Tuzo ya Amani ya Nobel 2018: Raia wa DRC Denis Mukwege ashinda kwa pamoja na Nadia Murad

Bw Mukwege ni mtaalamu wa majeraha mabaya kwenye viungo vya uzazi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Mukwege ni mtaalamu wa majeraha mabaya kwenye viungo vya uzazi

Raia wa DRC Denis Mukwege ashinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa juhudi zake kukabiliana na udhalilishaji wa kingono nchini humo.

Denis Mukwege ni mtaalamu wa masuala ya uzazi ya wanawake ambaye amekuwa akifanya kazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Yeye na wenzake wamewatibu na kuwafanyia upasuaji wa kurekebisha viungo maelfu ya waathiriwa wa udhalilishaji wa kingono, wengi ambao walidhalilishwa vitani.

Mukwege ametunukiwa tuzo hiyo pamoja na Nadia Murad.

Kamati ya Nobel imesema yeye "ni mmoja wa wasichana na wanawake takriban 3,000 wa jamii ya Yazidi ambao ni waathiriwa wa ubakaji na udhalilishaji wa kingono uliotekelezwa na wapiganaji wa Islamic State."

Bi Murad alishiriki kama sura ya vita vya kupigania kukombolewa kwa watu wa jamii ya Yazidi na kukabiliana na ulanguzi wa watu baada yake kufanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa IS Novemba 2014.

Tuzo hiyo huwa na zawadi ya takriban £700,000 ($1.1m; €950,000).

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bi Murad alishiriki kampeni ya kutetea kuchailiwa kwa Yazidi waliokuwa wametekwa

Berit Reiss-Andersen, mwenyekiti wa kamati ya Nobel, amesema wawili hao walikuwa muhimu sana katika kukabiliana na uhalifu huo.

Watu binafsi na mashirika 331 walikuwa wamependekezwa kushindania tuzo hiyo mwaka huu.

Washindi wametangazwa mjini Oslo na Bi Reiss-Andersen amesema wameshinda kwa "juhudi zao katika kupigania kumaliza matumizi ya udhalilishaji wa kingono kama silaha vitani."

Mapema wiki hii, tuzo ya Nobel ya Fizikia ilitunukiwa Donna Strickland, mwanamke wa tatu kuwahi kushinda tuzo hiyo na mwanamke wa kwanza kushinda katika kipindi cha miaka 55.

Raia huyo wa Canada alitangazwa mshindi pamoja na Mmarekani Arthur Ashkin na Mfaransa Gerard Mourou.

Tuzo ya Nobel ya Matibabu ilikabidhiwa wanasayansi wawili - Prof James P Allison kutoka Marekani na Prof Tasuku Honjo kutoka Japan - waliogundua jinsi ya kutumia mfumo wa kinga mwili kukabiliana na saratani.

Mukwege alivyoanzisha kampeni yake

Haki miliki ya picha AFP

Denis Mukwege ni daktari anayeshughulikia afya ya wanawake nchini DRC. Yeye na wenzake walikuwa wamewahudumia waathiriwa 30,000 wa ubakaji kufikia mwaka 2013.

Anasema: "Nilijiuliza - ni nini haswa kilikuwa kinaendelea? Huu ulikuwa tu si uhalifu bali mikakati mahsusi. Kuna wakati ambapo watu wengi wangebakwa kwa mpigo, tena wazi mbele ya watu wengine - kijiji kizima kingebakwa usiku. Basi wanapofanya hivyo hawaumizi tu wanaowabaka bali jamii nzima inayolazimishwa kuwatizama.

Vita Mashariki mwa DRC vimewalazimisha mamia kutoroka makwao hali inayohatarisha maisha yao

Kuna wakati waliobakwa hujaza vitanda vyote 350 vya hospitali ya Denis Mukwege. Mradi huu wa daktari Mukwege unafadhiliwa na shirika la kuwahudumia watoto la Unicef na wahisani wengine.

Waathiriwa pia hutibiwa katika zahanati inayohamishwa hamishawa na ambayo pia inafadhaliwa na wahisani hao hao.

Anasema wanawake wangejipeleka hospitalini wakiwa wamebakwa, na kujeruhiwa sehemu zao nyeti au kupigwa risasi au hata kumwagiwa kemikali.

"Mnamo 2011, visa hivi vilipungua. Tukadhani kwamba msimu huu mbaya ulikuwa unafika ukingoni. Kumbe wapi kwa sababu tangu mwaka uliopita wakati vita vilianza tena, visa hivi vikaanza kuongezeka tena. Yaani ni hali ambayo inaandamana na vita," alisema Mukwege.