Muktaar Robow: Mkuu wa zamani wa Alshabab azuiliwa kuwania uongozi Somalia

Mukhtaar Roobow anayejulikana pia kama Abu Mansur Haki miliki ya picha SBC
Image caption Mukhtaar Roobow anayejulikana pia kama Abu Mansur

Komanda wa zamani na mwanzilishi wa kundi la wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia ,Mukhtar Robow, amezuiliwa kuwania uongozi serikalini.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, wizara ya usalama imesema kuwa bwana Robow hawezi kuwania wadhifa wowote serikalini kwasababu bado anakabiliwa na vikwazo vya kisheria.

Taarifa hiyo imetolewa siku moja baada ya Robow kutangaza kuwa atawania uraisi wa jimbo la kusini magharibi katika ichaguzi ujao wa kimaeneo.

Mukhtaar Robow amesema uamuzi wake wa kuingia katika siasa unafuatia wito wa wananchi, wafuasi wake katika jimbo hilo la kusini magharibi.

Amedhihirisha kwamba yupo tayari iwapo atashinda, kuidhinisha uhusiano thabiti na serikali ya shirikisho katika mji mkuu Mogadishu, ambayo imekuwa katika mzozo na tawala za baadhi ya majimbo.

Lakini Robow ni nani?

Haki miliki ya picha SBC
Image caption Mukhtaar Robow

Bwana Robow alikuwa naibu kiongozi wa al-Shabaab na msemaji wa kundi hilo la wapiganaji wa kiislamu.

Mnamo mwaka 2000 alipata mafunzo katika kundi la kijihadi la al-Qaeda nchini Afghanistan.

Alijitoa katika al-Shabab mnamo 2012, kutokana na alichokitaja kuwa ni tofuati za mawazo na fikra.

Alijisalimisha pamoja na wapiganaji wake katika mji ulio kusini magharibu wa Hudur.

Baadaye aliliunda kundi lake la wanamgambo waliopigana vita dhidi ya Alshabaab.

Mnamo Juni mwaka jana,kufuatia taarifa kwamba Robow anashirikiana na serikali ya Somalia,Wizara ya mambo ya nje ilimuondoa katika orodha ya magaidi na kufutilia mbali kitita cha dola milioni 5 iliyokuwa imeahidi kwa yoyote atakayesaidia katika kukamatwa kwa Robow.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanaume mmoja akihuzunika karibu na maiti katika eneo ambapo bomu lililipukia jijini Mogadishu Oktoba 14, 2017

Je Robow ana nafasi gani ya kupata uongozi serikalini?

Mwandishi wa BBC Bashkas Jugosdaay anasema kuna mgawanyiko.

Kuna kundi linalomtazama na sura ya uovu unaotekelezwa na Alshabaab uliochangia vifo vya maelfu ya watu.

Hilo ni donda ambalo daima kovu yake itasalia na kwa hivyo huenda ikawa vigumu kwake kupata uungwaji mkono kikamilifu.

Na kuna upande wa pili ambao wanatazama faida inayotokana na kujisalimisha kwake na kutoa ushirikiano kwa serikali kuu ya Somalia katika kusaidia kupambana na kundi hilo la wapiganaji wa kiislamu.

Hivyo basi matumiani ni kwamba huenda faida ikaongezeka na pengine ndio anastahili kupata uongozi huo. Na kama anavyoeleza mwenyewe Robow, wapo watu waliomshinikiza kuwania uongozi, pengine ndio hakikisho la uungwaji mkono wake.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo

Usalama bado ni mtihani mkuu kwa utawala wa Somalia

Miezi michache baada ya kutwaa urais wa Somalia kutoka uwanja wa ndege kwa kuhofia mashambulio ya Al Shabaab, Mohamed Abdullahi alitoa ahadi yake kwa wananchi wa Somalia.

Alisema, 'Lengo langu ni kuwashinda Al Shabaab kwa miaka miwili ijayo. Natumai kwamba tukifanya kazi pamoja, tutaleta Amani na utulivu nchini Somalia'.

Lakini uongozi wake umeshuhudia mashambulio, na Mogadishu ingali mojawapo wa miji hatari zaidi duniani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii