu Tanzania ni milioni 59.

Hakuna tofauti kubwa kati ya idadi ya wanawake na idadi ya wanaume nchini humo kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania.

Makadirio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania

  • Idadi ya Jumla 2018: 54,199,163
  • Wanaume: 26,510,095 (48.9%)
  • Wanawake: 27,689,068 (51.1%)

Makadirio rasmi ya idadi ya watu Tanzania hufanywa kwa kutumia Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 kwa kutumia mbinu za kidemografia zinazohusisha mabadiliko katika viwango vya uzazi, vifo, uhamaji na uhamiaji.

Rais Magufuli anadaiwa pia kutoa tamko hilo katika "mkutano wa wanaume 14,000 ambao walipokea mafunzo katika nyanja tofauti mjini Dar es Salaam".

Watu 14,000 kuwaleta pamoja ni idadi kubwa sana ya watu. Ilikuwaje wanaume hao wakakutanishwa na tamko kama hilo kutolewa bila vyombo vingine vya habari kufahamu? Kwa kukadiria, hebu fikiria darasani mlikuwa wangapi, kisha ufanye hesabu utapiga mara ngapi ufikie idadi hiyo.

Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kwa kawaida kiwango chake ni kutoshea watu 23,000. Kwa idadi hii ya wanaume, wangekuwa wamepita nusu.

"Siwalazimishi, lakini ninawashauri kuoa wake wawilia au zaidi ili kupunguza idadi ya wanawake wasio na waume," anadaiwa kusema rais Magufuli siku hiyo, lakini baadhi wamekuwa wakijiuliza kama ni kweli alitoa kauli hiyo, mbona mwenyewe hajaoa zaidi ya mke mmoja?

Serikali ya Tanzania imesema nini?

Msemaji Mkuu wa Serikali ameshutumu taarifa hizo na kusema ni "uzushi na uhalifu wa kimtandao."

"Mhe. Rais hajawahi kuzungumzia jambo hili mahali popote. Lipuuzeni!!!

Baadhi ya waliochangia ujumbe huo wamekuwa wakitoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchukua hatua.

"Wenye chuki na raisi wetu wanazusha sana mambo kwakweli.Naomba wakibainika Washughulikiwe iwe fundisho kwa wazushi wenzao," ameandika Danny Nduhije.

Rashid Dile amesema: "Sjawai kuisikia habari hii tuombe mamlaka ishighulike na hili."

Samwel Gasaya: "Hii kitu imetrend sana na nimeuliza sana kuwa alisema lini na wapi hakuna jibu ila wanavyoipa promo si mchezo".

Rizick kessy: "Hivi mtu anaweza kumchafua kiongozi wa nchi hivi???."

Jonathan Ntala anawataka watu kuwa wazalendo : "Tatizo wengi tunapenda kuchukua kauli fulani za Mh. Rais na kuzigeuza geuza!

Tuweni wazalendo!"

Magoko naye akaandika: "Shida ya watu ni kukuza maneno yasiyo na maana duniani ,

Mh Rais alishawahi sema,hata MTU ukitembea kwenye maji watu watakuambia unatutimulia vumbi."

Robert Steven hata hivyo anasema yeye hana shaka na madai hayo.

"Mh. Huwa anaongeaongea mambo mengi mimi sina shaka na hili. Hata akisema kwani lina athari na uchumi wa nchi hii au technology," ameandika.

"Sheria ya Uhalifu wa kimtandao imeanzishwa kumkinga mh. Raisi tu........ Hata penye ukweli mpinzani hana haki... Kumbe tusiwe tunahoji ni bora liende."

Lakibug, anaamini habari za uzushi ni jambo la kawaida, suluhu ni kuzoea: "Fake news ni jambo lilokuja na social media, jaribuni kuzoea, mbona Trump hatishi tishi watu wanaomtungia fake news kila wakati? Anajiamini anapiga kazi.."

Mchungaji wa Ghana

Kuna video ambayo imekuwa ikisambaa pia ikimuonesha mchungaji mmoja wa Ghana akinukuu taarifa hizo zinazodaiwa kutolewa na Rais Magufuli kana kwamba ni za kweli.

Alikuwa akichangia mjadala kuhusu kuwaoa wake wengi na pia akitangaza kitabu chake.

Wakusnooz aliiona, na kuandika: "Kuna video moja nimeiona kuna majamaa wa ghana wanazungumza kuhusu idadi ya watu mpaka 2025 Tz wanawake watakuwa wengi kuliko wanaume na wakamtaja Raisi kasema inabidi tuoe zaidi ya mmoja".

Lakini amejibiwa na Roseenvelt: "Mkuu huu ni ulimwengu wa fake fake fake news!!! Magu atasingiziwa mengi sana!!! Kama ile ya kuhama dar ikifika july."

Pauline Mandari amezungumzia hilo kwenye Twitter: "Kama unalosema (Msemaji wa Serikali) ni kweli, huyu mchungaji wa huko Ghana haya maelezo anayoyaelezea kwenye tv shows zao kuhusu hilo unalolipinga wewe, je yeye haya maelezo aliyatoa wapi?."

Anataka mchungaji huyo ashtakiwe au arudi kwenye kipindi hicho na kuomba radhi.

"Na kama kweli raisi hajawahi kusema hivyo mahali popote basi mumtafute huyu mchungaji na kumpeleka mahakamani kwa kuharibu jina la raisi. Aeleze hayo maneno aliyatoa wapi? La sivyo arudi kwa hizo shows na kusema raisi of Tanzania is not begging ppl to take more than one wife," ameandika Pauline Mandari kwenye Twitter.